Sura ya baraza la mawaziri la Samia

Dar es Salaam. Utabiri kuhusu nafasi ya waziri mkuu umekwisha na tayari Dk Mwigulu Nchemba (50) ameteuliwa na kuidhinishwa na Bunge kushika wadhifa huo.

Kituo kinachofuata sasa ni kina nani watakaokuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri, ambalo Rais Samia Suluhu Hassan atakaa na Dk Nchemba kuliteua.

Hata hivyo, katika uteuzo huo lolote linaweza kutokea, kwa kuwa Rais Samia anatajwa akuwa amekuwa hatabiriki, kama anavyoeleza mmoja wa viongozi waandamizi serikalini, aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutoandikwa jina.

“Huu ni muhula wake wa mwisho, anaweza kuja na baraza la mawaziri ambalo hatukutegemea. Aliwahi kusema anataka wabunge vijana bungeni, si ajabu hata baraza lake likajaa vijana wengi.”

Licha ya hilo, wapo wanaowatazma baadhi ya wabunge kati ya sita walioteuliwa na Rais Samia kuwa sehemu ya baraza hilo, huku wengine wakisema zitashuhudiwa sura zilezile zilizokuwepo katika baraza lililopita.

Novemba 10, mwaka huu, Rais Samia aliwateuwa watu sita kuwa wabunge katika nafasi 10 alizonazo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.

Sita walioteuliwa wabunge ni Dk Dorothy Gwajima, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi Khamis Mussa Omar, Abdullah Ali Mwinyi, Dk Rhimo Nyansaho na Dk Bashiru Ally.

Dk Gwajima, Balozi Kombo na Dk Bashiru wanateuliwa kuwa wabunge kwa kipindi cha pili, baada ya awali kuteuliwa kushika nyadhifa hizo.

Kwa Dk Gwajima baada ya kuteuliwa mbunge pia aliyeuliwa kuwa Waziri wa Afya na baadaye akahamishiwa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, nafasi aliyodumu nayo hadi mwisho wa muhula.

Balozi Kombo naye, uteuzi wake wa kuwa Mbunge uliambatana na kupewa jukumu la kuiongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wadhifa aliodumu nao hadi mwisho.

Lakini, Dk Bashiru aliyewahi kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa CCM na Katibu Mkuu Kiongozi, yeye aliteuliwa kuwa mbunge katika Bunge la 12.

Katika baraza lililopita lililokuwa na wizara 26, kati ya hizo nne zipo ambazo zipo wazi kutokana na waliokuwa wanaziongoza kushindwa kurudi bungeni, wamepata nyadhifa nyingine au hawajateuliwa na Rais.

Wizara hizo ni Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, iliyokuwa ikiongozwa na Jerry Silla ambaye ameshindwa kwenye ubunge, Dk Stergomena Tax aliyekuwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambaye pia hajarudi bungeni. Alikuwa mbunge wa kuteuliwa.

Wizara ya Fedha iliyokuwa chini ya Dk Mwigulu Nchemba nayo iko wazi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Wizara ya nne ambayo iko wazi na iwapo Rais atataka kuendelea nayo ni ya Kazi Maalumu katika Ofisi ya Rais, Ikulu, iliyokuwa chini Kepteni George Mkuchika ambaye alitangaza kustaafu siasa.

Ingizo la baadhi ya wabunge wateule, mapengo ya wizara zilizo wazi na pengine hata Rais akiamua kuongeza au kupunguza baadhi ya wizara, vitasababisha baraza hilo kuonekana ama na sura mpya au wengi waliokuwemo kubadilishana nafasi.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwemo ni Dk Bashiru Ally, Nape Nnauye, Balozi Omar, Dk Gwajima, Balozi Kombo, Dk Nyansaho, Masanja Kadogosa, Paul Makonda na wengine waliomaliza na Rais Samia muhula uliopita.

Uwezekano wa Dk Bashiru kupewa moja kati ya nafasi hizo unatokana kwanza na taaluma yake ya sayansi ya siasa na utawala, nafasi zake kwenye awamu ya tano na ushiriki wake kwenye kampeni.

Miongoni mwa wanaotajwa kushika nafasi nyeti ni Dk Nyansako ambaye amewahi kufanya kazi Benki ya Azania na hadi anateuliwa kuwa mbunge alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) huku akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Kwenye nafasi ya Wizara ya Fedha jicho linatupwa kwa Balozi Khamis Omar ni mbobevu wa eneo hilo.

