Kila mwaka ifikapo tarehe 12 Novemba, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege (ATSEP International Day), siku maalum ya kutambua mchango muhimu wa wataalamu hawa katika kuhakikisha usalama wa anga duniani.
Kwa wasafiri wa anga, kila ndege inaporuka na kutua salama ni matokeo ya juhudi za watu wengi – wakiwemo marubani, waongoza ndege, wahudumu na maafisa wa usalama. Hata hivyo, kuna kundi muhimu la wataalamu ambao kazi yao mara nyingi haionekani kwa macho ya abiria, lakini mchango wao ni mkubwa katika kuhakikisha anga linabaki salama muda wote.
Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege ni wataalamu wa kielektroniki wanaohusika na usanifu, usimikaji, ufuatiliaji na matengenezo ya mifumo ya kielektroniki na programu zinazotumika kutoa huduma za uongozaji ndege. Mifumo hii ni pamoja na mitambo ya mawasiliano, urambazaji na ufuatiliaji (CNS – Communication, Navigation and Surveillance systems) ambayo inapatikana katika viwanja vya ndege na maeneo ya kimkakati nchini.
Wataalamu hawa hufanya kazi kwa saa 24 kila siku, kuhakikisha vifaa hivi vinafanya kazi kwa viwango vilivyowekwa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), ili kuruhusu ndege kupaa na kutua kwa usalama. Huduma wanazotoa zinawanufaisha waongoza ndege, marubani, pamoja na watoa taarifa za anga kote nchini.
Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chama cha wahandisi wa mitambo ya kuongoza ndege “Tanzania Air Traffic Safety Electronics Association” (TATSEA) , kimeadhimisha siku hii muhimu kwa kufanya hafla katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Rais wa chama hicho, Mhandisi Angela Kabali, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi wa Mitambo ya Kuongozea Ndege, Mhandisi Zawadi Maalimu, sambamba na wakuu wa vitengo kutoka vituo mbalimbali vya uhandisi wa anga nchini. Wahandisi walipata fursa ya kuonesha shughuli wanazofanya na kusherehekea kwa kukata keki kama ishara ya umoja na utambuzi wa mchango wao katika sekta ya anga.
Kwa upande wa kimataifa, maadhimisho haya mwaka huu yanafanyika Cape Town, Afrika Kusini, ambapo Mkutano Mkuu wa 53 wa Shirikisho la Vyama vya Kitaaluma vya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege Duniani (IFATSEA – International Federation of Air Traffic Safety Electronics Associations) unaendelea tangu tarehe 9 hadi 14 Novemba 2025.
Kwa ujumla, maadhimisho haya yanakumbusha umuhimu wa teknolojia na utaalamu katika kuhakikisha anga linaendelea kuwa salama, na ndege kuendelea kuruka kwa ufanisi bila hatari.
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi wa Mitambo ya Kuogozea Ndege, Mhandisi Zawadi Maalimu (wa tatu kushoto) akikata keki pamoja na Wahandisi wa Mitambo ya Kuogozea Ndege wakiongozwa na Rais wa chama cha Wahandisi wa Mitambo ya kuongoza Ndege (TATSEA), Mhandisi Angela Kabali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege (ATSEP International Day)
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi wa Mitambo ya Kuogozea Ndege, Mhandisi Zawadi Maalimu akizungumza na wakuu wa vitengo kutoka vituo mbalimbali vya uhandisi wa anga hapa nchini wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege (ATSEP International Day).
Rais wa chama cha Wahandisi wa Mitambo ya kuongoza Ndege (TATSEA), Mhandisi Angela Kabali akizungumza jambo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege (ATSEP International Day) yanayofanyika kila tarehe 12 Mwezi wa Novemba ya kila mwaka.
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi wa Mitambo ya Kuogozea Ndege, Mhandisi Zawadi Maalimu (kulia) akilishwa keki na Rais wa chama cha Wahandisi wa Mitambo ya kuongoza Ndege (TATSEA), Mhandisi Angela Kabali (kushoto) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege (ATSEP International Day), siku maalum ya kutambua mchango muhimu wa wataalamu hawa katika kuhakikisha usalama wa anga duniani.
Rais wa chama cha Wahandisi wa Mitambo ya kuongoza Ndege (TATSEA), Mhandisi Angela Kabali akiwalisha baadhi ya Wahandisi wa Mitambo ya kuongoza Ndege katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege (ATSEP International Day).
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi wa Mitambo ya Kuogozea Ndege, Mhandisi Zawadi Maalimu kiwa kwenye picha ya pamoja na wakuu wa vitengo kutoka vituo mbalimbali vya uhandisi wa anga hapa nchini wakiongozwa na Rais wa chama cha Wahandisi wa Mitambo ya kuongoza Ndege (TATSEA), Mhandisi Angela Kabali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege (ATSEP International Day).













