Dkt. GeorDavie Atemuliwa Balozi wa Afrika Mashariki na UN-PAF – Global Publishers


Nabii Mkuu na Kiongozi wa Kanisa la Ngurumo ya Upako jijini Arusha, Balozi Dkt. GeorDavie Moses, amepewa heshima kubwa kimataifa baada ya kuteuliwa rasmi kuwa Mwakilishi na Balozi wa Afrika Mashariki wa Shirika la Mabalozi wa Amani la Umoja wa Mataifa (UN-PAF).

Uteuzi huo ulifanyika Septemba 9, 2025 jijini New York, Marekani, na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Dunia wa UN-PAF, Balozi Kingsley Ossai, ambaye tayari ametuma barua rasmi za utambulisho kwa Serikali ya Tanzania, United Nations Chapter – Tanzania, pamoja na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ili kumtambua Dkt. GeorDavie katika nafasi yake mpya.

Kwa uteuzi huu, Dkt. GeorDavie anajiunga rasmi na mtandao wa viongozi wa kidunia wanaofanya kazi za kuhamasisha amani, mshikamano na maendeleo endelevu katika jamii.

Dkt. GeorDavie, ambaye pia ni Mlezi wa JMAT Taifa, amekuwa akitambulika kwa kazi zake za kiroho, kijamii na kiuchumi, zikiwemo programu za kuwawezesha vijana, wanawake na familia kujikwamua kupitia elimu, ujasiriamali na mafunzo ya thamani za kiutu. Shughuli hizi zimemfanya kuwa mmoja wa watetezi wa amani na maendeleo wanaotambulika kimataifa kutoka Tanzania.

Kwa mtazamo wa jamii ya kimataifa na wanaomfahamu katika eneo la Afrika Mashariki, matarajio ni kwamba wadhifa huu mpya utampa nafasi pana zaidi ya kuziwakilisha vyema nchi za Afrika Mashariki, kukuza ajenda za amani na kuendeleza jitihada za kuimarisha ustawi wa jamii kupitia UN-PAF.

Kwa upande wa waumini wake na watanzania kwa ujumla, uteuzi huu unaonekana kama hatua muhimu inayoonyesha jinsi mchango wake umeendelea kung’aa ndani na nje ya mipaka ya nchi.