Uchaguzi Zanzibar na tafasiri ya amani ya kweli

Sasa ni wiki ya pili tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Bunge na madiwani. Tofauti na chaguzi zilizopita, safari hii hakukuwa na mauaji, ulemavu, wajane, mayatima wala watu kupigwa viboko kama ilivyowahi kushuhudiwa awali.

Tangu kuanza kwa mchakato wa uandikishaji wapigakura hadi kufanyika kwa kura ya mapema Oktoba 28, 2025 na uchaguzi mkuu siku iliyofuata, kulikuwa na malalamiko na dosari kadhaa.

Chama cha ACT-Wazalendo kilidai watu wapatao 25,000 walinyimwa haki ya kuandikishwa, huku wengine mamia waliokuwa hawana sifa wakiruhusiwa kuandikishwa. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ililalamikiwa kwa kukaa kimya licha ya madai hayo kuambatanishwa na vielelezo.

Orodha ya wapigakura ilidaiwa kuwa na majina ya watu waliokwishafariki miaka mingi iliyopita, wengine wakiwa watu ninaowafahamu niliowahi kushuhudia mazishi yao. Wapo pia walioeleza kwamba walijiandikisha, lakini majina yao yalifutwa dakika za mwisho. Kuna ripoti kwamba mamia ya vijana waliovaa sare za vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walionekana wakipiga kura katika maeneo ambayo hayakuwa na kambi rasmi, mfano jimbo la Malindi.

Pemba, idadi ya waliopiga kura ya mapema ilifikia 14, mara sita ya waliotarajiwa, kwa mujibu wa madai ya upinzani.

Malalamiko mengine yalihusu ongezeko kubwa la wapigakura, karibu mara mbili ya uchaguzi wa 2020, jambo lililozua maswali. Kila mpigakura alipokea karatasi tatu kwa ajili ya urais, uwakilishi na udiwani lakini matokeo katika baadhi ya vituo hayakuendana. Kwa mfano, kama wapigakura walikuwa 250, idadi hiyo haikulingana katika matokeo yote matatu kama inavyotarajiwa.

Nilipokuwa nikitembelea baadhi ya vituo nilishuhudia makarani wakitumia mwanga wa simu zao kwa vile ndani kulikuwa na giza, hali iliyoibua shaka kuhusu uwazi uliokuwa umeahidiwa na ZEC. Hali kama hiyo ilikuwapo katika vyumba namba 3, 4 na 5 vya kituo cha Mwalimu Nyerere, jimbo la Bububu.

Matokeo ya ushindi wa kishindo wa CCM, hasa katika maeneo yaliyokuwa ngome za ACT – Wazalendo kama Pemba, yamezua mjadala. Wapo waliohoji uhalisia wa matokeo hayo, hasa kwa kuzingatia kwamba katika chaguzi zilizopita CCM ilikuwa ikipata chini ya asilimia 10 katika majimbo mengi.

Katika baadhi ya vituo, zilitumika kalamu za “marker pen” zenye wino unaofutika kirahisi, ambazo ACT –Wazalendo kilidai zilitumika kuwapaka alama wale waliopangwa kupiga kura zaidi ya mara moja.

Idadi rasmi ya wapigakura ilitajwa kuwa 720,000, jambo lililotiliwa shaka kutokana na madai ya maelfu kukataliwa kujiandikisha. Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2020, idadi ya wapigakura ilikuwa 448,482. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022, Zanzibar ilikuwa na watu milioni 1.88, hivyo makisio ya wapigakura kwa sasa yangeweza kufikia milioni 2.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyopita, alitangaza chama chake hakitambui matokeo hayo kwa madai ya wizi wa kura uliofanywa.

Kwa muhtasari, uchaguzi huu umeirudisha Zanzibar katika mgawanyiko usio na tija. Licha ya kauli za viongozi na vyombo vya habari vya serikali kwamba amani imerejea, ukweli ni kuwa hali ya kutoaminiana na uhasama bado ipo. ACT – Wazalendo inasisitiza imeporwa ushindi, huku CCM ikijivunia ushindi mkubwa, ikiutaja kuwa matokeo ya kazi nzuri ya Rais Hussein Mwinyi katika awamu yake ya kwanza.

Historia inaonyesha kuwa pale jamii inapogawanyika na kushikilia misimamo ya chuki, maendeleo huwa magumu kupatikana. Mitandao ya kijamii sasa imesambaza video zinazodai kuonyesha watoto waliovaa sare za vikosi wakipiga kura, jambo lililopigwa marufuku na ZEC.

Zanzibar imewahi kupata maridhiano ya kisiasa mara tatu kupitia uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini kila uchaguzi mpya unapokuja, maridhiano hayo hutikisika na hatimaye huvunjika bila talaka rasmi.

Katika hotuba ya uzinduzi wa Baraza Jipya la Wawakilishi, Rais Mwinyi aliahidi kuimarisha umoja wa Wazanzibari na kuongoza bila upendeleo kwa manufaa ya wote.

Ni kauli yenye matumaini, lakini kwa kuzingatia historia ya kuvunjika kwa maridhiano mara tatu na mazingira ya sasa ya kisiasa, safari ya kurejesha umoja wa kweli inaonekana kuwa ngumu.

Suluhisho linahitaji uaminifu wa kweli, dhamira njema na utayari wa pande zote kuweka maslahi ya Zanzibar mbele ya maslahi ya vyama. Ni lazima kuepuka kauli za uchochezi na mizengwe ya kisiasa. Katiba isichezewe na sheria zisitungwe kwa matakwa ya upande mmoja.

Tuombe Mungu, mvutano huu uwe mwisho wa mitihani ya kisiasa Zanzibar, na uwe mwanzo wa ukurasa mpya wa maelewano, upendo na amani kama ilivyokuwa kwa wazee wetu waliotutangulia. Yaa Rabbi, Mungu ibariki Zanzibar na watu wake.