Dar es Salaam. Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), kimelaani vurugu, mauaji na uharibifu wa mali vilivyotokea siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Pia, kimetoa pole kwa wote waliopoteza ndugu au mali, huku kikiunga mkono agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufanya uchunguzi wa kina na kuwawajibisha wahusika wote kwa mujibu wa sheria.
Maandamano yaliyozalisha vurugu hizo ambazo zilianzia Dar es Salaam na baadaye katika baadhi ya mikoa kama Arusha, Mwanza, Mara, Mbeya na Songwe zilisababisha taharuki na madhara.
Si hilo tu, bali vurugu hizo zilizua hofu na usumbufu wa shughuli za kila siku, kukwama kwa usafiri na usafirishaji wa mizigo, kupanda kwa gharama na wananchi kulazimika kubadili mtindo wa maisha.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatano Novemba 12, 2025 na TPBA, imeeleza kwa mujibu wa Katiba 1977 inatambua haki za binadamu kama uhuru wa maoni na maandamano, lakini haki hizo zina mipaka ya kisheria kulinda amani na usalama wa Taifa.
“Maandamano ya Oktoba 29, 2025 hayakuwa halali, kwani yalikiuka zuio la polisi na kusababisha vurugu. TPBA inasisitiza kuwa matumizi ya nguvu na silaha yanapaswa kuwa ya kiwango cha lazima pekee na kwa uwajibikaji wa kisheria,” imeeleza taarifa hiyo.
Kuhusu changamoto za intaneti, taarifa hiyo imeeleza mamlaka zinaweza kudhibiti mawasiliano kwa muda kwa mujibu wa sheria kulinda usalama wa Taifa.
Mbali na hilo, TPBA kimesema haki huambatana na wajibu wa kuheshimu Katiba na mamlaka halali, huku kikisema vyama vya siasa vilivyohusishwa na vurugu vinaweza kufutiwa usajili kwa mujibu wa sheria.
“TPBA inatoa wito wa utulivu, umoja, na mazungumzo ya maridhiano kama alivyoeleza Dk Emmanuel Nchimbi (Makamu wa Rais) kwa niaba ya Rais (Samia) ili Taifa liendelee kuwa la mfano wa amani barani Afrika,” imeeleza taarifa hiyo.
Novemba 7,2025 akimwakilisha Rais Samia katika mkutano mkuu maalumu wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Nchimbi alisema dhamira ya Serikali kuanzisha maridhiano ili kuhakikisha kila sauti inasikilizwa na kurejesha amani.
“Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba tunaanzisha mazungumzo ya maridhiano ili hata hao wachache wapate nafasi ya kusikilizwa ili kuwa na Taifa lenye amani, umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na dunia,” alisema Dk Nchimbi.
Sambamba na hilo, mkutano huo wa SADC ulimpongeza, Rais Samia na viongozi wengine waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Mbali na hilo, mkutano huo wa SADC ulitoa pole kwa ndugu na familia waliopotolewa na wapendwa wao wakati wa maandamano na vurugu zilizotokea Madagascar na Tanzania.