UCHAMBUZI WA TUZO: Ubaguzi wa kiitikadi na athari zake kwa umoja wa kitaifa

Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache barani Afrika yaliyofanikiwa kudhibiti migawanyiko ya kidini na kikabila.

Tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, misingi ya taifa hili imejengwa juu ya umoja, utu, usawa na ujamaa. Hata hivyo, katika enzi hizi za mfumo wa vyama vingi, changamoto mpya imeibuka ya itikadi za vyama vya siasa zimeanza kuwa chanzo cha mgawanyiko wa kijamii na kifikra, huku kukikosekana jitihada madhubuti za kudhibiti hali hiyo.

Itikadi ni mfumo wa mawazo, imani au falsafa inayomwelekeza mtu au kundi la watu kuamini katika mwelekeo fulani kuhusu uongozi, maendeleo na haki za kijamii.

Tatizo hujitokeza pale wananchi au viongozi wanapoitafsiri itikadi kwa misingi ya uhasama, badala ya kuichukulia kama chombo cha hoja na majadiliano ya kujenga.

Hapo ndipo jamii huanza kugawanyika si kwa hoja zenye uzito, bali kwa kuangalia mtu anatoka chama gani au anaamini katika itikadi ipi.

Katika mazingira ya sasa nchini, mijadala mingi ya kitaifa kuhusu masuala ya uchumi, elimu au demokrasia hupoteza uzito wake kutokana na misimamo ya kiitikadi.

Wapo wanaoamini ustawi wa taifa unatokana na utulivu na maendeleo chini ya chama tawala, huku wengine wakiuona ustawi huo kupitia mabadiliko ya mfumo. Mara nyingi, vijana hujihusisha zaidi na vyama vya mageuzi, ilhali wazee hubaki na vyama vya ukombozi.

Imefikia hatua mtu akitoa hoja yenye tija, badala ya kujadili kiini chake, wengi huanza kuuliza huyu anatoka chama gani?

Matokeo yake, hoja muhimu kwa maendeleo ya taifa hupotezwa na mijadala hubadilika kuwa mashambulizi ya kisiasa.

Mfano, anapojitokeza mwanasiasa wa upinzani kutoa ushauri kuhusu sera ya kilimo au uchumi, baadhi ya wafuasi wa chama tawala huona ni mashambulizi, si mchango wa kitaifa. Vivyo hivyo, wafuasi wa upinzani mara nyingi hukataa kuona mazuri yanayotekelezwa na Serikali.

Hali hii inasababisha kudhoofika kwa mshikamano wa kitaifa. Itikadi inapogeuzwa silaha ya kugawa watu, huvunja misingi ya umoja uliyojengwa kwa miaka mingi.

Kadhalika, inapunguza ubora wa mijadala ya kitaifa kwa kuwa watu hukosa kuvumiliana kimawazo na hoja zenye tija hupuuzwa. Matokeo yake, uamuzi muhimu hucheleweshwa au kuachwa kwa sababu ya siasa badala ya hoja.

Zaidi ya hayo, ubaguzi wa kiitikadi huzorotesha uwajibikaji. Wananchi wanaposhabikia vyama bila kuchambua hoja, viongozi hukosa kuwajibika ipasavyo kwa kuwa wanajua watateteana wao kwa wao.

Sababu za mwelekeo huu
Kwanza, uelewa mdogo wa kisiasa. Wananchi wengi hawajatofautisha kati ya siasa kama nyenzo ya maendeleo na siasa kama ushindani wa vyama.

Pili, mienendo ya baadhi ya wanasiasa imekuwa ikichochea hisia za kiitikadi ili kulinda maslahi binafsi badala ya kuelimisha umma.

Tatu, mitandao ya kijamii imekuwa uwanja wa mashindano ya maneno, kejeli na chuki, badala ya hoja za kimaendeleo.

Vilevile, historia ya mfumo wa chama kimoja imeacha athari za muda mrefu. Baadhi ya watu bado hawajakubali kivitendo falsafa ya vyama vingi kama jukwaa la hoja tofauti.

Mfumo huo wa zamani bado unaonekana katika fikra na tabia za watu wengi, ambao hawajazoea hoja kinzani kama jambo la kawaida na lenye faida kwa taifa.

Kwa hiyo, ingawa tumeingia kwenye mfumo wa vyama vingi, mabadiliko ya kifikra na kiutamaduni bado hayajakamilika.

Kutokana na hilo, wapo wanaohoji kwamba tunatokaje hapa?
Kwanza, kunahitajika elimu ya uraia na uzalendo. Wananchi waelimishwe kwamba tofauti za kiitikadi ni za kawaida, lakini hazipaswi kugawa taifa.

Elimu hiyo itawasaidia kuelewa haki, wajibu na umuhimu wa umoja, pamoja na madhara ya siasa za kibaguzi.

Kwa sababu bila elimu hii, wananchi wataendelea kutanguliza mbele vyama badala ya maslahi mapana ya taifa.

Pili, ni lazima kuimarisha maadili ya kisiasa. Vyama vya siasa viweke mbele uvumilivu, heshima kwa mawazo tofauti na kuhimiza hoja za kujenga. Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii navyo vinapaswa kutoa kipaumbele kwa mijadala yenye tija, badala ya malumbano.

Tatu, taasisi muhimu za taifa kama Bunge, Mahakama na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), lazima ziwe huru na zionekane kuwa na uwazi.

Uadilifu wa taasisi hizi utapunguza migongano ya kiitikadi inayotokana na kutoaminiana.

Nne, uongozi wa mfano ni muhimu. Viongozi wa kisiasa wanapaswa kuonyesha kwa vitendo kwamba taifa liko juu ya chama. Kujenga utamaduni wa kusikilizana na kukubaliana au kutokubaliana, ni msingi wa demokrasia; si kila tofauti ni uhasama.

Tano, tuimarishe utamaduni wa mazungumzo badala ya misimamo mikali. Mazungumzo huruhusu kila upande kueleza hoja zake, na hivyo hupunguza chuki na kuongeza uelewano.

Mwisho, ni muhimu kukuza utambulisho wa pamoja wa Utaifa wa Kitanzania. Raia anapojitambua kama Mtanzania kabla ya kuwa mwanachama wa chama chochote, nguvu za itikadi za kugawa hupotea.

Viongozi nao wanapaswa kuwa na uadilifu, uwajibikaji na moyo wa utumishi wa umma. Hii itasaidia kupunguza chuki na ubaguzi wa kiitikadi, na kuimarisha umoja wa kitaifa uliojengwa kwa jasho na hekima ya waasisi wa taifa letu.