Maandamano ya Oktoba 29 Hayakuwa Halali, TPBA Yatamka – Global Publishers

Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kimetoa tamko rasmi kuhusu matukio yaliyojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025, kikisisitiza umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria, wajibu wa raia, na mipaka ya matumizi ya haki za binadamu.

Kupitia tamko lililotolewa leo, TPBA imesema kimechunguza taarifa na tuhuma mbalimbali kutoka taasisi na mashirika ya haki za binadamu, na kusisitiza kuwa haki na uhuru wa mtu binafsi lazima vitumike bila kuathiri usalama wa taifa au kuvunja haki za wengine. Chama hicho kimezingatia Ibara ya 30(1) ya Katiba, inayosema haki za binadamu hazitumiwi kwa namna inayosababisha kuingiliwa kwa haki za wengine au kuvuruga maslahi ya umma.

TPBA imesema kuwa maandamano yaliyofanyika Oktoba 29 hayakuwa halali kisheria kwa kuwa yalikiuka zuio lililotolewa na Jeshi la Polisi, na baadhi yaligeuka vurugu, yakihusisha uharibifu wa mali, mashambulizi kwa askari, na uchomaji wa vituo vya kupigia kura.

Kuhusu tuhuma za matumizi ya nguvu kupita kiasi na vifo vilivyotokea, TPBA imesisitiza kuwa silaha au risasi ni hatua ya mwisho inayoruhusiwa kisheria pale mbinu nyingine zote zikishindikana. Chama hicho pia limeongeza kuwa uwajibikaji wa vyombo vya dola ni sehemu ya utawala wa sheria, na uchunguzi unapaswa kufanyika pale panapotokea tuhuma za matumizi ya nguvu za ziada, kama ilivyoagizwa na Rais wakati wa hotuba yake ya uapisho Novemba 3, 2025.

Aidha, TPBA imesema hatua za kudhibiti au kusitisha mawasiliano kwa muda wakati wa uchaguzi zinaidhinishwa kisheria pale zinapolenga kulinda usalama wa taifa au kuzuia uvunjifu wa amani. Chama hicho pia kimeonya vyama vya siasa na taasisi zinazohusishwa na vurugu kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 20(2) ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vinavyoshiriki au kushinikiza uvunjifu wa amani vinaweza kufutwa usajili na viongozi wake kuwajibishwa kisheria.