Nabii Mkuu Geor Davie ateuliwa UN-PAF Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Ngurumo ya Upako la jijini Arusha, Nabii Mkuu GeorDavie Moses ameteuliwa na Shirika la Mabalozi wa Amani la Umoja wa Mataifa (United Nations Peace Ambassadors Forum – UN-PAF) kuwa Balozi na Mwakilishi wa Afrika Mashariki.

Uteuzi huo umetangazwa hivi karibuni jijini New York, Marekani, ambapo Mwenyekiti wa Dunia wa UN-PAF, Balozi Kingsley Ossai, amethibitisha jukumu hilo jipya la kiongozi huyo wa dini.

Kufuatia uteuzi huo, Balozi Ossai ametuma barua za utambulisho rasmi kwa Serikali ya Tanzania, Ofisi ya United Nations Chapter Tanzania, pamoja na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa lengo la kumtambulisha Nabii Mkuu GeorDavie katika nafasi yake mpya ya kimataifa.

GeorDavie, ambaye pia ni mlezi wa Jumuiya ya Maombezi Tanzania (JMAT) Taifa, ni miongoni mwa viongozi wa dini nchini kutokana na mchango wake kwa jamii.

Balozi Ossai amesema GeorDavie amegusa maisha ya watu wengi kupitia miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kielimu, ikiwamo kusaidia vijana na wanawake kujiajiri na kuinua vipato vyao.

“Kazi hizi zimeendelea kumweka katika ramani ya viongozi wa kiroho wenye mchango mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania,” amesema Balozi GeorDavie.

Kupitia uteuzi huo, GeorDavie anatarajiwa kuendeleza falsafa yake ya kueneza amani na umoja katika nchi za Afrika Mashariki, akiwakilisha shirika hilo la UN-PAF kwenye majukwaa ya kikanda na kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka makao makuu ya UN-PAF, uteuzi wa GeorDavie unalenga kuimarisha juhudi za kuleta amani endelevu, ushirikiano wa mataifa, na maendeleo jumuishi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, GeorDavie ameshukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kutekeleza majukumu hayo mapya na kuomba ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali.