Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, amepinga kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo kwa kusikiliza ushahidi wa shahidi fiche wa Jamhuri.
Kesi hiyo, inayosikilizwa katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha kutoka Mahakama Kuu Songea na Ferdinand Kiwonde kutoka Mahakama Kuu Bukoba, ilitarajiwa kuendelea leo Jumatano, Novemba 12, 2025.
Leo, upande wa mashtaka ulimpeleka shahidi wa nne katika kesi hiyo, ambaye ni miongoni mwa mashahidi fiche wa Jamhuri (shahidi anayetoa ushahidi bila kuonekana mahakamani).
Mashahidi hao fiche ni raia wa kawaida (wasio askari) ambao Mahakama Kuu iliamuru wapewe ulinzi kutokana na maombi ya Jamhuri, kwa madai kuwa wamekuwa wakitishiwa usalama wao.
Mahakama hiyo, katika uamuzi uliotolewa na Jaji Hussein Mtembwa Agosti 4, 2025, ilielekeza mashahidi hao majina yao yasitajwe, wala anuani za makazi au taarifa zinazoweza kuwafanya watambulike wao, familia zao au watu wao wa karibu.
Pia, ilizuia kusambazwa kwa maelezo yao au nyaraka zozote zinazohusu mashahidi hao zinazoweza kusababisha watambulike bila idhini ya mahakama, huku ikielekeza watumie majina bandia wakati wote wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Jamhuri iliwasilisha mahakamani maombi ya ulinzi wa mashahidi hao chini ya Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi za Mwaka 2025 zilizotungwa na Jaji Mkuu, kwa mujibu wa kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Wakati kesi hiyo ilipoitwa leo Jumatano, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga, aliieleza mahakama kuwa wana shahidi mmoja, ambaye ni miongoni mwa mashahidi fiche waliopewa ulinzi, na wamempa jina la P11.
Kutokana na hali hiyo, shahidi huyo alikuwa katika kizimba maalumu kilichotengenezwa ndani ya ukumbi wa Mahakama ya wazi namba moja, ambamo hawezi kuonekana hata wakati akiingia, isipokuwa kusikika sauti yake pekee.
Baada ya taratibu za awali kukamilika, zikiwemo utambulisho wa mawakili na mshtakiwa na taarifa ya hali ya kesi, Jaji Ndunguru alimwuliza shahidi huyo kama yuko tayari, naye akajibu kuwa yuko tayari.
Hata hivyo, Lissu alisimama na kuieleza Mahakama kuwa anapinga shahidi kutoa ushahidi akiwa ndani ya kizimba hicho chenye kiboksi na badala yake, alitaka asimame katika kizimba cha wazi, si kwa shahidi huyo tu bali kwa mashahidi wote waliopewa ulinzi huo.
Katika pingamizi hilo, Lissu alitoa hoja sita kupinga shahidi huyo na wengine wa aina hiyo kutoa ushahidi wakiwa mafichoni katika kizimba hicho.
Amefafanua kuwa, kwa mujibu wa kanuni hizo, kiboksi hicho kinaitwa kizimba maalumu cha ushahidi kimetafsiriwa katika kanuni ya 3 kuwa ni sehemu ya kusimama au kukaa wakati wa kutoa ushahidi ili kumwezesha shahidi kutoa ushahidi bila kuonekana, isipokuwa kwa Jaji au Hakimu.
“Swali langu waheshimiwa majaji, shahidi hapo mlipo mnaweza kumuona? Mimi simuoni lakini kwa jinsi kilivyo hapo mlipo ninyi mnamuona? Kwa kuangalia kwa macho tu jinsi kilivyo hapo alipo hamuwezi kumuona.
“Kwa hiyo, shahidi amefichwa kwenu ninyi, kwa mshtakiwa na kwa wanaotazama. Watu pekee wanaomfahamu ni upande wa mashtaka. Hicho si kizimba maalumu cha shahidi,” amesema Lissu.
Katika hoja ya pili, Lissu amedai shahidi huyo hajabainishwa katika maombi ya ulinzi yaliyopelekwa mahakamani.
Amesema, kwa mujibu wa kanuni ya 5(1), Mahakama inaweza kutoa amri ya ulinzi iwapo itaridhika kuwa mtu aliyebainishwa katika maombi ni shahidi katika shauri hilo na maisha yake au usalama wake uko hatarini.
Amedai mtu aliyebainishwa ni yule aliyetajwa, lakini katika maombi ya ulinzi yaliyopelekwa mahakamani, hakuna hata moja kati ya viapo vilivyowasilishwa vinavyomtaja shahidi yeyote.