Mabadiliko hayatazamiwi sana katika Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwani Balozi Mahmoud Thabit Kombo anatajwa huenda nafasi ya kuendelea kushika wadhifa huo.

Kama ilivyo kwa Balozi Kombo, ndivyo inavyotarajiwa kuwa katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, ambako Dk Gwajima anapewa nafasi kubwa kuendelea nayo.

Eneo lingine linalotajwa huenda kusishuhudiwe mabadiliko ni katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (Tamisemi), Omar Mchengerwa anatazamiwa kuendelea nayo

Hali kama hiyo, huenda ikashuhudiwa pia katika Wizara ya Nishati, Dk Doto Biteko anaweza kuendelea na wakati huohuo akiendelea kuwa Naibu Waziri Mkuu.

Mtihani upo katika Wizara ya Ujenzi na ya Uchukuzi ambako kuna ingizo lenye kuleta ushindani. Ulega na Profesa Makame Marawa wanajikuta wakipamban ishwa nguvu na Kadogosa aliyekuwa Mkuruhenzi wa Mkuu wa (Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, Philemon Mtoi amesema katika baraza hilo la mawaziri, kutarajiwe baadhi ya sura zikijirudia, lakini mtazamo wa utendaji utabadilika maradufu.

Amesema kutakuwa na nidhamu na heshima ya kuwaangalia wananchi kama waajiri na si walalahoi na kauli za kejeli kwa raia hazitasikika tena.

“Kwa mara ya kwanza tunaweza kuwa na baraza litakalojikita katika kuwahudumia wananchi. Hii ni kutokana na yale yaliyoshuhudiwa,” amesema Mtoi.

Mwanazuoni huyo wa historia, amesema huenda kukawa na mabadiliko ya watu wachache watakaoingia katika baraza hilo, kutoka wale waliokuwepo, lakini wote watatenda kwa niaba ya wananchi.

Amesema baraza hilo litakuwa na nafasi ya kumshauri vema Rais na ushauri ukazingatiwa kabla ya kusubiri matokeo hasi.

“Ndani ya baraza hilo kutakuwa na hofu na pengine litakuwa na uhai kutokana na uhalisia wa mambo yalivyo,” amesema mwanazuoni huyo.

Kwa mtikisiko ulioshuhudiwa, amesema lazima kuwe na baraza litakalowezesha wananchi kuona kuwa Tanzania imezaliwa upya na sio mambo yaleyale.

“Lazima watendaji wasimame kutetea wananchi badala ya yule aliyekuteua kwa sababu wananchi wamekuwa hatari zaidi ya yule aliyekupa nafasi,” amesema Mtoi.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo analitazama baraza hilo, akisema sura ya bunge lililopo ndio itakayoakisi baraza la mawaziri.

Amesema baadhi ya wabunge ndio wanaoteuliwa kuwa mawaziri, hivyo walivyo wabunge ndivyo litakavyokuwa baraza la mawaziri.

“Hawa wabunge tuliwapataje ndio itakayoamua baraza litakuwaje. Kama Mbunge amechukuliwa kutoka wa tatu akaachwa wa kwanza, lazima amtumikie aliyemteua,” amesema.

Kwa upande mwingine, amesema walioteuliwa kuwa wabunge nao, ni miongoni mwa watakaoingia katika baraza hilo kwa kuwa, Rais huteuwa pale anapohisi huyo mtu ana sifa ya kuwa mahali fulani lakini amekosa kigezo cha ubunge.

“Baraza ili liwajibike, linategemea ukali wa Bunge. Bunge likoje na lina nguvu gani kuiwajibisha Serikali, ndio linafanya baraza liwajibike,” amesema Dk Masabo.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Theresia Mweikimba amesema kwa nyakati tulizopo linahitajika baraza la mawaziri lenye uwezo wa kuzikabili changamoto zilizopo si kuzipuuza.

Ameeleza linahitajika baraza lenye uwezo na nguvu ya kushauri na kumshawishi mkuu wa nchi katika mambo yanayohitaji hatua za haraka na lihakikishe anaifuata njia kwa masilahi ya Taifa.

“Zama za kumteua mtu kwa sababu ana maneno matamu katika kusifia, zimefika mwisho, watu wanahitaji mtu ambaye anakupongeza, wakati huohuo anaifanya kazi vizuri. Binafsi nawaona wengi wakirejea, lakini wapo watakaoachwa,” amesema.