UCHAMBUZI WA MALOTO: Huyu ndiye Waziri Mkuu atakayeendana na Rais Samia?

Upo mjadala sasa kuhusu majina ya mtu anayeweza kuwa waziri mkuu. Naam, ni mwanzo wa muhula mpya wa serikali. Kila kitu kinaanza upya. Hiki ndiyo kipindi cha mishangao, nyakati za kuibuka kwa haiba mpya kisiasa na kiuongozi.

Ni nyakati kama hizi, miaka 30 iliyopita, Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, aliduwaza wengi alipowasilisha jina la Fredrick Sumaye bungeni, ili aidhinishwe na wabunge kuwa Waziri Mkuu. Sumaye hakuwa mwanasiasa maarufu, Mkapa alimwibua.

Sumaye alikuwamo ndani ya Baraza la Mawaziri la Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi. Sumaye alishakuwa Naibu Waziri wa Kilimo, kisha Waziri wa Kilimo, lakini hakuwa na umaarufu. Alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, ndipo alianza kufuatiliwa na watu kumfahamu zaidi.

Nyakati kama hizi, miaka 20 iliyopita, Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, hakushangaza watu alipowasilisha jina la Edward Lowassa, kuwa Waziri Mkuu. Alikuwa amegusa matarajio ya wengi. Kwa urafiki wao, ushirikiano waliokuwa nao, ilikuwa rahisi kubashiri.

Miaka 10 iliyopita, kipindi kama hiki, Rais wa Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli, alituma bungeni jina la Kassim Majaliwa, ili wabunge wamwidhinishe kuwa Waziri Mkuu. Ulikuwa mshangao. Majaliwa alikuwa ametoka kuwa Naibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisheni, akishughulika na Elimu.

Unaweza vipi kuwaza kwamba Rais anaweza kumpandisha mtu ghafla kutoka Naibu Waziri hadi kuwa Waziri Mkuu? Zingatia, Majaliwa ndiye Mtanzania wa kwanza kuwa Waziri Mkuu, pasipo kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri kabla.

Majaliwa alikuwa Naibu Waziri. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 55 (2), inaelekeza wazi kuwa naibu mawaziri siyo wajumbe wa Baraza la Mawaziri. Kwa mantiki hiyo, Majaliwa ndiye mwenye rekodi ya kuingia Baraza la Mawaziri moja kwa moja akiwa Waziri Mkuu.

Muhtasari huu unalenga kujenga taswira kuwa hiki ni kipindi ambacho marais huwashangaza watu. Rais anakuwa na fursa ya kuteua yeyote miongoni mwa wabunge waliochaguliwa kutoka kwenye majimbo ya uchaguzi. Hivyo, anaweza kumpendekeza ambaye watu hawakumtarajia. Imeshatokea nyuma.

Ni mwanzo wa kila kitu kipya. Utamaduni wa Tanzania, kama ilivyoainishwa kwenye Katiba, kila baada ya miaka mitano, lazima kuwe na kituo. Wananchi wawapime viongozi wao, wawachekeche na kuchagua wapya. Huwaongezea muhula wawatakao na kuwakataa wale wasiorudhishwa nao. Ni siasa na mizungu yake.

Katiba ya Tanzania, ibara ya 51, ibara ndogo ya 1 na 2, inaeleza kuwa ndani ya siku 14 baada ya Rais kula kiapo, atapaswa kuteua Waziri Mkuu miongoni mwa wabunge wa kuchaguliwa anayetokana na chama chenye wabunge wengi au anayeungwa mkono na wabunge wengi.

Hata hivyo, lipo sharti la kikatiba kwamba Waziri Mkuu hatatambulika kuwa Waziri Mkuu mpaka kwanza athibitishwe kwa kura nyingi na wabunge, vilevile ale kiapo mbele ya Rais.

Katiba ibara ya 52, ibara ndogo ya 1 na 2, inafafanua majukumu ya Waziri Mkuu kwamba ndiye mtendaji na msimamizi wa shughuli za kila siku serikalini, vilevile ndiye kiongozi wa shughuli zote za Serikali bungeni.

Katiba ibara ya 55 (1), inaeleza wazi kuwa Rais atateua mawaziri miongoni mwa wabunge baada ya kufanya mashauriano na Waziri Mkuu. Na imeshaelezwa kuwa Waziri Mkuu hatashika nafasi hiyo mpaka kwanza ale kiapo.

Kwa kutafsiri Katiba ibara ya 57, ibara ndogo ya 2 (e), uwepo wa Serikali unategemea uwepo wa Waziri Mkuu. Hakuna mawaziri wala naibu mawaziri endapo kiti cha Waziri Mkuu kitakuwa wazi.

