::::::::
Imeelezwa kuwa Jumuiya ya nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ni jukwaa sahihi la kupata ufumbuzi wa Kudumu wa changamoto zinazozikabili nchi wanachama kama vile ukosefu wa amani, usalama na maendeleo endelevu.
Hayo yamebainishwa jijini Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Novemba 13, 2025 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kawaida wa Mawaziri wa ICGLR uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa DRC, Mhe. Judith Tuluka Suminwa.
Nchi wanachama zimetakiwa kuenzi Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo unaolenga kufikiwa kwa amani, usalama na maendeleo ya kweli kupitia ushirikiano, umoja na mshikamano bila kusahau kujitoa na kujituma kwa hali na mali kupigania malengo hayo.
Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa.
Tanzania katika Mikutano huo inaunga mkono agenda zinazojadiliwa ikiwemo ya amani na usalama na kusisitiza kuwa itaendelea kutoa mchango mkubwa kama inavyofanya katika nchi mbalimbali kuhakikisha kuwa amani ya kweli inapatikana kwenye Kanda.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Waziri Mkuu alisema kuwa nchi za ICGLR hazijafikia malengo ya Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya hiyo ambayo ni amani, usalama na maendeleo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuwa na umoja, ushirikiano na mshikamano ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto za kiusalama.
Alitaja ukosefu wa fedha na miundombinu duni ndani na baina ya nchi wanachama inachangia kwa kiasi kikubwa kutofikiwa kwa malengo hayo.
Viongozi hao wamehitisha hotuba zao kwa kusisitiza umuhimu wa nchi za ICGLR kubuni mikakati yao wenyewe itakayokwamua changamoto zao bila kutegemea msaada kutoka nje. Walihimiza umuhimu wa kuziwezesha taasisi za kikanda kwa rasilimali watu na fedha ili ziweze kushughulikia changamoto zinazotukabili zikiwemo za amani na usalama.




