BAADA ya takribani miezi mitano kupita hatimaye pazia la Ligi ya Wanawake linafunguliwa rasmi leo zikipigwa mechi nne kwenye viwanja tofauti.
Kutokana na ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake ambayo ukanda wa Cecafa unawakilishwa na JKT Queens, mabingwa hao wa Bara hawataanza kulitetea taji lao hadi watakapoishia kwenye michuano ya CAF.
Msimu uliopita bingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, JKT Queens alitwaa taji hilo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kulingana pointi 47 sawa na Simba iliyomaliza katika nafasi ya pili. Yanga Princess ilishika nafasi ya tatu huku Mashujaa ikimaliza ya nne.
Msimu huu zimeongezwa timu mbili ambazo. zimefikisha idadi ya timu 12 badala ya 10 zilizoshiriki msimu uliopita.
Pazia la msimu linazinduliwa na mechi nne — Geita Queens ambao wamepanda Ligi Kuu msimu huu wataikaribisha Ceasiaa Queens, wakati mabingwa mara nne Simba Queens watakuwa KMC Complex kukipiga na Bilo Queens ambao pia ni wageni, huku Alliance Girls ikiivaa Fountain Gate na Ruangwa Queens ikicheza dhidi ya Yanga Princess kwenye Uwanja wa CCM Majaliwa Lindi.
Msimu uliopita mechi za awali zilishuhudiwa sare mbili Yanga ikitoka 1-1 na Bunda Queens mkoani Mara na Mashujaa ililazimishwa sare ya bila mabao na Gets Program.
Matokeo mengine Simba iliitoa kichapo cha mabao 3-0 kwa mabingwa walionyakua taji hilo kwa mara ya kwanza 2017 Mlandizi Queens ambayo msimu uliopita haikufanya vizuri ikiambulia pointi moja tu kwenye mechi 18 na kushuka daraja.
Mabingwa watetezi walianza na ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Alliance Girls. Sasa swali ni je wapinzani hao wa ligi ya wanawake wataanza kama msimu uliopita?
Kati ya timu tatu zenye ushindani Simba pekee imefanya maboresho makubwa kuanzia wachezaji ikisajili takribani nyota 13 wapya, ikimtimua aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Yussif Basigi na kusajili benchi jipya la ufundi.
Sababu ya kumtimua Basigi ni kushindwa kutimiza malengo ya timu ambayo walijiwekea ya kunyakua mataji ya ndani, Ngao ya Jamii na ligi ambayo yote yaliokwenda kwa wapinzani wao JKT Queens.
Msimu huu imerudi kivingine imepoteza Ngao ya Jamii tena mbele ya JKT, Je, itaweza kurudisha taji la ligi kuu? Tusubiri kuona.
Timu zilizomaliza ndani ya nafasi ya nne kwenye michuano ya ligi daraja la kwanza zote zimepata nafasi ya kupanda zikichukua nafasi ya Mlandizi Queens na Gets Program.
Timu hizo ni Bilo Queens, Ruangwa Queens, Geita Queens na bingwa wa ligi daraja la kwanza Tausi Queens ambazo zote ni mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu.
Ingawa ni mara ya kwanza lakini Tausi FC inaonekana kuwa timu iliyojipanga kuanzia kambi yao, usajili wa wachezaji wakubwa kama Adama Congo kutoka Burkina Faso ambapo baada ya kufanya vizuri ligi daraja la kwanza akapata dili la kuuzwa Dux Logrono ya Hispania.
Nyota wengine walioongezwa msimu huu ni pamoja na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ aliyeipa mafanikio makubwa wekundu hao wa kike.
Nyota wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ndiye kocha msaidizi akisaidiana na Maria Ruiz kutoka Hispania.
REKODI YA MASAKA ITAVUNJWA?
Ni msimu wa sita sasa rekodi ya Aisha Masaka aliyetimkia Brighton & Hove Albion ya England, imeshindwa kuvunjwa Ligi Kuu Wanawake ya kufunga mabao mengi.
Msimu 2020/21 Masaka aliibuka mfungaji bora wa WPL akiweka kambani mabao 35 akiwa mzawa wa mwisho kufunga mabao hayo.
Tangu hapo msimu uliofuata Mrundi wa Simba Queens, Asha Djafar alifunga mabao 27, msimu 2022/23 akachukua tena Mkenya, Jentrix Shikangwa akifunga mabao 17 na mwaka jana Aisha Mnunka wa Simba akiweka kambani mabao 20.
Ulikuwa msimu wenye ushindani kwa wachezaji wazawa kwani mfungaji bora alijulikana kwenye mechi za mwisho wa msimu.
Hadi mechi za mwisho Opah Clement wakati ule yupo Simba alikuwa na mabao 34 mechi ya mwisho iliamua Masaka anachukua kiatu baada ya kufunga hat-trick.
Hata hivyo baada ya kuondoka kwa nyota hao waliopata timu nje ya nchi hakukuwa na ushindani kwa wachezaji wazawa jambo linaloonyesha kuna pengo kwa washambuliaji hao. Msimu uliopita Stumai alikaribia kuifikia rekodi hiyo alimaliza kinara wa mabao akiweka kambani 28, swali ni je, msimu huu wataweza kuifikia au kuivunja? Hali hiyo inaonyesha namna gani wazawa wamekataa ushindani kwenye upachikaji mabao na badala yake wamemuachia mzigo Stumai.
Rekodi nyingine inayosubiriwa kwa hamu kuvunjwa au kufikiwa ni ya nyota wa zamani wa Simba Gaucho ambaye kwa sasa anaitumikia Tausi ya kufunga mabao mengi kwenye dabi.
Dabi ya wanawake kwa misimu ya hivi karibuni imekuwa ya kitofauti na msisimko wa aina yake, ule ufalme wa Simba kuifunga Yanga kila uchao ni kama unaondoka taratibu hivi.
Gaucho ndiye mshambuliaji pekee aliyeifunga Yanga mabao mengi tangu dabi ya wanawake ichezwe amefunga mabao 10.
Rekodi nyingine Gaucho huyo huyo alifunga hat-trick kwenye dabi ambayo haijavunjwa na mchezaji yeyote wa kigeni au mzawa.
10 – Idadi ya mabao aliyofunga Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ katika dabi
1 – Hat trick pekee iliyofungwa kwenye dabi na Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ wa Simba
Kiungo wa Simba, Vivian Corazone alisema baada ya kupoteza ubingwa msimu uliopita sasa msimu huu wamejipanga kurejesha taji hilo.
“Unajua ni ndoto ya kila mchezaji kuchukua ubingwa na kuwakilisha timu kwenye michuano ya kimataifa, tumepoteza msimu uliopita lakini huu tumejipanga kuurejesha.”
Kocha wa Alliance, Sultan Juma alisema msimu uliopita hawakuwa na maandalizi mazuri.
“Tunajua msimu huu utakuwa mgumu zaidi kwa sababu kuna timu mbili zimeongezwa kwa hiyo kila moja itahakikisha kupambana, mechi na Fountain haijawahi kuwa rahisi tunapokutana lakini sisi tunazihitaji zaidi pointi tatu.”