Pemba. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amefichua kuwa chama hicho kuandikiwa barua na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Zena Said inayowataka kupeleka jina la Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Othman maarufu ‘OMO’ hadi sasa bado hawajapeleka jina hilo, kwa madai hawajaridhika na mazingira ya kisiasa yaliyopo visiwani humo.
Wakati ACT Wazalendo, wakiweka msimamo humo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, leo Alhamisi Novemba 13,2025 ametangaza baraza jipya la mawaziri huku akiacha wizara nne, ambazo ni maalumu kwa mawaziri watakaotokana na chama hicho kikuu cha upinzani.
Wizara hizo ni Afya, Utalii na Mambo ya Kale, Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, akisema nafasi hizo zitakuwa wazi kwa siku 90 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
“Kama mnavyotambua kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, inataka chama au vyama vya upinzani, vilivyopata wajumbe katika Baraza la Wawakilishi tuwapatie nafasi za uwaziri na kuna fomula.
“Chama pekee kilichopata viti ni ACT Wazalendo waliopata viti 10 vya uwakilishi, ambapo nafasi zao katika baraza la mawaziri ni nne. Nimeiacha wazi nafasi hizo, hadi pale tutakapokubaliana kwamba wanaingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa au la,” amesema Dk Mwinyi.
Akizungumza na wanachama na viongozi wa ACT Wazalendo leo Alhamisi, Novemba 13,2025 katika ofisi ya chama hicho Mtambile, wilayani Mkoani Pemba, amesema waliandikiwa barua hiyo, Novemba 4,2025.
Katika mazungumzo yake, Othman amesema ACT Wazalendo hakitakuwa tayari kushiriki mazungumzo yoyote yanayolenga kuunda SUK bila ya kuheshimu misingi ya haki na matokeo halisi ya uchaguzi uliopita.
“Wanafanya wanayofanya kwa sababu wanaamini stahiki yetu ni nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais tu, jambo hili lazima…,” amesema Othman.
Othman amedai uchaguzi wa Oktoba 29, uligubikwa na kasoro mbalimbali hivyo, mazungumzo yoyote yatakayofanyika lazima yaendane na uamuzi ya wananchi uliodhihirika kupitia mchakato huo.
Katika uchaguzi huo ulioshindanisha vyama 11, Dk Mwinyi wa CCM, alishinda kiti cha urais kwa kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 akifuatiwa na Othman aliyepata 139,399 sawa na asilimia 23.22.
Kutokana na kura hizo, ACT Wazalendo kina sifa zote za kupeleka jina la mwanachama atakayeteuliwa na Dk Mwinyi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Katiba hiyo, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010, ibara ya 39 (3), kifungu kidogo (1), Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar atateuliwa iwapo chama chake kitapata asilimia 10 au zaidi kura za urais.
Katika mkutano huo, wenye lengo la kuzungumza na wanachama na viongozi kuhusu Oktoba 29, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar Ismail Jussa amesisitiza hawakuwa tayari kuingia katika mazungumzo na CCM ikiwa lengo kufunika ukweli au kupitisha mambo kwa urahisi.
Jussa amefafanua kuwa mazungumzo yoyote kati ya vyama hivyo, lazima yajikite katika kuhakikisha haki inatendeka, ili wale wote waliohusika kuvuruga uchaguzi kuwajibishwa mara moja.