Migogoro ya kisiasa ni miongoni mwa mambo yanayoathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya kiuchumi katika mataifa mengi duniani.
Migogoro hiyo, pia husababisha kukosekana kwa amani na kutishia usalama wa watu, hivyo kusababisha kusimama kwa shughuli za kila siku zinazofanywa na wananchi kujipatia kipato.
Baadhi ya wadau wanatahadharisha kuwa migogoro hiyo isipotatuliwa ipasavyo huweza kuleta athari mbaya zaidi zikiwamo kusimama kwa shughuli za uzalishaji mali, kutishia wawekezaji, kuchafua taswira ya nchi kimataifa, mambo yanayodhoofisha biashara na uchumi wa nchi kiujumla.
Mataifa kadhaa yaliyowahi kupitia mizozo ya kisiasa yakiwemo Zimbabwe, Kenya na Libya miongoni mwa mengi, yameshuhudiwa yakipitia mtikisiko kiuchumi kutokana na mizozo hiyo ambayo ilisababisha baadhi kuingiliwa na mataifa makubwa, kusitishiwa misaada ya kimataifa na huduma zingine muhimu za kibinadamu.
Kufuatia uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa Oktoba 29, 2025, kwa mara ya kwanza Tanzania imeingia katika historia ya kushuhudia mpasuko wa kisiasa uliotokana na maandamano ya vijana yaliyozua taharuki katika miji kadhaa na kuathiri shughuli za kijamii katika maeneo hayo.
Mara baada ya kuapishwa, Jumatatu Novemba, 3, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alilaani ghasia hizo kuwa si matendo ya kiungwana huku akisisitiza umuhimu wa maridhiano ya mazungumzo badala ya matumizi ya nguvu katika kumaliza tofauti za kisiasa.
“Taifa halijengwi kwa kugawanyika, taifa linajengwa kwa suluhu ya maridhiano na mazungumzo katika kumaliza tofauti zilizopo,” alisisitiza Rais huyo alipoapa kuendelea na muhula wake wa pili katika Serikali ya awamu ya sita.
Wakirejea kumbukumbu za mataifa yaliyowahi kupitia hali kama hiyo, baadhi ya wadau wanatahadharisha kuwa kilichotokea ni darasa kwa makundi yote nchini ili kuliepusha Taifa na athari mbaya kiuchumi.
Kwa kipindi cha takribani siku sita tangu siku hiyo, shughuli za kibiashara ambazo awali zilionekana imara zilipungua, miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya ilisimamisha shughuli zote za kiraia kupisha vyombo vya dola kuimarisha doria za kiusalama.
Masoko yalifungwa huku shughuli za usafiri na uchukuzi wa ndani kwa nchi kavu na majini nazo zikisimama kwa kipindi chote hicho, hali iliyoathiri mzunguko wa fedha na maumivu kwa familia zinazotegemea kutoka ili kupata mahitaji muhimu ya siku.
“Athari zilizotokea kufuatia ghasia hizo ni darasa kwa Taifa, kila upande umepata somo kutokana na nafasi yake maana hakuna kundi ambalo halijaguswa kuanzia Serikali, vyama vya siasa, wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema Sheikh Mussa Kundecha kupitia kipindi maalumu cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Jumapili, Novemba 9, 2025, akisisitiza hatua za haraka kuponya Taifa.
Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ndiyo lango kuu la kupitisha bidhaa nchini na kwa mataifa jirani yanayoizunguka Tanzania, nayo ilisimamisha huduma, bidhaa na mizigo mingi yakiwamo magari ya yanayopelekwa nchi jirani yaani In Transit (IT) yalikwama kupisha hali ya kiusalama kurejea.
Kufuatia hali hiyo, wafanyakazi waliokuwa wakitegemea malipo ya kila siku walikosa kipato huku serikali nayo ikipoteza mapato kutokana na walipakodi za kibiashara za kila siku kusitisha shughuli zao kwa kipindi chote hicho kilichodumu kwa takribani wiki moja.
Kampuni za usafirishaji wa ndani nazo zilisimamisha safari kwa hofu ya vurugu na uharibifu wa mali. Mabasi ya masafa marefu kutoka na kuingia kwenye miji na majiji yalisitisha safari zake huku treni za mizigo na abiria ikiwamo ile ya SGR nazo zilisitisha huduma kwa muda.
