Wadau waomba kuanzishwa jukwaa la kilimo misitu Afrika Mashariki

Dar/ Mara. Wadau wa mazingira na kilimo mseto wamependekeza kuanzishwa kwa Jukwaa la Uratibu wa Kilimo-Misitu Afrika Mashariki kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisera, kitaasisi na utekelezaji wa miradi ya kilimo-misitu katika eneo hilo.

Mapendekezo hayo yametolewa leo Jumatano, Novemba 12, 2025 wakati wa kikao cha majadiliano kuhusu kilimo mseto katika maeneo kame ya Afrika Mashariki kilichoandaliwa na Swedish International Agriculture Network Initiative (SIANI) kwa ushirikiano na Vi Agroforestry mkoani Mara.

Mtaalamu wa kilimo, Mary Irunga kutoka Kenya amesema ipo haja ya kuwa na uratibu wa pamoja ili kuhakikisha manufaa ya kilimo misitu yanapatikana kwa nchi zote wanachama.

“Hakika kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta mbalimbali katika nchi za Afrika Mashariki ili kufanikisha manufaa ya kilimo-misitu.

“Uganda, Kenya na Tanzania zina mazingira yanayofanana kiikolojia, kijamii na kiuchumi, ambapo takribani asilimia 60 hadi 70 ni maeneo kame na yenye ukame wa wastani,” amesema Irunga.

Amesema changamoto kama mmomonyoko wa ardhi, ukataji miti hovyo na athari za mabadiliko ya tabianchi ni za pamoja, hivyo zinahitaji mkakati wa pamoja wa kikanda ili kuzitatua kwa ufanisi.

“Jumuiya ya Afrika Mashariki tayari ina mfumo wa kisiasa na taasisi za kushirikiana katika masuala ya mazingira na kilimo, hivyo ni wakati mwafaka wa kuanzisha jukwaa hili kama chombo cha uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa sera na miradi ya kilimo-misitu,” amesisitiza Irunga.

Kwa mujibu wa wadau hao, jukwaa hilo litasaidia kuratibu utekelezaji, kufuatilia matokeo na kupanua mbinu bora za kilimo misitu katika nchi za Afrika Mashariki, likiwa chachu ya kukuza uchumi wa kijani na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Wamesema kilimo mseto ni suluhisho la ustahimilivu katika maeneo kame na kwamba majadiliano ya kisera yanapaswa kuambatana na hatua za vitendo.

Mtaalamu wa Kilimo Mseto kutoka Uganda, Sarah Kizia amesema kilimo mseto ni njia ya vitendo, rahisi kupanua na yenye tija kiuchumi kwa jamii za maeneo kame, akisisitiza umuhimu wa kukiwekea sera wezeshi ili kuleta matokeo chanya ya muda mrefu.

Kizia amesema kilimo mseto kinaendana na vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa na kimataifa, ikiwamo kutokomeza njaa, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kurejesha mifumo ya ikolojia.

“Kilimo mseto huenda kisitatue kila changamoto ya maeneo kame, lakini ni miongoni mwa nyenzo zenye nguvu zaidi tulizonazo za kurejesha mandhari, kuimarisha maisha ya watu na kuongeza ustahimilivu,” amesema Kizia.

“Kuwajengea uwezo na kuwapa mitaji vijana, pia yametajwa kuwa mambo yatakayofanikisha kuongeza uwekezaji katika kilimo mseto.”

 Amesisitizwa kuwa mfumo huo ni suluhisho la kudumu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuhakikisha usalama wa chakula na ajira kwa vijana Afrika Mashariki.

Mwakilishji wa vijana kutoka Kenya, Miriam Chemtai amesema katika kuhakikisha malengo ya muda mrefu yanafanikiwa, lazima vijana washirikishe kwakuwa wao ni kundi kubwa miongoni mwa watu wa ukanda huu.

“Tunapendekeza vijana wawezeshwe kujiunga katika makundi mbalimbali ili waweze kupata mitaji na kufanya kazi kwa pamoja.

