:::::::::::
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetangaza rasmi kuanza kutoa msaada wa kisheria bila malipo kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya jinai, yakiwemo uhaini, kula njama ya kutenda kosa la jinai, uharibifu wa mali, unyang’anyi wa kutumia silaha, uchomaji mali na maandamano bila kibali. Huduma hiyo imeanza kutolewa tangu tarehe 7 Novemba, 2025, katika mikoa kadhaa nchini.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Wakili Maduhu William alisema uamuzi huo umetokana na tathmini iliyoonyesha kuwa watuhumiwa wengi, hususan vijana wenye umri kati ya miaka 19 hadi 25, hawana uelewa wa kutosha wa masuala ya kisheria na hawamudu gharama za kuajiri mawakili.
Kwa mujibu wa TLS, mashauri hayo yamefunguliwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mara, Mwanza, Arusha, Njombe na Kigoma, huku idadi kubwa ya watuhumiwa ikiendelea kuongezeka.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila mtu ana haki ya kutendewa haki kwa usawa mbele ya sheria. Hivyo TLS tumeamua kujitolea kuwawakilisha watuhumiwa wote wanaokabiliwa na mashauri haya bila malipo na bila masharti yoyote,” alisema Wakili Maduhu.
Taarifa za TLS zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 400 walikamatwa Dar es Salaam, zaidi ya 200 mkoani Mwanza, takribani 312 Kilimanjaro, huku watuhumiwa 300 kati yao wakiwa tayari wameachiliwa.








