Dodoma. Wakati jina la Waziri Mkuu mpya wa Tanzania likitarajiwa kutangazwa kesho bungeni, baadhi ya wabunge wameeleza matarajio yao kuhusu aina ya kiongozi wanayemtamani kushika wadhifa huo.
Wengine wamesema wanatamani apatikane Waziri Mkuu mwenye sifa kama za hayati Edward Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa sita wa Tanzania.
Akizungumza kuhusu suala hilo leo Jumatano Novemba 12, 2025 bungeni jijini Dodoma, Mbunge wa Newala Mjini mkoani Mtwara, Rashid Mohamed Mtima amesema Waziri Mkuu ni mhimili muhimu wa Serikali.
“Mimi binafsi natamani tupate Waziri Mkuu ambaye atahakikisha utumishi wa umma unafanya kazi kwa ufanisi ili wananchi wetu majimboni waweze kuhudumiwa ipasavyo.
“Tunatamani Waziri Mkuu ambaye ataweza kushuka hadi kwenye halmashauri na wakala mbalimbali kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo,” amesema.
Mbunge huyo amesema anatamani apatikane Waziri Mkuu ambaye anathamini nafasi ya wabunge katika kuisimamia Serikali, ambayo yeye ndiye kiongozi wake mkuu.
Kwa upande wake Mbunge wa Sengerema, Tabasamu Khamis amesema anatarajia waziri mkuu atakayechaguliwa awe na kasi inayolingana na ile ya Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake, Kassim Majaliwa.
“Ninamtazamia Waziri Mkuu atakayevivaa viatu vya Kassim Majaliwa kiongozi ambaye alikuwa akifanya kazi kwa bidii na kushuka hadi kwa wananchi sambamba na kuzunguka nchi nzima kusikiliza wananchi,” amesema Tabasamu.
Pia amesema Bunge la sasa lina wabunge wapya kwa zaidi ya asilimia 75, wengi wao wakiwa vijana wenye ari na kasi mpya ambao wamepitia changamoto na uzoefu wa kufanya kampeni.
“Hivyo, si Bunge la kuja na mawazo binafsi; mtu asipobadilika anaweza kushangaa ifikapo Uchaguzi Mkuu wa 2030 zaidi ya asilimia 90 ya wabunge wakipoteza nafasi zao na kuja wapya kabisa,” amesema.
Aidha, mbunge huyo amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma za kijamii, akisema: “Changamoto kubwa tuliyonayo ni huduma za kijamii. Wakati tunatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ni lazima tuhakikishe huduma za kijamii hazisahauliwi. Miradi mikubwa iwe asilimia 50, na miradi ya huduma za jamii nayo iwe asilimia 50, ili maendeleo yawe ya usawa kwa wananchi wote.
“Haiwezekani miradi mikubwa ichukue asilimia 70 ya bajeti, halafu miradi ya huduma za kijamii ibaki na asilimia 30 pekee,” alisema.
“Bajeti zetu lazima ziwe na uwiano unaowezesha wabunge wengi kuwa salama kisiasa na wananchi kunufaika moja kwa moja. Ni muhimu huduma za kijamii ziwe angalau asilimia 50, na shughuli nyingine za kuendesha serikali zichukue asilimia iliyosalia la sivyo, mbele ya safari naona giza.”
Mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Esther Matiko amesema inawezekana Waziri Mkuu akatoka katika eneo lolote nchini, mradi awe mbunge wa jimbo, akisisitiza kuwa awe na vigezo vyote vya kushika wadhifa huo.
“Waziri Mkuu ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni na mwakilishi wa Serikali ndani ya Bunge. Tunahitaji Waziri Mkuu mwenye maono, mzalendo, na atakayebeba ajenda zote za Serikali pamoja na yale yanayojadiliwa bungeni, kwa sababu yeye ndiye daraja kati ya Serikali na Bunge,” amesema Matiko.
Ameongeza kuwa Waziri Mkuu ni kiungo muhimu katika Serikali, hivyo ni lazima awe mtu anayefahamu changamoto za Watanzania na kuelewa mahitaji yao halisi.
Mbunge wa Tunduru Kasikazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu amesema anatamani waziri mkuu atakayechaguliwa awe mchapa kazi, kwa kuwa ndiye mtendaji mkuu wa Serikali.
“Natamani tuwe na waziri mkuu mbunifu, ambaye mara zote anatafuta majawabu ya changamoto za wananchi. Tunahitaji waziri mkuu mwenye mfumo wa uendeshaji wa Serikali unaoshirikisha wabunge wote, kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi mezani kwake kutoa mchango wa kutatua changamoto za wananchi,” amesema.
Amesema anatamani apatikane Waziri mkuu aliye na kariba ya hayati Edward Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa sita wa Tanzania.
“Sokoine alifariki mwaka niliyozaliwa, lakini nimekuwa nikifuatilia kwa karibu uwajibikaji wake. Tunamhitaji Sokoine wetu ambaye hatasubiri mambo yaletwe mezani kwake; atachukua hatua mapema, bila kusubiri kuagizwa,” amesema Ado.
