Andabwile sasa mambo freshi Yanga

KESI iliyokuwa ikiendelea kati ya Yanga na kiungo wa klabu hiyo, Aziz Andabwile imemalizika baada ya pande zote kufikia makubaliano na sasa kila kitu kipo freshi.

Andabwile aliyewahi kuichezea Mbeya City na Fountain Gate kabla ya kutua Yanga, huu ni msimu wake wa pili ndani ya klabu hiyo.

Mwanaspoti inafahamu kwamba Andabwile alisaini mkataba wa miaka mitatu kwa makubaliano ya kulipwa fedha kwa awamu tatu.

Lakini, hivi karibuni mambo yalibadilika baada ya kiungo huyo kufungua kesi TFF kwa madai ya kutopewa ada ya usajili ya msimu huu 2025/26.

ANDA 01


Gazeti hili lilifanya mahojiano na uongozi wa TFF kupitia Mkurugenzi wa Sheria na Habari, Boniface Wambura, aliyekiri kuwa madai hayo yamefikishwa katika chombo hicho.

Baada ya muda mfupi kupitia mtandao wa kijamii, Andabwile alisema anaomba radhi kwa taharuki iliyotokea, huku akisema yeye na Yanga wameshafikia makubaliano.

Licha ya kiungo huyo kusema hayo, lakini kesi hiyo ilikuwa bado haijafutwa TFF hadi muda wake wa kusikilizwa ulipofika ambao ulikuwa ni jana.

ANDA 02


Hata hivyo, mwanasheria wa kiungo huyo, Judith Zebedayo alinukuliwa akisema ishu ya mchezaji huyo na Yanga lilikuwa suala la upungufu wa mawasiliano.

“Kila kitu kilikuwa kimekamilishwa na hapa taarifa zilifika kwa kuchelewa, lakini kwa sasa kila kitu kipo sawa.

“Mawakili wa pande zote mbili tumekuja TFF kutoa maelezo kwamba swala hili limefikia muafaka na kila pende ilishafanya maridhiano.”

ANDA 03


Andabwile ambaye kiwango chake kimeanza kuwateka mashabiki wa Yanga na taratibu wameanza kumsahau Mganda Khalid Aucho aliyetimkia Singida Black Stars.

Ni kama ameanza na kismati msimu huu, huku akiwa na rekodi ya kucheza dakika nyingi kuanzia michuano ya kimataifa mpaka ndani ya ligi.

Katika mechi nne za mashindano ilizocheza Yanga msimu huu, nyota huyo amecheza tatu kwa dakika zote 90, huku moja pekee dhidi ya Pamba Jiji akitokea benchi wakati timu hiyo ikishinda 3-0.

Yanga ilianza dhidi ya Simba na kushinda bao 1-0, ikafuata Wiliete Benguela ya Angola katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda 3-0.

Katika mechi hizo amefunga mabao mawili yote dhidi ya Wiliete akianza ugenini na kumalizia nyumbani, huku akiwakosha mashabiki kwa kiwango bora anachozidi kukionyesha.

Ikumbukwe, msimu uliopita 2024/25 Andabwile alicheza mechi tano pekee kwa dakika 125, akiwa hana rekodi ya kufunga wala kuasisti.