Askofu Nkwande: Kilichotokea Oktoba 29 aibu, fedheha walioshiriki mauaji kwa kutoa amri na kushabikia watubu

Mwanza. Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza limeadhimisha Misa maalumu ya kuwaombea wote waliofariki na kujeruhiwa, kuwapa pole Watanzania na kuzifariji familia zilizokutwa na madhira ya kupoteza ndugu katika matukio ya vurugu na maandamano yaliyotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Maandamano yaliyozaa vurugu yalitokea wakati na baada ya siku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025 maeneo ya mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Mara, Arusha, Dodoma, Mbeya, Songwe, Ruvuma na Geita na kusababisha vifo, majeruhi,  uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Adhimisho hilo takatifu limefanyika katika Kanisa Kuu la Epifania – Bugando Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza jana Alhamisi, Novemba 13, 2025 kuanzia saa 10:30 hadi 12:15 jioni, likiongozwa na Askofu wa Jimbo hilo, Renatus Nkwande.

‎Misa hiyo ambayo imehudhuriwa kwa wingi na mamia ya waumini wa dhehebu hilo jijini Mwanza, ni sehemu ya misa za kuombea marehemu ifikapo Novemba.

‎Akizungumza wakati wa kufungua misa hiyo na kwenye mahubiri yake, Askofu Nkwande amesema katika matukio hayo kasoro imepatikana kwenye Taifa la Tanzania, na kasoro hiyo ni ya kuilaani, kuisemea na kuikemea.

‎Askofu Nkwande amewapa pole waathirika wote, huku akisisitiza pole ya wote na ya kitaifa kwani Watanzania wote wamekumbwa na msiba wa kitaifa ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi.

‎”Tulikuwa tumefungwa kwenye boksi hatuoni nje ndani kuna kiza. Ni aibu na fedheha tunapaswa kuomba kisijirudie, walichokifanya ni dharau, fedheha kwa nchi yetu, ni msiba mkubwa ambao haujawahi kutokea lazima wote tupige magoti kumuomba Mungu msamaha.”

‎”Tumepitia hicho Watanzania, Taifa letu lilikosa heshima na wapo vijana wetu tuliowasomesha wakafanye kazi wamemwaga damu. Ni janga kubwa katika nchi yetu.”

‎Askofu Nkwande ameshangazwa na baadhi ya Watanzania ambao walikuwa wanachekelea matukio hayo, kushangilia, kuwapongeza wauaji, kutoa maneno ya mizaha na kejeli kwa waathirika waliopoteza maisha na kujeruhiwa, kwani matukio hayo yanatengeneza funzo baya kwa kizazi kinachojifunza leo.

‎”Tumeona video zikionyesha mauaji, huko siyo kujitetea bali ni kuendeleza mauaji. Tulichokiona tuna sababu ya kusema kabisa ule ni unyama, hawa wamemkosea Mungu na wametukosea sisi Watanzania, hivyo tunaalikwa kutubu na kuiamini injili.”

‎Akirejea neno la Mungu kutoka Injili ya Mathayo, Zaburi ya 13, Luka 6 na 25, na Hekima 3:1, Askofu Nkwande amewataka watu wote walioshiriki kwa kunyamazia uovu, kutoa amri, kushabikia kwa kutoa maneno ya kejeli, kutubu dhambi ya mauaji, huku akishauri pande zote kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

‎”Poleni sana Watanzania, hili liwe fundisho na kamwe lisijirudie, na kama kweli tunataka kumaliza turejee meza ya mazungumzo, na walioshiriki wakiri dhambi zao,” amesema Nkwande.

‎Amesema wapo waliofikwa na umauti katika harakati za kuonyesha hisia zao na kwamba walipaswa kusikilizwa lakini hawakusikilizwa, pia wapo waliokuwa majumbani, wanaotoka hospitalini na waliokuwa wanakimbia hovyo kwa woga kwa sababu Watanzania hawajazoea kusikia risasi.

‎Ambapo amewaombea wote waliofariki dunia Mungu awarehemu na kuwasamehe dhambi zao, huku akiwataka waumini kuwakumbuka ndugu na familia za waliopoteza watu wao kwenye matukio hayo, kwa kuwatembelea, kuwapa pole, kuwafariji na kuwapa moyo.

‎”Machoni pa wajinga panadhaniwa kwamba kufa kwao ni hasara kwao na kuondoka kwao ni kujitakia. Hivi kweli hatujui walichokuwa wanatafuta au walichokuwa wanaomba? Waliomba haki, usalama wa maisha yao, na kusikilizwa,” amesema Askofu Nkwande.

‎”Wasiokuwa na bunduki wala silaha waliokuwa na mdomo tu wapiga kelele wakauawa. Kuua ni dhambi, kisasi kwa mkiristo ni dhambi na wala usipange au kudhamiria kwenda kuua.”

‎Askofu ‎Nkwande amesema anashangazwa na watu wanaoua ili waungwe mkono na kutengeneza hofu ili kuogopwa, huku akiwataka wakistro kuacha visasi na kupanga mauaji ya kukusudia.

‎Muumini aliyeshiriki misa hiyo, Joyce Antony amempongeza Askofu Nkwande kwa maneno ya faraja kwani matukio hayo yalileta mshtuko mkubwa kwa wananchi ukizingatia hawajawahi kupata na maafa ya aina hiyo.

‎”Kwa kweli tumesikitishwa na kuumizwa na vijana wetu waliopoteza maisha na kupata majeraha. Naomba viongozi waliopo madarakani washikamane wawe na upendo,” amesema Joyce.

‎Naye, Liberatus Ndegeulaya amesisitiza pande zinazokinzana kurudi katika meza ya mazungumzo ili mambo yaliyotokea yasijirudie, kufikia muafaka na kuanza upya.

‎”Kupitia neno la Baba Askofu tunajifunza kwamba tunapaswa kutanguliza utu ambao unajengwa katika misingi ya haki ambayo inaleta amani,” amesema Ndegeulaya.