NAHODHA wa Tanzania Prisons, Salum Kimenya amesema Ligi Kuu Bara msimu huu ni ngumu, hata hivyo wanajipanga kwa mechi ijayo dhidi ya Tabora United itakayopigwa Novemba 22 kwani, wamejiandaa vizuri kupata pointi tatu ili kujiweka pazuri kiushindani.
Prisons itakuwa ugenini katika mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora na itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi mechi ya mwisho kwenye Uwanja wa KMC, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kimenya amesema timu iliyojiandaa vizuri ndio itakayopata ushindi huku akiweka wazi kuwa hawana hofu yoyote kuikabili Tabora United kwani wanaamini wao ni bora na wanazihitaji pointi tatu.
“Tunatarajia mchezo mzuri na wa ushindani kutokana na kila timu kutaka matokeo tutaingia uwanjani kushindana na tuna kila sababu ya kupata matokeo kutokana na maandalizi tunayoendelea nayo tunatambua Tabora United na wao wanatambua umuhimu wa pointi hizo tatu,” amesema Kimenya na kuongeza;
“Ligi ni ngumu ubora umeongezeka kuanzia wachezaji, mabenchi ya ufundi lakini pia chachu kubwa ni wadhamini ambao wanatupa nguvu ya kujituma zaidi. Ninachokiona sasa ni namna ambavyo timu bora zitakavyokuwa zinapata pointi tatu kutokana na ubora;
“Ubora wa ligi umeongezeka kutokana na kila msimu timu kuongeza ufanisi kiuchezaji na kiutendaji ndani ya uwanja ukiondoa wachezaji pia makocha wenye ubora wameongezeka,” amesema Kimenya.
Akizungumzia mchezo kwa ujumla Kimenya amesema wanaenda kukutana na timu shindani ambayo ina wachezaji wengi wazoefu licha ya kutokuanza vizuri msimu lakini wanatambua ubora wao wataingia kwa kuiheshimu.