Aucho mambo safi, kuivaa CR Belouizdad

SINGIDA Black Stars inajiandaa kusafiri kwenda Algeria kwa ajili ya pambano la kwanza la makundi la Kundi C la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CR Belouizdad na habari nzuri kwa mashabiki wa klabu hiyo ni kurejea kwa kiungo nyota wa kikosi hicho aliyekuwa majeruhi.

Kiungo Khalid Aucho aliyekosa mechi iliyopita ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji kutokana na kuwa majeruhi, amerejea na kuliwahi pambano hilo litakalopigwa Novemba 22 na kulifanya benchi la ufundi kuchekelea likiamini uzoefu wake utaibeba timu hiyo dhidi ya Waarabu.

Kocha msaidizi wa Singida BS, David Ouma amesema kiungo huyo yupo fiti na tayari ameanza mazoezi sambamba na wachezaji ambao hawajaitwa kwenye vikosi vyao vya timu za taifa ambavyo vina mchezo wa kirafiki.

“Aucho atakuwa sehemu ya kikosi katika mchezo unaofuata kwani tayari ameshaanza mazoezi. Timu ipo Dar es Salaam itakaa kambini wiki moja kabla ya safari ambapo tuna mpango wa kusafiri Novemba 19 tayari kwa ajili ya mchezo wetu wa kwanza,” amesema Ouma na kuongeza;

AUC 01


“Kocha mkuu ameacha programu zote kabla ya kurudi tayari kwa kuifuata CR Belouizdad hivyo tunaendelea na maandalizi tukifuata maelekezo aliyoyaacha mwalimu. Malengo ni kuona timu inakuwa na utimamu na ubora.”

Akizungumzia kilichomuweka Aucho nje ya uwanja, Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza amesema alikuwa anasumbuliwa na nyama za paja, lakini tayari amekaa sawa na ameshaanza mazoezi kwa ajili ya mechi zilizo mbele.

AUC 02


“Aucho amerudi anaendelea vizuri hata mchezo dhidi ya Pamba Jiji kocha alifanya uamuzi wa kumpumzisha tu lakini alikuwa na utayari wa kucheza mechi hiyo baada ya kupona.”

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, ni mmoja ya wachezaji walioisaidia Singida kutinga makundi licha ya kushiriki michuano ya CAF kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza katika nafasi ya nne Ligi Kuu Bara msimu uliopita nyuma ya Yanga, Simba na Azam FC.

Singida ilitinga hatua hiyo sambamba na Azam katika Kombe la Shirikisho huku Simba na Yanga zikifuzu Ligi ya Mabingwa na kuandika rekodi kwa Tanzania, baada ya kuing’oa Flambeue de Center ya Burundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1.