Dar es Salaam. Katika kuhakikisha watoto chini ya umri wa miaka 18 wanadhibitiwa kutazama maudhui yasiyofaa, mtandao wa Instagram umekuja na mwongozo wa ukadiriaji wa filamu yaani PG-13.
Hii ina maana kuwa watoto wataona maudhui yanayofanana na yale yanayoruhusiwa katika filamu za PG-13. Tofauti na hapo hawataweza kuona chochote kisicho cha umri wao.
Kupitia hilo, sasa wazazi au walezi wataweza kuchagua kiwango kipya cha udhibiti mkali zaidi (Limited Content Setting).
Kupitia akaunti hizo wazazi watapata njia mpya za kutoa maoni na kuripoti maudhui ambayo wanaona hayafai kwa vijana wao.
Imetajwa hatua hiyo itasaidia watoto kutoona maudhui yasiyofaa ambayo kwa namna moja au nyingine yanaharibu kisaikolojia.
Mpangilio wa Limited Content
Unazuia maoni (comments) kabisa kwa watoto.
Unapunguza zaidi aina ya maudhui yanayoonekana.
Mwaka ujao utaongeza vizuizi kwa mazungumzo ya akili unde (AI).
Takwimu zinaonyesha asilimia 96 ya wazazi hasa wa Marekani wamefurahia kuwa na chaguo hili jipya.
Instagram imetoa fursa kwa wazazi kushiriki katika tathmini ya maudhui zaidi ya milioni tatu ili kuboresha sera hizi. Matokeo yanaonyesha kuwa chini ya asilimia mbili ya machapisho yaliyopendekezwa kwa vijana yalionekana hayafai kwa mtazamo wa wazazi.
Katika hili sasa wazazi pia wataweza:
Kushiriki katika tafiti za mara kwa mara kupitia programu ya Instagram.
Kuripoti machapisho wanayoamini hayafai kwa vijana wao, ambapo Instagram itayakagua kwa haraka na kutoa mrejesho.
Ikumbukwe mabadiliko haya yameanza kutekelezwa Marekani, Uingereza, Australia, na Canada, na yatakamilika kufikia mwishoni mwa mwaka 2025 kabla ya kuanza duniani kote.
Kwa mujibu wa Instagram kuanzia sasa, akaunti zote za vijana walio chini ya miaka 18 zitawekwa moja kwa moja katika mpangilio wa “13+”, bila uwezo wa kubadilisha bila ruhusa ya mzazi.
Katika hili Instagram inatumia teknolojia ya utambuzi wa umri (age prediction technology) kuwazuia wale wanaojaribu kujisajili kama watu wazima. Lengo ni kuhakikisha vijana wanaona maudhui salama na yanayofaa umri wao.
Kwa mujibu wa mfano wa filamu za PG-13, vijana bado wanaweza kuona maudhui yenye lugha kali kidogo au mapendekezo ya kimahaba, lakini Instagram inalenga kupunguza visa hivyo kwa kiwango cha chini kabisa.
Mabadiliko ya sera za maudhui
Sera hiyo mpya ya mtandao wa Instagram inaenda mbali zaidi kwa kuficha au kutoonyesha: Lugha kali au isiyo na maadili. Vitendo hatarishi au maudhui yanayohamasisha mienendo hatarishi.
Pamoja na maudhui yanayohusiana na matumizi ya tumbaku, pombe, bangi au bidhaa za watu wazima.
Mbali na hayo watoto hawataweza ku-follow akaunti zinazochapisha mara kwa mara maudhui yasiyofaa kwa umri wao.
Vilevile, maneno ya utafutaji yanayohusiana na mada nyeti kama pombe, vurugu au kujidhuru yatakuwa yamezuiwa.
Pia, maudhui yasiyofaa hayatapendekezwa katika Explore, Reels, au Feed, hata kama yametumwa na mtu anayefuatwa.
Aidha, sehemu ya kuchati ya DMs na Akili Unde (AI), kwa sasa Instagram zitafuata mwongozo wa PG-13, hivyo hazitatoa majibu yanayofaa watu wazima kwa watoto.