::::::::
Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema haitamwacha nyuma mtoto yeyote katika safari ya elimu, huku ikizindua rasmi Taarifa ya Tathmini ya Sera za Urejeaji na Mpango wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Kuwarejesha Shuleni Wanafunzi Waliokatiza Masomo katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MOEST), Dkt. Hussein Mohamed Omar, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kila mtoto nchini anapata fursa ya kuendelea na elimu bila kujali changamoto zilizowakatisha masomo.
Alisema uzinduzi huo siyo wa vitabu pekee, bali ni tukio lenye maana kubwa kwa taifa, kwa sababu linarejesha matumaini kwa watoto wa Kitanzania waliokatishwa ndoto zao za kielimu.
Dkt. Omar alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha mpango huo unatekelezwa ipasavyo, huku akihimiza jamii kuelewa na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
Alisema jukumu la Serikali ni kuhakikisha maandalizi, uratibu na usimamizi wa rasilimali unafanyika kwa ufanisi katika ngazi zote, ili kufikia matokeo chanya kwa watoto wote.
Dkt. Omar alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wadau wa elimu akiwemo Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), UNICEF na taasisi nyingine kwa mchango wao mkubwa katika kuandaa na kutekeleza mpango huo unaolenga kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote.
Aidha, aliwapongeza Mwenyekiti wa Bodi ya TEN/MET, Bw. Simon Nanyaro, na Mratibu wa Taifa, Bi. Martha Makala, kwa uongozi wao thabiti na ushirikiano wa karibu na Serikali katika kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi na yenye usawa kwa watoto wote nchini.
Katika uzinduzi huo, Dkt. Omar pia alizindua Taarifa ya Utafiti wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Urejeaji miongoni mwa wanafunzi wa kike waliokatisha masomo kutokana na ujauzito. Taarifa hiyo imeonesha mafanikio makubwa, ikiwemo zaidi ya wanafunzi wa kike 13,000 na wanafunzi wa kiume 17,000 kurejea shule na kuendelea na masomo yao.
Kabla ya kufungua rasmi mpango huo, Dkt. Omar alihitimisha kwa kutoa wito kwa wadau wote wa elimu nchini kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika safari ya elimu.
Alisema hatua hiyo ni mwanzo wa utekelezaji mpana wa sera na mwongozo wa urejeaji, na kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya msingi ya elimu.





