Mama, wanawe wahukumiwa kunyongwa kwa kumuua baba wa kambo

Karagwe. Ni matukio nadra katika familia pale mama na wanawe wanapokula njama na kupanga mauaji kama ilivyotokea kwa Anastazia John na wanawe wawili waliokula njama na kumuua mumewe, na kuishia kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Hukumu hiyo ya kifo  dhidi ya mama na wanawe wawili imetolewa Novemba 10,2025 na Jaji Immaculata Banzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, masjala ndogo ya Karagwe na kuwekwa katika tovuti ya Mahakama leo Novemba 12,2025.

Kabla ya kutekeleza mauaji, Anastazia aliyekuwa mshtakiwa wa tatu, aliwapa wanawe hao, Vistus Zakaria aliyekuwa mshtakiwa namba moja na Erick Zakaria mshtakiwa wa pili, dawa za kienyeji kwa ajili ya kuwasafisha baada ya kuua.

Pamoja na kuwapa dawa na kutekeleza mauaji, bado hazikuwasaidia kukwepa mkono wa dola, kwani katika purukushani za kuua, mshtakiwa Vistus alijeruhiwa kwa panga na mwanamke aliyejitokeza kutoa msaada kwa marehemu.

Jeraha hilo lilimfanya atafute matibabu ambapo alienda kwa kaka yake aitwaye Richard Zakaria akimuomba amtafutie daktari wa kumtibu na alipombana aeleze nini kimemkuta, akasema Ezekiel amekufa na aliyemuua ni yeye (Vistus).

Mauaji hayo yalitokea Februari 10,2024 katika kijiji cha Kashanda kilichopo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, ambapo mama na wanawe hao walipanga na kutekeleza mauaji ya Ezekiel Zakaria ambaye alikuwa ni mume wa Anastazia.

Marehemu alikuwa ni mtoto wa kambo wa Anastazia ambapo baada ya mume wa Anastazia aitwaye Zakaria Marko kufariki dunia mwaka 2008, ndipo marehemu na mama yake wa kambo wakaamua kuoana, ndoa iliyotawaliwa na migogoro.

Migogoro kati ya wawili hao ilitokana na hatua ya marehemu kuchukua ardhi yote iliyoachwa na mumewe hadi kusababisha abaki bila ardhi ya kuwapa wanawe.

Hali hiyo iliwafanya mshtakiwa wa kwanza na wa pili kumchukia baba yao huyo na ndipo Februari 7, 2024 walikutana na mama yao na kupanga mipango ya kumuua ili kurejesha ardhi yao waliyodai imechukuliwa na marehemu.

Wakati wakipanga mauaji hayo, mama yao aliwapa dawa za mitishamba kwa ajili ya kuwasafisha ili wasigundulike baada ya kufanya kuua, ambapo mshtakiwa wa pili alinunua panga kwa ajili ya kulitumia kufanya mauaji hayo.

Ilipofika jioni, wawili hao walikodi pikipiki na kwenda kijiji cha Kashanda ambapo mshtakiwa wa kwanza alimkatakata kwa panga na kumuua baba yao.

Katika hukumu yake, Jaji Banzi alisema upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha shtaka dhidi ya washtakiwa na kwamba wao ndio walisababisha kifo cha marehemu na walifanya kwa nia ovu na  kudhamiria.

Jaji alisema amefikia uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi tisa wa Jamhuri yakiwamo maelezo ya kukiri kosa ya washtakiwa na kukataa utetezi wao kuwa hawakuandika maelezo hayo bali walilazimishwa tu na polisi kuyasaini.

Kulingana na Jaji Banzi, aina ya silaha waliyoitumia kumkata nayo marehemu kichwani mara tatu, mapigo waliyoyapiga na maeneo waliyopiga, yanathibitisha kuwa walikuwa na nia na dhamira ovu ya kumuua.

Hivyo Mahakama inawatia hatiani kwa kuua kwa kukusudia na kueleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, adhabu kwa kosa hilo ni moja, nayo ni kunyongwa hadi kufa.

Shahidi wa kwanza, Atanazia Anthony aliieleza Mahakama kuwa siku ya tukio, marehemu alikwenda nyumbani kwake huko Kashanda na baada ya mazungumzo, aliamua kuondoka licha ya mwanamke huyo kumsihi asiondoke kwake.

Kulingana na shahidi huyo, muda mfupi baada ya kuagana naye na kurudi ndani alisikia kishindo kikubwa kama vile mtu aliyeanguka na baada ya kusikia hivyo, alichukua silaha aina ya panga na kutoka nje kujua sauti hiyo ilikuwa ya nini.

