Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ametoa wito kwa watumishi wa umma na maofisa wa Serikali mkoani humo, kujenga utamaduni wa kutumia siku za mapumziko na likizo kujifunza ujuzi wa uwekezaji, ikiwemo katika sekta ya madini, ili kujitayarisha kwa maisha baada ya kustaafu.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika mradi wa uchenjuaji na urutubishaji wa dhahabu unaojengwa na Kampuni ya Tampmed Mining Limited katika Kata ya Msasa, Wilaya ya Chato, leo Alhamisi Novemba 13, 2025, Shigella amesema maisha yanahitaji kujituma, ubunifu na kutokata tamaa.
Amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kutumia muda wao wa mapumziko kujifunza shughuli mbalimbali za kiuwekezaji badala ya kutumia muda mwingi katika starehe zisizo na tija.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martini Shigella alipotembelea ujenzi wa mradi binafsi wa uchenjuaji Dhahabu unaomilikiwa na Kampuni ya Tampmed Mining limited wilayani Chato.
“Maisha ni kupambana, ni kujituma na ni kutokata tamaa. Tuna watumishi wa Serikali ambao hawajui hata duara linavyochimbwa. Wakati wa wikiendi (mwisho wa juma) ambao haupo kazini, usikae tu kuangalia televisheni; nenda ukajifunze jinsi duara linavyochimbwa, au uone hatua za uchenjuaji wa dhahabu. Hivyo utapata maarifa yatakayokusaidia kupanga shughuli zako za kimaisha,” amesema Shigella.
Ameongeza kuwa watumishi wanapaswa kuanza kuweka akiba na kujifunza uwekezaji wakiwa bado katika ajira, ili watakapostaafu wawe na ujuzi utakaowawezesha kuendesha miradi yenye tija.
“Usisubiri hadi ustaafu. Wengine husema nikistaafu nitanunua daladala, lakini kila siku utakumbana na gharama za matengenezo. Ni bora kuanza mapema, ili ukistaafu uwe na maarifa yatakayokusaidia kufanya shughuli kama hizi kwa ufanisi,” amesema.
Katika ziara hiyo, Shigella ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkurugenzi wa Wilaya ya Chato pamoja na maofisa mbalimbali kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa na wilaya.
Amesema uthubutu katika umri wa ujana unachangia mafanikio ya baadaye kwa kila mfanyakazi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amewataka wafanyakazi na wananchi kuachana na malalamiko dhidi ya Serikali na badala yake wajenge utamaduni wa kuweka akiba na kujifunza ujuzi mbalimbali utakaowawezesha kunufaika na fursa zilizopo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita SACP Safia Jongo.
“Tumepata elimu kubwa kwamba maisha baada ya kustaafu yanawezekana. Tatizo ni kwamba baadhi ya watu wanalalamika kwamba hakuna maendeleo, ilhali wamekosa ubunifu na uwezo wa kutambua fursa zilizopo,” amesema Kamanda Jongo.
Aidha, amewahimiza vijana kuachana na matendo yasiyo na tija kama ubakaji, wizi na uporaji, na badala yake wachangamkie fursa za maendeleo zinazowazunguka.
“Nitoe wito kwa vijana, fursa zipo. Acheni ubakaji, wizi na uporaji mkidhani ndiyo njia za mafanikio. Tafuteni fursa halali ili mjikwamue kiuchumi badala ya kuilaumu Serikali,” amesema.
Kamanda Jongo pia amewahamasisha wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani Geita, hasa madini, akieleza kuwa hali ya usalama mkoani humo ni ya kuridhisha.