Dk Nchemba kutoka Makunda hadi kukalia kiti cha Waziri Mkuu

Jumanne ya Januari 7, 1975 katika kijiji cha Makunda, Wilaya ya Iramba, mkaoni Singida, alizaliwa mtoto wa familia ya wakulima na wafanyakazi wa kawaida.

Hapo ndipo ndoto yake ya elimu na hatimaye utumishi wa umma ilianza kwa hatua ndogo ndogo.

Sasa hivi, Dk Mwigulu Lameck Nchemba ni mmoja wa wanasiasa wenye nafasi ya juu nchini, akitokea si kwa bahati, bali kwa mchanganyiko wa maarifa ya kitaalamu, uamuzi wa kisiasa na kujitolea kwa watu wake.

Safari ya elimu ya Dk Nchemba ilianza Shule ya Msingi Makunda, ikapitia Shule ya Sekondari Ilboru na kisha Sekondari ya Mazengo ambako alihitimu mwaka 2000.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikopata shahada ya kwanza ya Uchumi (2004), kisha Uzamili (2006) na hatimaye PhD ya Uchumi, vyote katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kabla ya kuingia kikamilifu katika siasa, Dk Nchemba alifanya kazi kwa kipindi cha miaka kadhaa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama mtaalamu wa uchumi.

Mwaka 2010, Dk Nchemba aligombea ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Alichaguliwa kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi.

Tangu wakati huo, ameshika nyadhifa kadhaa za uwaziri.

Alianza kama Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Novemba 2015 – Juni 2016), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Juni 2016 – Julai 2018), Waziri wa Sheria na Katiba (Mei 2020 – Machi 2021), Waziri wa Fedha (Machi 31, 2021 – Novemba 2025), na sasa, kuanzia Novemba 13, mwaka huu, ameteuliwa na Rais Samia kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.

Fimbo ya Uongozi; mchanganyiko wa utaalamu na siasa

Kwa kuwa ana shahada ya juu zaidi (PhD katika Uchumi), Dk Nchemba si mwanasiasa tu, bali ni mtaalamu wa data, sera na namba.

Hii inaonekana wazi kwenye namna anavyodai uwajibikaji na uwazi hasa alipoteuliwa kuongoza Wizara ya Fedha.

Alipoibuka katika sakata la ‘Tegeta Escrow’ akiwa katika Wizara ya Fedha, alitoa kauli kwamba wote wanaohusika wawe chini ya sheria bila kujali cheo.

Alipoingia Wizara ya Fedha, iliyompa jukumu la kuandaa bajeti ya Taifa na kusimamia mapato na matumizi, alikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kukusanya mapato, kuboresha uwazi wa matumizi na kuhakikisha kuwa uchumi bado unakua licha ya mabadiliko ya kisera na uchumi duniani.

Katika mahojiano ya hivi karibuni, Nchemba aliweka wazi msimamo wa Serikali juu ya jinsi uchumi wa kilimo unavyopaswa kubadilika; kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo cha biashara.

“Tuna azma ya kufanya kilimo kuwa biashara katika mnyororo wake mzima,” alisema.

Pia, aliongoza uzinduzi wa ofisi ya kanda ya Kaskazini ya Tanzania Agricultural Development Bank (TADB) Arusha, ni ishara kwamba Serikali inawekeza kwenye kilimo, mifugo na uvuvi kama njia sahihi ya kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini.

Hivyo, alitoa msukumo kwa taasisi za umma kutumia mfumo wa ununuzi wa umma (National e-Procurement System – NeST) ili kuongeza uwazi na uwajibikaji. “Hakuna mbadala wa kutumia mfumo huu,” alisisitiza.

Hata akiwa katika jukwaa la kitaifa, Dk Nchemba hajawahi kusahau mizizi yake. Kwenye mikoa ya Iramba na Singida nyakati za mapumziko yake, amekuwa akifanya ziara kwa kitembelea wananchi akilenga kusikiliza kero zao, kushughulikia matatizo ya barabara, umeme, afya na elimu.

Kwa mfano, Aprili 2024 alienda maeneo ya Doromoni, Kidaru na Kisiri katika Wilaya ya Iramba na kuwaeleza wananchi juu ya utekelezaji wa miradi ya serikali.

Kama kila kiongozi aliye na nafasi yoyote ya juu ni wazi lazima atakabiliwa na changamoto za hapa na pale, hivyo hata kwa Dk Nchemba likadhalika amepitia pia.

Kutoka kwenye ongezeko la deni la umma, kukusanya mapato ya ndani ya serikali, kushughulikia athari za vita na janga la Uviko-19, hadi kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati ya serikali, yote haya yamekuwa sehemu ya majukumu yake.

Lakini zaidi ya hayo, ameweka wazi msukumo wa kuleta utawala wa sheria na uwajibikaji si maneno tu bali matendo, kama alivyokuwa akitoa kauli kuhusiana na kesi ya ‘Escrow.’

Kwa uteuzi wake kuwa Waziri Mkuu, hatua hii inaashiria kuongezeka kwa wigo wa majukumu yake, si tu uchumi na fedha, bali pia uongozi wa Bunge, kazi za kila siku za serikali na utekelezaji wa sera za Taifa.

Tanzania iko katika mwelekeo wa mabadiliko ya uchumi, miundombinu na teknolojia na Dk Nchemba amewekwa katikati ya mchakato huu.

Njia iliyo mbele yake ni kuweka mikakati ya muda mrefu ya Maendeleo (Dira 2050), kuhakikisha vijana wanapata ajira, sekta ya kilimo inakuwa nguvu ya uchumi na nchi inakuza teknolojia ya fedha (fintech) kama alivyosisitiza.

Mwigulu Nchemba si tu mwanasiasa wa wizara nyingi, wala si tu mtu wa namba, bali ana mchanganyiko wa kiasili, mizizi ya kijijini, elimu ya juu, uzoefu wa kitaalamu, na uwezo wa kisiasa.

Sasa, safari yake inawaacha wengi wakitazama kwa msisimko, kile ambacho atafanya katika wadhifa wake mpya: uchumi unaobadilika, sera zinazoeleweka, utawala wa uwazi na maendeleo ya watu wengi.

Tangu nchi ilipopata Uhuru, Dk Nchemba anakuwa Waziri Mkuu wa 13. Mawaziri wakuu waliomtangulia ni Julius Nyerere  (Septemba 2, 1960—Januari 22, 1962), Rashidi Kawawa (Januari 22, 1962—Desemba 9, 1962 na baadaye Februari 17, 1972—Februari 13, 1977), Edward Sokoine (Februari 13, 1977—Novemba 7, 1980 na baadaye Februari 24, 1983—Aprili 12, 1984), Cleopa Msuya (Novemba 7, 1980—Februari 24, 1983 na baadaye Desemba 7, 1994—Novemba 28, 1995).

Wengine ni Salim Ahmed Salim (Aprili 24, 1984—Novemba 5, 1985), Joseph Warioba (Novemba 5, 1985—Novemba 9, 1990), John Malecela (Novemba 9, 1990—Desemba 7, 1994), Frederick Sumaye (Novemba 28, 1995—Desemba 30, 2005), Edward Lowassa (Desemba 30, 2005—Februari 7, 2008), Mizengo Pinda (Februari 9, 2008—Novemba 20, 2015), Kassim Majaliwa Majaliwa (Novemba 19, 2015—Novemba 2025).