Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limesikitishwa na vitendo vya vurugu vilivyotokea Oktoba 29, vilivyosababisha watu kupoteza maisha na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Bakwata limesema Oktoba 29, siku ya kupiga kura kulizuka kundi lililokuwa likiwatisha watu, kupora na kuharibu mali, miundombinu mbalimbali ikiwemo kuchoma vitu vya mafuta na ofisi za umma.
Maandamano yaliyozua vurugu hizo yalianzia Dar es Salaam na baadaye katika baadhi ya mikoa kama Arusha, Mwanza, Mara, Mbeya na Songwe zilisababisha taharuki na madhara katika miji mikubwa na kuzua hofu na usumbufu wa shughuli za kila siku na kusababisha kuporomoka kwa mzunguko wa fedha.
Tamko hilo, la Bakwata lilitolewa jana Alhamisi Novemba 13,2025 kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu wa Baraza la Ulamaa la Bakwata, Sheikh Hassan Chizenga limeeleza uhalifu huo uligawanyika katika makundi mbalimbali ikiwemo wapo waliofurahia na waliochukizwa.
“Kutokana na vitendo hivi vya kihalifu, ililazimu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kudhibiti hali na ndani yake kukatokea vifo vya watu wasiokuwa na hatia,”.
“Wengine walipata ulemavu wa kudumu, pamoja na uharibifu, wizi na upotevu wa mali, yote haya yakisababishwa na kundi hiklo lililokuwa likifanya fujo, wizi na uharibifu mkubwa wa miundombinu,” imeeleza na Bakwata.
Kutokana na hilo, Bakwata inalaani vitendo vya klihalifu ambavyo udhibiti wake umesababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.
“Kwa umoja wetu tumeuamia sana kwa haya yalitokea hasa maisha ya watu kupotea kutokana na vitendo hivi vya kihalifu. Mafundidho yetu yanasema maisha ya mtu mmoja kupotea nis awa na kupoteza maisha ya watu wote,”
“Ndio maana kwa umoja wetu kabla ya uchaguzi mkuu tumefanya kazi kubwa ya kuhimiza umuhimu wa kuituza amani. Pale haki inapobidi kudaiwa, basi idaiwe kwa utaratibu usiovunja amani na kusababisha maafa makubwa,” imeeleza.
Bakwata imesisitiza kulaani vitendo vya kihalifu, likitokea wito kudhibitiwa na kuhakikisha havitokei tena katika Taifa letu,
Sambamba na hilo, Bakwata imeitaka Serikali kufanya uchunguzi kwa kina kuhusu vurugu hizo ili kubaini vinara wa kuchochoe vijana wa Tanzania kufanya uhalifu uliosababisha maisha ya watu kupotea.
“Tunaiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wamekubwa na maafa haya na wala hawakuhusika,”
“Katika kipindi hiki tunaisihi Serikali iangalie panapohitajika, kwa maslahi mapana ya nchi yetu.Panapohitaji Suluhu pafanyike kama mafundisho yetu yanayosema ‘Na Suluhu ni kheri’ surat annisaa aya ya 128,”
Pia, Bakwata limefafanua kuwa panapohitaji maridhiano basi Serikali iwe tayari kufanya hivyo kwa maslahi ya mapana na Tanzania na wananchi wake.
“Ingawa tunaisihi Serikali Suluhu na maridhiano isiwe ni zawadi wanayopewa wale wanaohusika na kushiriki katika uhalifu huu uliosababisha maafa haya,” imeeleza.