Wahamiaji haramu 38 wa Ethiopia wanaswa wakiingia nchini bila kibali

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia raia 38   wa Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila kibali.

Pia, linamshikilia dereva na mmiliki wa gari aina ya Toyota Noah, Stanslau Mazengo (51), ambaye alikuwa akiwasafirisha  kwa kutumia njia za vificho.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin  Kuzaga amesema hayo leo Jumatano Novemba 12, 2025 na kubainisha kwamba, walikuwa  wakisafirishwa kupitia pori la ranchi ya Matebete Kijiji cha Igumbilo, Kata ya Chimala Wilaya  ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Katika hatua nyingine, Kamanda Kuzaga amesema  mtuhumiwa Stanslau baada ya kuhojiwa, amekiri kuwasafirisha wahamiaji hao haramu na alikuwa akiwapeleka kuwahifadhi kwenye nyumba moja huko Chimala.

“Watuhumiwa walikuwa wakiwasafirisha kwa njia za kificho kwa lengo  la kuwapeleka nchini Afrika Kusini,” amesema kamanda huyo.


Wakati huohuo , Kuzaga ameonya wananchi wenye tamaa na fedha  kuacha mara  moja kuwezesha  raia wa kigeni kuingia nchini bila kufuata utaratibu, badala  yake wawape maelekezo sahihi ya kuingia nchini kwa kuwasiliana na mamlaka husika .

Ametoa wito kwa wakazi wa Mbeya, kuwa mabalozi wa kutoa taarifa kwa siri kwa mamlaka za ulinzi na usalama, sambamba na kuwataka waliokamatwa na Polisi kubanwa ili waeleze mitandao yao.