Mwenyekiti wa Chadema mbaroni, ahojiwa madai ya uharibifu wa mali

Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel amekamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, kisha kuachiwa kwa dhamana.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Alhamisi Novemba 13, 2025, Wakili wake, Panga Bungaya amesema Welwel alikamatwa jana Novemba 12, 2025, eneo la Kibaoni, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Amesema baada ya kukamatwa alihojiwa kufuatia tuhuma mbili zinazomkabili ambazo ni kuharibu mali pamoja na kuhamasisha wengine kuharibu mali.

“Alihojiwa nikiwepo pale kituoni (Karatu) ambapo anakabiliwa na tuhuma mbili ambazo ni kuharibu mali pamoja na kushawisi wengine kuharibu mali,” amesema na kuongeza:

“Baada ya mahojiano, Polisi waliruhusu apewe dhamana na baada ya kudhaminiwa ametakiwa kwenda kuripoti kituoni asubuhi ya leo Alhamisi.”

Juzi Jumatatu, Novemba 10, 2025, Jeshi la Polisi liliwaachia kwa dhamana viongozi waandamizi wa Chadema, akiwemo John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara.

Kwa mujibu wa wakili wao, Hekima Mwasipu, dhamana hiyo iliwataka viongozi hao walioachiwa jioni kuripoti Jumanne saa 5 asubuhi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.

Mbali na Heche, wengine ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, maarufu kama Boni Yai.

Lema, Golugwa na Boni Yai ni miongoni mwa waliokamatwa hivi karibuni na Polisi ambao ilidai wanahusika dhidi ya maandamano yaliyozaa vurugu kabla na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro, Dodoma, Mara na Ruvuma.

Heche alikuwa anashikiliwa na Polisi tangu Oktoba 22, 2025 alipokamatwa nje ya geti la Mahakama Kuu Dar es Salaam, alipokuwa akienda mahakamani kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uhaini.