Ongezea ukweli kwamba, kikatiba, Waziri Mkuu wa Tanzania ndiye mshauri mkuu wa Rais kiutendaji na msimamizi mkuu wa utekelezaji sera na mipango ya kila wizara na kila taasisi ya umma.

Waziri Mkuu ndiye msimamizi wa rasilimali za umma, ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za serikali. Ndiye mkuu wa shughuli za serikali bungeni. Hakuna serikali bila Waziri Mkuu. Shughuli za Bunge haziwezi kufanyika bila uwepo wa Waziri Mkuu.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 33 (2) inataja Madaraka ya Rais kuwa ni Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

Umeshaona kuwa Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa serikali, na kwamba mkazo kabisa, inabainishwa kwamba Waziri Mkuu ndiye mtekelezaji mkuu wa maagizo ya Rais.

Mwongozo huo wa kikatiba, unampambanua Waziri Mkuu kama kiongozi ambaye anapaswa kuwa na hekaheka nyingi za kimajukumu na mwenye kuonekana kuliko mwingine yeyote serikalini.

Rais nafasi yake ni ule ukuu wa Serikali, Ukuu wa Nchi na Ukuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama (Amiri Jeshi Mkuu). Ukiwa tu mkuu, unatakiwa usikike au uonekane kwenye vitu vya lazima, kwa hiyo si kila mara utaonekana, wakati Waziri Mkuu kama mtendaji mkuu wa Serikali, anatakiwa aonekane mara kwa mara.

Vipo vikao vya Baraza la Mawaziri ambavyo Rais ndiye mwenyekiti wake. Ni hapo ndipo ripoti za kiutendaji hutolewa na kujadiliwa, vilevile mipango, dira, maazimio ya Serikali hujadiliwa na kupitishwa kabla ya kwenda kwenye utekelezaji. Huko kwenye utelezaji, waziri mkuu ndiye mwenye uwanja wake.

Wajumbe wa Baraza la Mawaziri ambao mbali na Rais, ni Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, mawaziri kamili wa wizara na Mwanasheria Mkuu, hutumia vikao vyake kumshauri Rais kuhusu mambo mbalimbali ya Serikali. Rais akitoa baraka za jambo kufanyika, Waziri Mkuu anaingia kazini kwenye utekelezaji.

Jinsi Katiba inavyobainisha, Rais ni kama kocha kwenye timu na Waziri Mkuu ni nahodha. Kocha hupanga safu ya wachezaji ndani ya uwanja na kuelekeza mtindo wa kucheza lakini haingii uwanjani. Nahodha anakuwapo ndani ya uwanja akicheza pamoja na wachezaji wenzake, akihakikisha kila mchezaji anawajibika kwenye eneo lake kulingana na maagizo ya kocha.

Kama nahodha alivyo bosi kwa wachezaji wenzake ndani ya uwanja, ndivyo Waziri Mkuu alivyo kiongozi kwa mawaziri wengine. Kama kocha ambavyo hubaki nje ya uwanja akitazama wachezaji wake wanavyotekeleza mafundisho yake, ndivyo Rais anavyopaswa kuwa. Katiba inaagiza hivyo.

Kama ambavyo kocha hufanya mabadiliko ya wachezaji kwa kumtoa hata nahodha inapobidi ili kutafuta ushindi, ndivyo na Rais akiona mawaziri wake hawaendi anavyotaka anaweza kuwaondoa na kuteua wengine na hata kumpumzisha Waziri Mkuu anapojisikia.

Kwa kutazama nafasi ya Rais na wajibu wa Waziri Mkuu. Kwa kutambua aina ya utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan, sasa ni ruhusa kujadili majina. Je, nani anaifaa Tanzania ya sasa, ambaye ataendana na mtindo wa Rais Samia.

Muhula uliopita umempambanua Rais Samia kuwa aina yake ya uongozi ni ndani ya mipaka yake ya kikatiba. Haingilii mawaziri na anaacha nafasi kwa Waziri Mkuu kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Rais Samia anahitaji Waziri Mkuu ambaye atauvaa uwaziri mkuu ipasavyo, atakayejitoa kwa asilimia 100 kumsaidia Rais na kuwatumikia Watanzania. Hapaswi kuwa Waziri Mkuu mtaka sifa, anayeuwazia urais.

Waziri mkuu mwajibikaji, aliye tayari kubeba lawama zote za Serikali, huto atamfaa Rais Samia. Siyo mwigizaji, mkwepa lawama, ili ajilinde kuelekea kuupata urais. Je, nani huyo? Basi ndiye atamfaa Rais Samia na Watanzania katika uendeshaji wa Serikali.