BODI ya Azam Football Club imemtangaza rasmi Octavi Anoro (42), raia wa Hispania, kuwa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa klabu hiyo, kwa mkataba wa miaka miwili utakaomalizika mwaka 2027.
Anoro anachukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa CEO, Abdulkarim Nurdin maarufu kama Popat, kupandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa klabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Azam FC, Anoro anakuja na uzoefu mpana wa kimataifa katika maeneo ya utawala, usimamizi na biashara ya soka, jambo linalotarajiwa kuimarisha mwelekeo wa kiutendaji wa klabu hiyo.
Katika hatua nyingine, Bodi ya klabu imemteua Rashid Seif Mohamed kuwa Msaidizi wa Mtendaji Mkuu (Assistant CEO). Rashid ni mhitimu wa Shahada ya Umahiri katika Utawala wa Michezo (Master’s in Sports Management) na pia anamiliki leseni ya ukocha ngazi ya pili kutoka Chama cha Soka cha England (FA).
Uteuzi huu mpya unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Azam FC kujijenga kiweledi, kuimarisha uongozi na kuendeleza mageuzi ya muda mrefu yatakayowezesha klabu kusonga mbele kwa kasi katika mpira wa miguu wa kisasa.