Moshi. Ulaji usio sahihi kwa watoto umetajwa kuchangia ongezeko la watoto wenye uzito uliopitiliza, hatua inayowaweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza wakiwa bado wadogo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, Dk Jonas Kessy amesema wazazi wengi wamekuwa wakiwaanzishia watoto vyakula mapema kinyume na maelekezo ya kitabibu.
Ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza kwenye Wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo katika hospitali hiyo wanatoa huduma za bure za upimaji wa sukari, shinikizo la damu, uzito wa mwili pamoja na kutoa ushauri wa kiafya kwa wananchi.
Kessy ambaye pia ni Mratibu wa Huduma za Tiba katika hospitali hiyo, ameeleza kuwa lishe isiyo sahihi inasababisha watoto kuwa na uzito mkubwa kupita kiwango, jambo linalowaweka katika hatari ya kupata magonjwa kama kisukari na shinikizo la damu wanapokuwa wakubwa.
“Mtoto wa miezi mitatu unakuta ameshaanza kupewa vyakula au maziwa ya kopo, wazazi wakiamini kuwa hawana maziwa ya kutosha. Kitaalamu, mtoto anatakiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita bila kupewa chakula kingine,” amesema Dk Kessy.
Dk Kessy amewataka wazazi na walezi kufuata ushauri wa madaktari na wataalamu wa lishe wanaoutoa kliniki na kuongeza kuwa elimu kuhusu lishe sahihi kwa watoto inapaswa kuzingatiwa kwa umakini mkubwa.
Aidha, ameeleza kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiongezeka kila kukicha, hali ambayo inachangiwa na mabadiliko ya mfumo wa maisha na watu kutofanya mazoezi.
“Wanaoathirika zaidi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni watu wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea, lakini kutokana na mfumo wa maisha leo hii kijana wa miaka 30 ana presha au kisukari. Hii inatokana na ulaji usio sahihi, kutofanya mazoezi na kutumia vyakula visivyo na virutubishi vya kutosha,” amesema.
Dk Kessy amesema kila mtu anapaswa kufahamu kiwango chake sahihi cha uzito kulingana na umri na urefu, kwani tofauti kubwa zinaweza kuashiria hatari ya kupata magonjwa mbalimbali.
“Tunatakiwa kula mlo kamili, kufanya mazoezi angalau mara nne kwa wiki, kuepuka vyakula vya mafuta mengi, kupunguza unywaji wa pombe na kuepuka kabisa uvutaji wa sigara,” amesisitiza.
Dk Kessy amesisitiza kuwa kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara ni hatua muhimu katika kupunguza ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika jamii.
Mkazi wa Shiri, Wilaya ya Hai, Aminiel Munis, amesema huduma za upimaji wa afya ni muhimu kwani zinawasaidia wananchi kujitambua mapema.
Naye Olipya Kimario, mkazi wa Karanga, Manispaa ya Moshi, amepongeza huduma za upimaji wa bure, akisema zinawawezesha wananchi wengi kupata huduma ambazo awali walishindwa kuzimudu kutokana na changamoto za kifedha.
Kwa upande wake, Fatuma Juma, mkazi wa Msitu wa Tembo, ameomba Serikali kuongeza utoaji wa huduma hizo mara kwa mara ili wananchi waweze kufuatilia afya zao kwa urahisi.