Alipotoka nje alikuta tayari Ezekiel amejeruhiwa na kulikuwa na watu wawili ambao hawafahamu na mmoja alikuwa ameshika panga ambapo huyo mwenye panga alimvamia na kuanza kumkata kwa panga kichwani, mikono na vidole.

Katika kujitetea, shahidi huyo alisema alifanikiwa kumkata mtu huyo mkono wa kulia, na ndipo shahidi huyo akakimbilia nyumbani kwa mtu aliyemtaja kuwa ni Jovin huku akipiga mayowe ya kuomba msaada kutoka kwa majirani.

Baada ya Jovin kuona hali aliyokuwa nayo, alipiga ngoma ambayo huashiria kuna jambo ambapo watu wengi walijitokeza kutoa msaada ambapo alipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu ya majeraha mabaya aliyokuwa nayo mwilini.

Shahidi wa pili, Richard Zakaria ambaye ni kaka wa mshtakiwa wa kwanza na wa pili, alieleza kuwa Februari 11,2024 saa 12:30 asubuhi akiwa amelala, aliamshwa na mtoto aliyemwambia kuwa mshtakiwa wa kwanza anahitaji kumuona.

Aliamka na kwenda kuonana naye alimkuta ameumia mkono na alipomuuliza amefanyaje alikataa kueleza zaidi ya kumuomba ampeleke kwanza hospitali akatibiwe, huku akimwahidi kuwa baada ya kupata matibabu atamweleza kila kitu.

Alipomuuliza kama nyumbani alikotoka ni salama, alimjibu kuwa ni salama na wote ni wazima isipokuwa marehemu ambaye hakuwepo nyumbani, kauli ambayo hakuridhika nayo hivyo akamtaka ampe ufafanuzi unaoeleweka,

Ndipo akamweleza kaka yake kuwa Ezekiel ni marehemu na alipomuuliza amekufaje na kwa nini mkono wake umekatwa, ndipo akamwambia yeye ndiye amemuua na ndipo akajaribu kutafuta daktari kumtibu ndugu yake bila mafanikio.

Akiendelea kutafuta daktari, shahidi huyo alikutana na mtendaji wa kijiji, Jonasia Venant ambaye ni shahidi wa tatu na kumdokeza kuwa mshtakiwa wa kwanza yuko nyumbani kwake na amefanya tukio hilo la mauaji na anahitaji daktari.

Shahidi huyo wa tatu alimshauri kuendelea kumtafutia matibabu wakati yeye akienda kuwajulisha viongozi na taarifa hizo zilifika kituo cha Polisi Karagwe, ambapo maofisa wa Polisi walifika na kufanikiwa kumtia mbaroni Vistus.

Polisi walimchukua mshtakiwa wa kwanza na kumpeleka hospitali ambapo uchunguzi ulianza mara moja na washtakiwa wengine  walikamatwa na kufikishwa Polisi kwa mahojiano, ambapo walikiri na kueleza mwanzo mwisho.

Mashahidi wengine ambao ni maofisa wa Polisi walieleza namna walivyofika eneo la tukio, kushiriki katika uchunguzi wa mwili wake, kukamata watuhumiwa wa mauaji hayo, huku daktari aliyefanya uchunguzi akieleza sababu za kifo chake.

Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza alikiri kumuua marehemu lakini akasema hakudhamiria kumuua na kueleza kuwa Februari 10,2025, marehemu alimpigia simu na kumwita nyumbani kwake kuna kazi anataka aifanye.

Alipofika, baba yake wa kambo alianza kumshambulia akimtuhumu kuwa yeye ndio kiini cha mgogoro kati yake na mkewe na alipomuuliza kivipi, hakumjibu na badala yake alimpa dakika moja awe ameondoka hapo nyumbani kwake.

Baadaye marehemu aliingia ndani ya kibanda chake na kutoka na panga na kujaribu kumkata nalo lakini alifanikiwa kulikwepa, alipojaribu kwa mara ya pili alifanikiwa kumkata katika mkono wake wa kulia.

Mshtakiwa huyo alieleza kuwa katika kujitetea alifanikiwa kumzidi nguvu marehemu na kunyang’anya panga na kulishika na mkono wa kushoto na kujaribu kukimbia, lakini marehemu alimkimbiza na ndipo alitumia panga dhidi yake.

Kwa upande wake, mshtakiwa wa pili alikanusha kushiriki mauaji hayo na kwamba siku ya tukio alikuwa msituni akichoma mkaa na aliporudi nyumbani jioni ndipo aliposikia taarifa za mauaji ya kaka yake na alishiriki maziko yake.

Mshtakiwa wa tatu naye alikanusha kumuua marehemu wala kupanga mauaji hayo kwa kushirikiana na mtu yoyote miongoni mwa washtakiwa wenzake, na kwamba alikamatwa na Polisi jioni baada ya kushiriki mazishi ya mumewe.