“Kwa hiyo katika orodha ya mashahidi wote wanapigwa wamepewa amri hakuna hata mmoja ambaye jina lake makazi yake yalipelekwa kwa Jaji Mtembwa, hakuna. Vilevile hakuna waliokuwa wanawatishia kwenye hizo affidavits, wala vitisho vya aina gani, hakuna,” amesema Lissu.
Katika hoja ya tatu, Lissu amedai hakuna mahali ambapo Mahakama ilitoa amri ya matumizi ya kizimba maalumu, na upande wa mashtaka haukuomba hilo.
Ameirejelea hati ya maombi ya ulinzi ya Jamhuri, akisema hawakuomba matumizi ya kizimba maalumu na Mahakama haikutoa amri hiyo.
“”Hawakuomba na matumizi ya kizimba maalumu na mahakama haikuitoa amri kuwaruhusu kutumia kizimba maalumu wanakujaje kutumia hapa? Kwa hiyo, hawawezi kupata kile ambacho hawakukiomba,” amesema Lissu.
Katika hoja ya nne, amedai matumizi ya kizimba maalumu yanaathiri haki ya kusikilizwa kwa usawa kinyume na kanuni ya 6(2) na 5(f).
Amehoji shahidi akitoa ushahidi kwenye kesi kubwa kama hiyo bila mahakama kumfahamu wala mashtakiwa isipokuwa waendesha mashtaka hiyo inawezaje kuwa usikilizwaji wa haki na Mahakama itatoaje uamuzi wa haki.
Amedai maslahi ya haki si suala la kanuni tu bali ni msingi wa utendaji wa Mahakama yoyote kwa mujibu wa Katiba ya Ibara ya 13(6)(a) na 107(A)(2)(a).
“Kwa hiyo, waheshimiwa majaji kumruhusu shahidi atoe ushahidi kwenye hicho kizimba si tu kukanyaga kanuni, bali ni kukiuka misingi ya utoaji haki ya Katiba yetu.
“Mahakama hii isije ikajiruhusu kukanyaga misingi ya haki ya Katiba yetu, waheshimiwa majaji msije mkakubali katika mazingira haya niliyoyasema kutumika kuharibu utendaji haki,” amesema Lissu.
Katika hoja ya tano, Lissu amedai sheria inayotoa ulinzi wa mashahidi, ambayo ndiyo chanzo cha kanuni hizo, ni batili kwa kuwa haijawahi kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.
Amesema kanuni hizo zilichapishwa Julai 11, 2025, wakati kesi hiyo ilianza Aprili, miezi mitatu kabla na kanuni hizo na kwamba ndizo zinaleta mgogoro.
Amedai sheria inaanza kutumika siku inapochapishwa au tarehe nyingine yoyote na kwamba haiwezi ikaanza kutumika kwa kurudi nyuma, hivyo haiwezi kutimika katika kesi yake kwa sbabau aliposhtakiwa haikuwepo.
Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 7 ya Mwaka 2018, iliyoongeza kifungu cha 194 cha CPA kuhusu ulinzi wa mashahidi, haijawahi kuchapishwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali.
Amesema, kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Tafsiri ya Sheria, sheria inaanza kutumika baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
Amedai kuwa sheria inapotangazwa kwenye Gazeti la Serikali itaonekana katika tovuti ya Serikali, ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Rais Utumishi, ya Mahakama na ya Bunge.
Pia amedai nakala ngumu (hardcopy) hupatikama kwenye kila maktaba ya Mahakama Kuu ya Ofisi ya AG, na katika Duka la Vitabu vya Serikali Dar es Salaam na Dodoma, Maktaba ya Bunge Dar es Salaam na Dodoma, na katika Hansard za Bunge, lakini huko kote haipo.
Katika hoja ya sita, amedai wakiruhusu utaratibu huo, hawataweza kudhibiti matumizi mabaya ya taratibu za Mahakama, kwani haijulikani shahidi huyo ni nani, kama anasoma ushahidi au kama anatumiwa ujumbe.
Ametolea mfano kesi moja ambayo watu 14 walihukumiwa kunyongwa bila kumuona shahidi, na mmoja alipoulizwa amewahi kutoa ushahidi mara ngapi, alijibu “mara tano.”
Julai 30, 2025, wakati kesi hiyo ikiwa hatua ya uchunguzi wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lissu alipinga pia matumizi ya kanuni hizo na akaahidi kuzishitaki Mahakama ya Rufani.
Baada ya Lissu kumaliza hoja zake, Wakili Katuga aliomba muda wa kuandaa majibu ya hoja hizo. Hata hivyo, kwa kuwa leo ilikuwa mwisho wa kikao cha usikilizwaji, kesi imeahirishwa hadi tarehe itakayopangwa, ambapo Jamhuri itajibu hoja za Lissu.