“Pia, wajengewe uwezo ili waweze kufahamu kuhusu kilimo cha shamba darasa, kwa kupata mafunzo, usimamizi katika programu mbalimbali na kufanya miradi mbalimbali na kuweza kupata masoko na kutengeneza nafasi za ajira,” amesema.

Wataalamu hao wamependekeza wakulima wa kilimo mseto wapewe msamaha wa kikodi na bei nzuri ya mazao

Mtaalamu wa masuala ya kilimo kutoka Tanzania, Omary Mwaimu ametoa wito kwa Serikali na wadau wa maendeleo kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo mseto, ikiwamo kuwapatia msamaha au unafuu wa kikodi ili kuongeza hamasa ya uwekezaji katika sekta hiyo.

Mwaimu amesema hatua hiyo itawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kulinda mazingira.

“Wakulima wawezeshwe ili waweze kujikita zaidi kwenye kilimo mseto. Ni muhimu wapatiwe msamaha wa kikodi au unafuu wa kikodi, wawezeshwe kuuza hewa ya ukaa, na mazao yanayotokana na kilimo mseto yapewe bei nzuri zaidi ambayo itatoa hamasa kwao kuwekeza,” amesema Mwaimu.

Ameongeza kuwa utoaji wa motisha kama hiyo utasaidia kuongeza idadi ya wakulima wanaojihusisha na kilimo mseto, hivyo kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuimarisha usalama wa chakula katika maeneo kame ya Afrika Mashariki.

Wataalamu hao pia wameeleza kuwa, ili teknolojia yoyote iweze kuchukuliwa na kutumika katika kilimo ni lazima mkulima awezeshwe na eneo la ugani liweze kuimarishwa.

Mtaalamu wa kilimo kutoka Tanzania, Dk Peter Mlay amesema wakati wa utekelezaji mashambani, kuna changamoto nyingi ambazo wakulima wanakumbana nazo, hivyo ili teknolojia isaidie eneo husika ni vema majaribio yafanyike.

“Maana kuna teknolojia inaweza kutatua changamoto katika maeneo yote, tatizo la ukosefu wa maji kwenye udongo, rutuba kwenye udongo au mmomonyoko wa udongo. Si zote zitafanya kazi katika maeneo yote. Pia, kunaweza kuwa na baadhi ya teknolojia ikatatua matatizo yote kwa pamoja,” amesema.

Amesisitiza kuwa, ni vema kuwapa elimu hiyo wakulima waweze kuwa wabunifu na kufanya majaribio ya teknolojia hizo kwenye mashamba yao, kuhusu tatizo linalowakumba na kisha kurudi kupata elimu kwa wataalamu.

“Upande wa kuboresha huduma za ugani, wagani wetu lazima wapate mafunzo yanayoendana na kilimo mseto na pia lazima tuhakikishe tunaboresha uhusiano na wakulima wetu kuhusu utabiri wa hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi,”amesema Dk Mlay.

Mwakilishi wa wanawake kutoka nchini Kenya, Elizabeth Githendu amesema jamii za Afrika Mashariki, wakiwamo wakulima, wana uelewa wa kina kuhusu miti gani inafaa kupandwa mashambani ili kurutubisha udongo, na pia majani au mimea gani ikikua shambani hupunguza rutuba ya udongo.

Wanajua pia majani gani ni bora kwa lishe ya mifugo yao, na jinsi ya kuweka uwiano kati ya miti, mazao na malisho katika mfumo wa kilimo chenye tija.

Githendu amesema katika ngazi ya mandhari ni muhimu jamii ziwe sehemu ya ubunifu na uamuzi.

“Tunahitaji kuhusisha wadau kupitia mikutano ya kitaalamu ili kusaidia kuimarisha umiliki wa jamii, uendelevu na ukuaji wa pamoja.

“Jambo jingine muhimu ni namna tunavyoweza kudokumentisha na kushirikisha maarifa haya. Tafiti zinazoendelea zitasaidia jamii kujaribu mbinu mpya, tukitambua kwamba si kila mbinu itafanya kazi kila mahali, inaweza kufanikiwa eneo moja lakini isiwe na matokeo mazuri eneo jingine,” amesema Githendu.