TRA YAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA USALAMA WA BIASHARA ZAO


:::::::::: 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda leo tarehe 13.11.2025 amefanya ziara katika soko la Kimataifa ya Kariakoo jijini Dar es Salaam na kuwahakikishia wafanyabiashara usalama wa biashara zao.

Akiwa sokoni hapo Kamishna Mkuu amekutana na viongozi wa wafanyabiashara na wamachinga pamoja na wafanyabiashara wenyewe na kuwapa pole kwa kufunga biashara zao kwa muda katika kipindi cha uchaguzi pamoja na madhira mbalimbali waliyoyapata katika kipindi hicho.

“Nimekuja kuona shughuli mnazofanya lakini pia kuwapa pole kwa changamoto zilizotokea, nimekuja kuona biashara zinaendeleaje na nimefurahi kuona biashara zinaendelea kama kawaida na nimethibitishiwa na wauzaji nilioongea nao kuwa wanauza kama kawaida na wateja wanakuja,”amesema CG Mwenda.

CG Mwenda ameshuhudia shughuli za biashara zikiendelea kama kawaida katika soko la Kimataifa la Kariakoo na hali ikiwa shwari ambapo amewahakikishia wafanyabiashara kuwa TRA itaendelea kulinda ustawi wa biashara zao kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili.

“Biashara zenu binafsi ni biashara za Umma, na sisi ni wabia wa biashara hizo hivyo tunao wajibu wa kuzilinda na kuhakikisha zinastawi” amesema Mwenda.

Amesema kuimarika kwa biashara katika soko la Kariakoo kunahakikisha kufunguka kwa biashara katika maeneo mengine ya nje ya Dar es Salaam na nchi jirani na kuwataka viongozi wa wafanyabiashara wafanye tathmini ya athari zilizotokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi katika biashara zao ili kushauri hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Kariakoo Bw. Severin Mushi amesema hali ya biashara katika Soko la Kariakoo imeimarika na kueleza kuwa wateja na wafanyabiashara waliopo ndani ya Soko hilo wapo salama huku akitoa wito kwa wananchi kwenda kufanya manunuzi kama kawaida. 

Naye Mwenyekiti wa Wamachinga Bw.  Stephen Lusinde amesema biashara za Wamachinga ndani ya soko la Kariakoo na biashara nyingine zililindwa na vijana takribani 150 kipindi chote cha changamoto wakati wa uchaguzi na kuwahakikishia usalama wananchi wanaotaka kwenda Kariakoo kufanya manunuzi.

= = = = = =