Dodoma. Kauli ya fyekeo na rato aliyoitoa Dk Mwigulu Nchemba muda mfupi baada ya kuthibitishwa na Bunge, kuwa Waziri Mkuu mteule, imewaibua wabunge wakimtaka kuiweka kwa vitendo ili isiwe kauli ya mdomoni.
Hata hivyo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande ambaye alikuwa msaidizi wa karibu wa Dk Mwigulu katika wizara hiyo, amesema ahadi za mteule huyo huwa haziachwi bila kutekelezwa na kwamba usimamizi wake kwa watumishi hautiliwi shaka.
Dk Mwigulu Nchemba jina lake limethibitishwa leo Alhamisi Novemba 13, 2025 na wabunge baada ya kuwasilishwa na Mpambe wa Rais Samia Suluhu Hassan, Mpambe wa Rais (ADC), Brigedia Jenerali, Nyamburi Mashauri na baada ya kupigiwa kura, alipata kura 369 kati ya 371 zilizopigwa ndani ya ukumbi wa Bunge huku kura mbili zikiharibika.
Katika maneno ya kushukuru mbunge huyo wa Iramba Magharibi mkoani Singida, mbali na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wabunge wote ikiwamo wa kambi ya waliowachache bungeni, lakini ametoa onyo kwa watumishi wazembe na walarushwa.
“Watumishi wavivu, wazembe na wala rushwa nakuja na fyekeo na rato lazima kila mmoja awajibike na tutekeleze ahadi alizozitoa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, watumishi na Watanzania wote lazima twende na gia ya kupandia mlima cha msingi ni kuwa chombo kifike salama,” amesema Mwigulu.
Fyekeo na rato ni zana zinazotumika kwa ajili kufyekea nyasi au kukusanyia majani kwa ajili ya malisho ya mifugo ama kwa mtu anayefanya usafi wa eneo lililo na nyasi.
Dk Mwigulu amesema katika uongozi wake atahakikisha watumishi wa umma wanatenga muda wa kuwasikiliza wananchi na inapobidi lazima waondoke maofisini waende wakatatue kero za watu.
“Watanzania wa mazingira ya chini watasikilizwa kwa nidhamu katika ofisi za umma, tutahakikisha watumishi wanakwenda kutatua kero za wananchi katika maeneo yao, lakini Dira ya Taifa ya Maendeleo imebeba matumaini makubwa ya Watanzania na kazi ni kubwa, twendeni tukaisimamie,” amesema Dk Nchemba.
Hata hivyo, Dk Mwigulu ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatizwa na wabunge kwa kushangiliwa, amesema mambo yote yaliyoongelewa kwenye dira, ilani na ahadi za viongozi yatatimia ikiwa Taifa litaendelea kumtanguliza Mungu na kuwa na hali ya amani kwani bila amani yote yanayotarajiwa hayawezi kufikiwa.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha Hamad Chande, amesema mara nyingi Dk Mwigulu huwa anayaishi aliyoyaahidi, hivyo hawezi kusema jambo ambalo hana uwezo w akulitekeleza.
“Uzuri wa huyu mheshimiwa, pande zote za Muungano anakubalika, sina shaka naye na hata hayo anayosema najua atakwenda kuyatekeleza kwa hatua, hana papara katika usimamizi wa mambo wala hawezi kurudi nyuma,” amesema Chande.
Chande amesema katika utendaji wa kazi na kiongozi wake huyo (Dk Mwigulu), hakuwahi kujuta kufanya naye kazi na wakati wote alifurahi ushirikiano na miongozi aliyokuwa akiipata kwa waziri huyo.
Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde amesema Dk Mwigulu ni kiboko ya nidhamu kwa watumishi wazembe na anaimani kubwa kuwa sasa Watanzania wanakwenda kupata haki lakini akamuomba aongeze kitu kimoja.
Lusinde amesema kuwa na fyekeo na rato ni sawa lakini usipokuwa na kiberiti haitakuwa na maana, inabidi majani yafyekwe na kukusanywa kisha kiberiti kiyachome.
Amesema nidhamu katika utumishi imeshuka na dharau zimekuwa ni nyingi, hivyo kukosekana kwa maelewano kati ya watumishi na wananchi jibu linakwenda kupatikana kwa Dk Mwigulu.
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Cecilia Pareso amesema uzoefu aliona na kazi alizozifanya kwenye wizara alizopitia Dk Mwigulu ndizo zinambeba na hawana shaka naye kwa jambo lolote.
Pareso amesema wana matarajio makubwa kutoka kwa Dk Mwigulu ambaye hufanya kazi zake kwa kujiamini bila kumuogopa mtu ili mradi akihisi kama hajamuonea.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), Mary Chatanda amesema wana imani kubwa na Dk Mwigulu kutokana na uimara wake na mapenzi yake kwa nchi, huku akimtaka akapiganie haki za wanyonge.
Chatanda amesema Dk Mwigulu atakwenda kupigania katika usimamizi wa ilani ya uchaguzi bila hofu kwa kuwa, alishiriki katika kuiandaa na ndiyo maana wamekubali kumthibitisha pasipokuwa na hofu.
Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu Ado amesema wabunge wa upinzani ambao ni wachache bungeni wanamkopesha imani Dk Mwigulu, wakitarajia kuwa atajikita katika kusimamia rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi.
Ado amesema wananchi wana matumaini kwamba Serikali mpya itasikiliza kilio cha muda mrefu cha kupata Katiba mpya.
Pia, amesisitiza kipaumbele cha Waziri Mkuu kinapaswa kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowakabili wananchi wa kawaida, huku akisisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji katika matumizi ya rasilimali za Taifa.
Mbunge huyo amewataka wabunge wote kuungana katika kuijenga Tanzania yenye misingi ya haki, usawa na maendeleo endelevu kwa wote.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussen Bashe katika ukurasa wake wa Instagram ameweka picha aliyopiga na Dk Mwigulu enzi wakiwa mawaziri, yeye (Bashe) wa kilimo na Dk Mwigulu, Fedha kisha akandika: “Hongera Comrade, pia pole. Umekabidhiwa jukumu hili na Mh Rais Samia Suluhu Hassan na Bunge tumekuthibitisha katika nyakati tofauti na nyakati zingine katika historia ya Taifa letu.”
“Wengi wanakifahamu CMR Mwigulu waziri, naibu waziri, naibu katibu mkuu wa CCM, wanakufahamu mtumishi wa BOT. Binafsi nakufahamu Mwigulu muuza tofali na daiwaka ambaye wakati ukipiga tofali Tegeta, mkeo alikuwa anapika mama Ntilie.”
“Nakufahamu Mwigulu ambaye mchunga ng’ombe ambaye alikuwa anapeleka mifugo pori la Milima ya Sekenke na Bonde la Wembele wakati wa kiangazi. Taifa leo limepata Waziri Mkuu daiwaka mpiga matofali ambaye anajua maisha ya mtu wa chini kabisa ambae anafahamu maana ya umasikini ni nini.”
“Binafsi sina mashaka na uwezo wako, dhamira yako ya kutumikia Taifa letu, changamoto zinazotukabili naamini zimepata mtu sahihi wa kumsaidia Mh Rais kukabiliana na umasikini wa Tanzania.”