SERIKALI YAONYESHA DHAMIRA YA KUINUA SEKTA YA HORTICULTURE NCHINI

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema dhamira yake ni kuendeleza sekta ya horticulture kama injini muhimu ya mageuzi ya kilimo, ukuaji wa uchumi na ajira nchini, ikiahidi kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji, masoko na miundombinu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Yonanzi, amesema serikali imejipanga kuhakikisha sekta hiyo inakuwa miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa viwanda na biashara ya kimataifa.

Dkt.Yonazi ametoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji wa Kilimo cha Horticulture 2025 (HoBIS2025) lililofanyika jijini Dar es Salaam, likihusisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wanadiplomasia na wadau wa maendeleo.

Amesema kupitia kongamano hilo, serikali inataka kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuongeza tija katika uzalishaji, usindikaji na mauzo ya nje ya mazao ya horticulture.

Amesema serikali imeendelea kufanya mageuzi ya kisera na kimuundo ikiwemo marekebisho ya kodi, uwezeshaji wa wakulima kupitia mikopo nafuu ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji, maghala ya baridi, bandari na viwanja vya ndege. “Dhamira ya serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara ya mazao ya horticulture Afrika Mashariki na Kati,” amesema Dkt.Yonazi.

Akizungumzia mafanikio ya sekta hiyo, Yonazi amesema uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni 1.1 mwaka 2003/04 hadi zaidi ya tani milioni 8.4 mwaka 2023/24, huku mauzo ya nje yakipanda kutoka Dola za Marekani milioni 64 mwaka 2004 hadi takribani Dola milioni 569 mwaka 2024.

Pia amepongeza juhudi za wakulima, wajasiriamali na taasisi kama TAHA kwa mchango wao mkubwa katika ukuaji huo.

Aidha, amesema mafanikio haya yanaendana na dira za kitaifa ikiwemo Tanzania Agriculture Master Plan 2050, Agenda 10/30 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III), ambazo zote zimeweka horticulture kama kipaumbele cha kimkakati cha kukuza uchumi jumuishi na endelevu. “Kupitia dira hizi, tunajenga mfumo wa kilimo unaozalisha ajira, lishe bora na kipato kwa wananchi wetu,” amesisitiza.

Dkt.Yonanzi alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau wa sekta binafsi, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo kuwekeza zaidi katika utafiti, teknolojia na ubunifu ili kuongeza ubora na ushindani wa bidhaa za Tanzania kwenye masoko ya kimataifa. Amesema ushindani wa sasa unahitaji ubora, ufuatiliaji wa viwango na usimamizi wa minyororo ya thamani kutoka shambani hadi sokoni.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Yonazi amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi kupitia Tume ya Rais ya Mageuzi ya Kodi na Wizara ya Kilimo, kuhakikisha vikwazo vinavyokwamisha biashara ya horticulture vinaondolewa. Amesema HoBIS2025 si tu jukwaa la mijadala, bali ni hatua ya utekelezaji wa maamuzi yatakayowezesha sekta hiyo kufikia viwango vya kimataifa. “Tanzania ya leo inajenga msingi wa kesho yenye uchumi wa kijani, unaotegemea kilimo chenye tija na thamani kubwa,” amesema kabla ya kufungua rasmi kongamano hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amesema sekta ya horticulture imekua kwa kasi kubwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni 1.1 mwaka 2003/04 hadi tani milioni 8.4 mwaka 2024, na mapato ya mauzo nje kuongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 64 hadi milioni 569.

Amesema mafanikio hayo yametokana na sera madhubuti za serikali, uwekezaji wa kimkakati na ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Pia ameongeza kuwa horticulture sasa imepewa kipaumbele katika mipango ya kitaifa kama ASDP II, Agenda 10/30, na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Mweli amesisitiza kuwa Tanzania bado ina fursa kubwa ya kuongeza tija kupitia teknolojia rafiki kwa mazingira, kuongeza thamani ya mazao, na kuimarisha mifumo ya usafirishaji na uhifadhi baridi ili kufikia viwango vya kimataifa.

Mtendaji wa Chama cha Wakulima wa Horticulture Tanzania (TAHA), Dkt. Jacqueline Mkindi, aliwakaribisha washiriki wote akibainisha kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujenga ushirikiano, kubadilishana ujuzi na kuibua fursa za uwekezaji zitakazochochea ushindani wa sekta hiyo.