Hata hivyo, amesema uamuzi wa nani awe waziri mkuu unabaki wa Rais.
Kuhusu uwezekano wa kuteuliwa waziri mkuu mwanamke, mbunge huyo amesema: “Mimi ni mmoja wa waumini wa fikra za mwanamapinduzi Thomas Sankara wa Burkina Faso, ambaye aliwahi kusema kuwa ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi si suala la hisani, bali ni sharti la lazima kwa mafanikio ya mapinduzi ya kijamii.
“Ninaamini kuwa ili taifa lifanikiwe, tunapaswa kuwa na wanawake wengi katika vyombo vya maamuzi. Hata hivyo, mimi naamini sifa na uwezo vinaanza mbele ya umri, jinsia au vigezo vinginevyo. Kwa hiyo, tuongozwe kwanza na sifa na uwezo wa mtu,” amesema.
Mbunge wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa, amesema kwa mujibu wa utaratibu wa nchi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uteuzi wa Waziri Mkuu ni jukumu la Rais pekee.
“Ni vizuri tukawa na subira. Matarajio ya Mheshimiwa Rais yako wazi; si ya kubahatisha. Kuna dira aliyoiweka kama mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambayo inabeba malengo makubwa ya taifa letu na mwelekeo wa tunapotaka kufika,” amesema Kadogosa.
Amesema Ilani ya CCM na bajeti iliyopitishwa na Bunge ndizo zinazoonyesha mwelekeo wa Serikali ijayo.
Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani amesema anatamani kupata waziri mkuu atakayefanya kazi kwa karibu na Bunge, kuunganisha Serikali na wananchi, na kuendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania, hususan wale wa kipato cha chini, wakulima na wafanyabiashara wadogo vijijini.
“Tunahitaji kiongozi imara anayejali mahusiano kati ya Serikali na wananchi wake, ambaye atashughulikia changamoto zinazowakabili wananchi katika majimbo, halmashauri, manispaa na vijiji vyetu,” amesema Cherehani.
Kuhusu hoja kwamba wingi wa wabunge wa CCM unaweza kufanya Bunge lipoteze makali, Cherehani amesema wingi huo si kigezo cha kukosa uthubutu.
Amesisitiza kuwa matatizo yanayowakabili wananchi katika majimbo ndiyo yanayotoa nguvu ya hoja ndani ya Bunge.
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, pia amesema kuwa anamtamani Waziri Mkuu mchapakazi:
“Tunaangalia na Rais aliyeko madarakani, Samia Suluhu Hassan ambaye ni mchapakazi. Neno ‘meno’ ya mbunge ni kuhakikisha Serikali inasimamiwa vizuri na wabunge wanayo meno hayo ya kuisimamia Serikali,” amesema mbunge huyo.
Naye Mbunge wa Ulanga, Salim Almasi amesema anatamani waziri mkuu atakayewaunganisha wabunge kuwa timu moja yenye lengo la amani na maendeleo ya taifa.
“Tunahitaji waziri mkuu mwenye misimamo thabiti, ambaye anaweza kusimamia msimamo wake kwa lengo la kurekebisha tabia za watendaji serikalini na kuhakikisha wanatekeleza jukumu lao kwa uzalendo na kwa manufaa ya Watanzania wote,” amesema Almasi.
Ameongeza kuwa: “Bunge lililopita, lenye wabunge wengi wa CCM, liliweza kufanya kazi kwa ufanisi. Nina uhakika Bunge hili jipya pia litaendelea kufanya kazi vizuri, likisimamia sera na mikakati ya Serikali kwa ufanisi.”
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (CCM), amesema anamtegemea Rais kuteua Waziri Mkuu atakayefanya kazi kubwa ya kuunganisha Watanzania, kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuisimamia dira ya taifa.
“Tunahitaji waziri mkuu ambaye atakuwa mtiifu kwa Rais lakini pia atazungumza lugha moja ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya Watanzania. Tunaunga mkono chaguo lolote, mwanaume au mwanamke na tutampa ushirikiano wa kutosha ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema Waitara.
Ameongeza kuwa wingi wa wabunge wa chama kimoja siyo kizuizi cha ufanisi wa Bunge.
“Hata kwenye mabunge ya chama kimoja, wabunge walikuwa wakali kuisimamia Serikali. Hivyo wingi wa wabunge wa CCM haupunguzi uwezo wa Bunge kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema.
Mbunge wa Mtwara Mjini, Dk Joeli Nanauka, amesema anatamani Waziri Mkuu atakayekuwa na uwezo wa kutafsiri ilani ya CCM na dira ya maendeleo ya taifa kwa vitendo, na kuleta matokeo yanayohitajika.
“Tunatarajia kiongozi ambaye ataweza kuunganisha watu katika maeneo mbalimbali. Suala la jinsia si changamoto; Waziri Mkuu anaweza kuwa wa jinsia yoyote. Lakini pale masilahi yanapokuwa hayatekelezwi, nitasimama kidete kuhakikisha yanafanyika,” amesema Dk Nanauka.