Na Mwandishi wetu – Bungeni Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Said Johari, amemtaja Waziri Mkuu mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Kiongozi mchapakazi, akidhihirisha uwezo wake wa kuwatumikia watanzania kwenye nafasi mbalimbali alizowahi kushika kwenye serikali za awamu mbalimbali.
Mhe. Johari amebainisha hayo leo Alhamisi Novemba 13, 2025 Bungeni Mjini Dodoma wakati akimnadi Mteule huyo na kusoma azimio la Bunge la Tanzania, muda mfupi kabla ya Bunge kumuidhinisha kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, kufuatia Rais Samia kumteua kushika nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa awali na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Mwanasheria Mkuu amesema Dkt. Mwigulu si mgeni kwa Wabunge na Watanzania, akisema uwezo wake wa kujituma usiku na mchana bila ya malalamishi kwa muda wote ni miongoni mwa yanayomtofautisha na wengine, yakiwa sababu pia ya Wabunge kuweza kumuidhinisha.
Uteuzi wa Mwigulu Nchemba mwenye umri wa Miaka 50 umetangazwa rasmi bungeni mjini Dodoma, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na kuthibitishwa kwa kura za ndio za Wabunge 369 kati ya 371 zilizopigwa huku kura mbili zikitangazwa kuharibika.
Safari ya kisiasa ya Mwigulu ilianza kupanda kasi mwaka 2010 aliposhinda ubunge wa Jimbo la Iramba Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alirudi tena bungeni mwaka 2015. Ndani ya chama chake amejipatia heshima kama kiongozi mwenye msimamo thabiti na anayejali nidhamu katika utumishi wa umma. Amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, mjumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na sekretarieti ya chama chake kwa miaka mingi.
Dkt. Mwigulu pia amewahi kushika nafasi mbalimbali serikalini. Alianza kama Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi mwaka 2015, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2016. Mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, nafasi aliyoishikilia hadi uteuzi wake kuwa Waziri Mkuu.