Vijana ACT Wazalendo wataja njia kufanikisha maridhiano

Dar es Salaam. Ngome ya vijana wa ACT – Wazalendo imetoa kauli kufuatia vurugu zilizotokana na maandamano ya Oktoba 29, 2025 ikisisitiza maridhiano kuponya Taifa.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa ngome hiyo, Abdul Nondo alipozungumza na waandishi wa leo Jumatano, Novemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam.

Akisoma maazimio ya ngome hiyo, Nondo amesema maridhiano ya kweli nchini hayawezi kufanikiwa bila kujenga msingi wa haki, ukweli na uwajibikaji, akitoa wito wa kuanzishwa kwa mchakato shirikishi utakaowezesha umoja wa kitaifa baada ya matukio ya maandamano ya Oktoba 29, 2025.

Amesema vijana wa ACT – Wazalendo wanaona ni muhimu kwa Taifa kuendelea kutafakari kuhusu matukio hayo kwa nia njema ya kujenga maridhiano endelevu, badala ya kukejeli na kupuuza kilichotokea.

“Hatua ya kwanza katika kujenga amani ya kudumu ni kutambua maumivu yaliyowapata  waliofiwa na wapendwa wao, waliojeruhiwa na walioharibiwa mali zao na kuona namna ya kuwafariji ili kutafuta suluhu na  kuhakikisha matukio kama hayo hayatokei tena,” amesema.

Akitoa pole kwa familia ambazo zimepoteza ndugu, kujeruhiwa kupoteza mali katika kipindi hicho, Nondo amehimiza umuhimu wa Serikali kukiri kuwa matukio yaliyofanyika ni makubwa, na kuchukua juhudi za kuponya majeraha ya kijamii na kuimarisha mshikamano wa Taifa.

“Chama chetu kinaamini kuwa maridhiano ya kweli yanaanza kwa kuzungumza ukweli na kukubaliana namna bora ya kujenga mustakabali wa pamoja bila chuki, visasi wala viburi kwa makundi mbalimbali, ” amesisitiza Nondo.

Ngome hiyo, imewapongeza mawakili wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kwa kujitolea kutoa msaada wa kisheria kwa vijana waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka sehemu mbalimbali nchini, kufuatia ghasia hizo.

Pongezi kwa mawakili hao zinatokana na tamko lao walilolitoa jana Jumanne Novemba 11, 2025 kuwa TLS itatoa utetezi wa kisheria kwa washtakiwa wote wa kesi za matukio hayo.

Akipongeza hatua hiyo, Nondo amesema inaonesha dhamira njema ya kulinda haki za raia kwa mujibu wa sheria.

Nondo amesema maridhiano ya kweli yatakayoponya Taifa yanapaswa kushirikisha wadau kutoka asasi mbalimbali za kiraia, wananchi, viongozi wa dini na vyama vya siasa.

Akigusia kauli ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohammed Kawaida, aliyoitoa hivi kuhusu maandamano hayo, Nondo amesema ni muhimu kwa viongozi wote wa vijana nchini kuzungumza lugha moja na kuhimiza amani badala ya lawama.

Nondo amesema katika mchakato wa majadiliano ya kitaifa, viongozi wa serikali na wa CCM wanapaswa kukiri na kukubali kuwa kilichotokea ni maafa mabaya na washiriki maridhiano kama wadau, si viongozi wa maridhiano.

“Maridhiano ya kweli ni lazima yajumuishe makundi yote ya kijamii wakiwemo wananchi, viongozi wa serikali na Chama cha Mapinduzi wawe sehemu ya wadau na kuwe na third part (mtu wa tatu) ambaye atakuwa msuluhishi,” amesema Nondo.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti UVCCM – Taifa, Kawaida alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ghasia hizo, alieleza kusikitishwa na yaliyotokea akisema vyama vya siasa vinapaswa kulaani matukio hayo na kuonya wale wanaotoa kauli za kuyachochea.

Pia, alitoa wito kwa vijana nchi kuacha kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kueneza habari za chuki na uvunjifu wa amani badala yake, watumie mitandao kwa fursa za maendeleo.

Hata hivyo, Nondo amesema Taifa linapaswa kujiuliza chanzo cha tofauti za kisiasa na kijamii zilizolifikisha hapa kusudi ipatikane njia bora ya kuzitatua kwa njia ya amani.

“Serikali inapaswa kuwasikiliza wananchi hasa vijana na kuhakikisha masuala yanayohusu haki, usawa na maendeleo yanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ili kuepusha matumizi ya nguvu kutafuta suluhu baada ya ghasia za kudai haki,” amesema.

Kwa mujibu wa Nondo, ACT – Wazalendo inasisitiza kuwa misingi ya maridhiano lazima ijikite katika kutambua makosa yaliyopita na kuanzisha majadiliano ya wazi kwa kuaminiana, yatakayosaidia Taifa kusonga mbele bila kurudia makosa ya zamani.

Nondo ameeleza kuwa chama chake kinapendekeza Serikali kuanzisha uchunguzi huru wa matukio yote yaliyotokea katika maandamano ya Oktoba 29 ili kubaini ukweli na kutoa suluhu kwa mustakabali wa nchi.

Aidha, Vijana ACT – Wazalendo wameshauri majeruhi wa matukio hayo   wasaidiwe kupata haki ya matibabu na familia zilizopoteza wapendwa wao zipewe faraja na usaidizi unaostahili kama ishara ya nia njema ya Taifa kuelekea maridhiano ya kweli.

Nondo amesisitiza kuwa ngome ya vijana wa ACT – Wazalendo itaendelea kushirikiana  na wadau wengine kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa Taifa lenye amani, haki na umoja wakitoa wito kwa vijana kuungana bila kujali tofauti zao.