Nahodha Mtibwa Sugar atoa siku 14

NAHODHA wa Mtibwa Sugar, Erick Kyaruzi amesema licha ya kutoruhusu mabao mengi katika mechi tano walizocheza, lakini kuna uhaba wa mabao ya kufunga akieleza kuwa siku 14 walizonazo kabla ya kushuka uwanjani watajisahihisha.

Pia amewatoa hofu mashabiki kuwa licha ya matokeo waliyoanza nayo kutokuwa mazuri sana, lakini Mtibwa Sugar ina nafasi ya kufanya vizuri na kumaliza msimu ikiwa pazuri, na ishu ya kushuka daraja haipo.

Mtibwa Sugar imecheza mechi tano na kuvuna alama tano ikiwa imeshinda moja, sare mbili na kupoteza mbili, inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi. Itarejea tena uwanjani Novemba 25, 2025 kuikaribisha KMC inayoburua mkia na pointi tatu.

Katika mechi hizo tano, Mtibwa Sugar imefunga mabao mawili na kuruhusu matatu, huku ikiwa na matumaini ya kurejea vyema kwenye ubora pale ligi itakapoendelea kwa bingwa huyo mara mbili wa Ligi Kuu mwaka 1999 na 2000.

Kyaruzi ameliambia Mwanaspoti kuwa, matokeo waliyonayo si mazuri sana na kwakuwa wametambua walipojikwaa, wanaendelea na mazoezi kuhakikisha mechi zinazofuata wanafanya vizuri na kujiweka nafasi nzuri.

Amesema tatizo kubwa imekuwa upande wa kutotumia vyema nafasi wanazopata kufunga mabao, jambo ambalo wanaendelea kulifanyia kazi kwa siku hizi za maandalizi ya mechi ijayo dhidi ya KMC.

“Eneo la beki sijaona kama kuna makosa mengi kwani tumeruhusu mabao matatu, tutajitahimini ila zaidi tunaendelea kufanyia kazi ufungaji mabao ili kujitoa nafasi za chini,” amesema beki huyo.

Nyota huyo wa zamani wa Kagera Sugar, ameongeza kuwa pamoja na matokeo waliyoanza nayo, bado wana uwezo wa kubadili upepo kwakuwa kikosi kina ari na morali, huku wachezaji wakisaka rekodi na historia.

“Wachezaji wengi ni kinda ambao wanatafuta mafanikio, kwa maana hiyo ishu ya kushuka daraja haliwezi kujirudia, ligi ndio imeanza na tunao uwezo wa kubadilika na kukaa nafasi za juu,” amesema.

Kwa upande wake straika wa timu hiyo, Raizin Hafidh, amekiri uwepo wa ukame wa mabao kikosini akieleza licha ya kutopata nafasi ya kucheza, lakini anayo matumaini kurekebisha makosa.

“Sijapata nafasi kubwa ya kucheza kutokana na mipango ya benchi la ufundi na changamoto za kifamilia, nikipata nafasi hiyo naweza kubadili upepo,” amesema mfungaji bora huyo wa Ligi ya Championship msimu uliopita akifunga mabao 18 sawa na Abdulaziz Shahame aliyekuwa TMA na Andrew Simchimba aliyekuwa Geita Gold.