Baadhi ya viongozi wa mataifa jirani waliutaja mzozo huo kuathiri biashara na uchumi wa nchi zao kutokana na kusimama kwa shughuli za uchukuzi na utulivu wa jamii katika Taifa jirani yao.
“Kukosekana kwa amani Tanzania kunatuathiri sote katika ukanda wetu huu kwa namna moja ama nyingine,” alisema Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, akitaja huduma za reli ya Tazara inayounganisha mataifa haya mawili, alipozungumza wakati wa hafla ya uapisho wa Rais Samia, Novemba 3, 2025.
Katika mitaa ya jiji kuu la biashara, Dar es Salaam, daladala ambazo ni uti wa mgongo wa usafiri wa wananchi wa kipato cha chini zilisimama, madereva na wamiliki wa vyombo hivyo wakihofia ghasia ambazo zingeweza kuharibu magari yao.
Mama lishe walifunga migahawa yao, waendesha bodaboda walitulia ndani huku ofisi za watumishi nazo zikifungwa, kila kitu kilisimama, ndivyo inaweza kuelezwa. Sekta ya fedha nayo iliguswa kufuatia kufungwa na kwa benki katika miji iliyoathirika, ambayo ndiyo yenye mzunguko mkubwa wa watu ikiwemo Dar es Salaam na kuathiri mzunguko wa fedha.
Mbali na athari hizo, baadhi ya biashara ziliripotiwa kuharibiwa vibaya ikiwamo kuchomwa moto kwa vituo vya mafuta, maduka na baadhi ya maeneo ya uwekezaji wa watu kutokana na ghasia hizo hali iliyorudisha nyuma uchumi wa wamiliki wa miradi hiyo.
Aidha, mbali na uharibifu wa bidhaa, vifo vya watu na majeruhi wakiwamo vijana viliripotiwa katika maeneo kadhaa kufuatia mzozo huo ingawa idadi kamili bado haijathibitishwa.
Hii imeathiri uchumi kwani waliopoteza maisha ama kupata ulemavu ni nguvu kazi muhimu katika uzalishaji mali na ujenzi wa uchumi wao binafsi na wa taifa kwa ujumla.
Athari kama hizi si mpya katika bara la Afrika na duniani kote. Mataifa kadhaa yamewahi kupitia mizozo ya kisiasa pengine zaidi ya hali iliyotokea Tanzania.
Taifa jirani la Kenya liliwahi kupitia mgogoro mkubwa wa kisiasa mwaka 2007 baada ya uchaguzi uliogubikwa na vurugu.
Kufuatia vurugu hizo, uchumi wake uliripotiwa kupoteza kudorora. Sekta ya utalii iliporomoka huku biashara zikiyumba hali iliyoathiri maisha ya wananchi.
Zimbabwe pia ilikumbwa na kuporomoka kwa uchumi baada ya mivutano ya kisiasa, ambapo sarafu ya nchi hiyo ilipoteza thamani yake kwa kiwango kikubwa.
Kwa Tanzania, mgogoro wa kisiasa wa Oktoba, 29, 2025 umekuwa kengele ya tahadhari ambao wachambuzi wa siasa na uchumi wanasema umeonesha jinsi siasa zisipoendeshwa kwa kusikilizana na kukubaliana zinavyoweza kuangusha uchumi mzima unaotegemea amani na imani ya wananchi.
Wadau wote, wakiwemo viongozi wa dini wanasema biashara, usafiri, viwanda, huduma zote muhimu na kila kitu huathiriwa moja kwa moja migogoro ya kisiasa inapotokea na kurejesha hali ya kawaida huhitaji juhudi kubwa kujenga upya utulivu, huku wakionya kuwa bila hatua hizo, athari za kisiasa zikiendelea huumiza uchumi na maisha ya watu wa kawaida kwa muda mrefu.
“Tumrudie Mungu wetu, tutazame tumejikwaa wapi kama Taifa na turejee kwa kujenga upya kwa kuziba nyufa zilizopasua umoja wetu na kutufikisha hapo hali hii haipaswi kujirudia,” anasisitiza Mtumishi wa Mungu na mhamasishaji wa amani, Ombeni Luka.