Michango ya NSSF yaiponza kampuni ya SCI Tanzania, sasa kulipa Sh2.3 bilioni

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeiamuru Kampuni ya SCI Tanzania Limited kulipa michango ya wafanyakazi wake kwa zaidi ya miaka mitatu kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), yenye thamani ya zaidi ya Sh2.3 bilioni.

Fedha hizo ni malimbikizo ya michango ya wafanyakazi kati ya Machi 2021 hadi Julai 2024.

Maombi hayo ya madai namba 5966/2025 yalifunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bodi ya Wadhamini wa NSSF, wakidai kampuni ya SCI Tanzania Limited.

Ilielezwa mahakamani kwamba wadai hao wawili wanadai Sh1.64 bilioni ikiwa ni michango ambayo haijarejeshwa, pamoja na faini zinazopaswa kulipwa kwa NSSF.

Hukumu hiyo imetolewa Novemba 11, 2025 na Jaji Arnold Kirekiano, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani, Jaji Kirekiano aliamuru kampuni hiyo kulipa jumla ya Sh2.3 bilioni, ikiwa ni malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wake.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mdaiwa ameshindwa kupeleka michango ya wanachama wa NSSF kwa kipindi hicho, yenye thamani ya zaidi ya Sh1.64 bilioni, na adhabu ya kulimbikiza ikafikia Sh685.2 milioni, na hivyo kufanya jumla iwe zaidi ya Sh2.3 bilioni.

Nakala ya hukumu hiyo inaonesha kuwa NSSF, kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, iliwasilisha madai hayo baada ya barua ya kumbusho iliyopelekwa kwa kampuni hiyo Septemba 2, 2024, ikitaka kutekelezwa wajibu wa kisheria juu ya utumiaji wa michango ya wanachama, kushindikana.

Katika maombi hayo, wadai walikuwa wakiomba Mahakama iiamuru kampuni hiyo kulipa deni la Sh1.647 bilioni, ikiwa ni michango ya wanachama ambayo haijalipwa kati ya Machi hadi Julai 2024.

Pia, mfuko huo uliiomba Mahakama iiamuru kampuni hiyo kulipa Sh685.2 milioni, ikiwa ni faini kwa mujibu wa sheria, ambayo inataja kuwa ni mchango wa ziada wa kisheria kwa kuzingatia kiwango cha riba ya asilimia tano kwa mwezi kwa mwajiri atakayechelewesha mchango, ambacho huendelea kupanda hadi deni lote litakapolipwa.

Maombi mengine ni gharama za shauri hilo na gharama nyingine zinazohusiana na kufungua kesi, pamoja na nafuu nyingine ambayo Mahakama itaona inafaa kutoa.

Jaji Kirekiano amesema Mahakama ilitoa kibali kisicho na masharti kwa Kampuni ya SCI Tanzania Limited kufika na kujibu shauri hilo la madai, lakini kampuni hiyo ilishindwa kuwasilisha utetezi wake ndani ya muda uliowekwa kisheria.

“Ni msimamo wa sheria kwamba pale ambapo shauri la muhtasari halitetewi, tuhuma katika lalamiko huchukuliwa kuwa zimekubaliwa,” amesema Jaji Kirekiano akirejelea uamuzi wa kesi ya CRDB Bank Limited dhidi ya John Kagimbo Lwambagaza (2002) TLR 117.

Baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa, Mahakama iliridhika kuwa SCI Tanzania Limited imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria, na hivyo ikaamuru kampuni hiyo kulipa zaidi ya Sh2.3 bilioni, pamoja na riba ya asilimia tano kwa mwezi kwa kuchelewesha hadi pale madeni yote yatakapolipwa.

Aidha, Jaji huyo ameamuru kampuni hiyo kulipa gharama zote za kesi.