KOCHA wa Azam FC, Florente Ibenge amesema waamuzi wameikwamisha kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo waliyotoka sare ya bao 1-1, lakini hilo ameachana nalo na sasa akili yake iko DR Congo akiwaza namna watakavyotoka na poiti tatu, huku akifungukia ubora wa AS Maniema akifahamu kwamba wapinzani wao hao wana timu yenye rekodi bora kushinda kikosi chake.
Novemba 21, mwaka huu, Azam itakuwa nchini DR Congo kuikabili Maniema katika mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hizo zipo Kundi B sambamba na Nairobi United ya Kenya na Wydad kutoka Morocco.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema, kwa sasa hawazi kabisa matokeo yaliyopita ingawa timu hiyo imetoka na sare mara mbili mfululizo katika Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania na Namungo zote kwa matokeo ya 1-1. Kabla ya hapo iliichapa Mbeya City hivyo imekusanya pointi tano katika Ligi Kuu Bara na kukamata nafasi ya 11.
Alisema kuwa, shida imekuwa kwao lakini pia waamuzi hawakwepi lawama, kwani wamekuwa wakifanya vitendo vinavyoigharimu kikosi chake.
“Bahati mbaya sana kwenye mechi tulizopata sare tumekuwa tukikumbana na makosa ya waamuzi yanayotupunguzia kasi ya kufunga mabao, lakini hatuwezi kulalamika sana, tunasonga mbele,” alisema ibenge.
“Jambo muhimu ambalo nimelichukua mimi na wachezaji ni kutengeneza nafasi nyingi zaidi na kuzitumia ili hata mechi iwe ngumu vipi lazima tupate pointi tatu.”
Kocha huyo raia wa DR Congo, ana kibarua cha kuiongoza Azam iliyofuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi michuano ya CAF kusaka rekodi zaidi kimataifa.
Kuhusu wapinzani wanaokwenda kukutana nao, Ibenge alisema Maniema sio timu rahisi kama wengi wanavyodhani kwani anaifahamu vyema. “Kwa sasa nimeanza hesabu ya kuwaangalia Maniema, ni timu ninayoijua, lakini ni ngumu kutokana na ubora walionao.
“Ukweli ni kwamba Maniema ina uzoefu na mechi za makundi Ligi ya Mabingwa, kwa sababu msimu uliopita iliishia hapo ukilinganisha na Azam, lakini bado naamini timu yetu itakwenda kuweka rekodi nyingine kubwa,” alisema kocha huyo aliyewahi kuipa RS Berkane ya Morocco ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.