Hekaheka ya kujinusuru wasio na makazi Oktoba 29

Dar es Salaam. Ni usiku wa Oktoba 29, 2025 mitaa ya Ubungo, wakati wengi wakiwa majumbani wamelala, wengine wakihangaika kusaka njia za usalama, Patrick Matano alikuwa bado barabarani akitafuta sehemu ya kujificha.

“Watu wengine waliniambia, ‘Dogo umefika, ujifiche,’ muda huo walikuwa wanasema ni saa 10:00 jioni,” anasema Matano (14), miongoni mwa vijana wasio na makazi wanaolala kwenye vibanda vya biashara vilivyopo Mwenge.

Anasema wakati huo sauti ya milio ya risasi ilisikika kwa mbali.

“Niliposikia milio ya risasi, niliingia kwenye mabanda ya watu ya biashara, nakaa huko nikiona pametulia natoka nje. Nikiona wameanza tena kurusha, naingia tena kwenye mabanda,” anasimulia katika mazungumzo na Mwananchi yaliyofanyika Novemba 11, 2025 eneo la Mwenge.

Matano anasema kwa siku zote sita alikuwa akiishi kwenye vibanda vilivyopo Mwenge.

Vibanda alivyokuwa anajificha Patrick Matano baada ya katazo la kutokuonekana nje kwa wananchi ifikapo saa 12 jioni na pindi aliposikia milio ya risasi na mabomu



“Kuna baadhi ya watu walikuwa wananiambia, ‘Dogo jifiche,’ kila inapofika saa 10:00 jioni. Nilikuwa najificha kwenye magari na wakati mwingine kwenye vibanda,” anasimulia.

Matano, aliyetokea mkoani Dodoma, anasema hakujua angekimbilia wapi, bali mabanda ya biashara yaliyotelekezwa yaligeuka kuwa kinga yake ya muda.

Kwa Matano anayefanya kazi ya kuosha vioo vya magari kwenye mataa yaliyo Mwenge na vijana wengine, maisha ya mitaani yalikuwa magumu hata kabla ya Oktoba 29. Lakini vurugu zilipoibuka, mitaa ikafungwa, magari kutosafiri na maduka kufungwa, hali ikawa ngumu maradufu.

Vijana wasiokuwa na makazi maalumu wakiwa wamelala chini ya daraja la Kijazi, Ubungo, jijini Dar es Salaam ambalo lilitumika kwa wao kujihifadhi kipindi cha vurugu za maandamano zilizotokea Oktoba 29, 2025



Katika kichaka jirani na taa za kuongoza magari njiapanda ya Sinza, Mwananchi lilifanya mazungumzo na baadhi ya vijana wasio na makazi waishio mtaani kujua yaliyojiri Oktoba 29.

Licha ya kuwa hali imerejea katika utulivu, eneo hilo bado walikuwapo vijana takribani saba, wakisikiliza muziki na kupiga hadithi za hapa na pale.

Abubakar Salum anakumbuka hali ile kama ndoto mbaya isiyoisha akieleza: “Tuliposikia milio ya risasi na mabomu, tulilala chini. Wakati mwingine tulijificha kwenye miti.”

Kichaka kilichopo pembezoni mwa mto Gide nyuma ya mitambo ya kufua umeme Ubungo, kilichotumiwa na vijana wasiokuwa na makazi maalumu kwa ajili ya kujificha kutokana na vurugu zilizosababishwa na maandamano Oktoba 29, 2025



Anasema ilivyo sasa hata sauti ya upepo humfanya ashtuke akihofia kurudi kwa milio ile ya risasi na mabomu.

Kwa upande wake, Jimmy Lioha, siku hiyo ilikuwa mwanzo wa mateso mengine akisimulia: “Tulikuwa Ubungo. Ilibidi tukimbie na kuingia mtoni kwenye vichaka. Huko tulitulia.”

Lakini utulivu haukudumu akieleza: “Wakati tupo huko, walitufuata, wakatukamata, wakatupiga halafu wakaondoka.”

Siku chache baadaye, anasema walijikuta baadhi yao wakikamatwa.

“Waliwakamata vijana, wakawapigisha push-up, wakawaambia wabebane. Ukishindwa unapigwa. Usipombeba mwenzako, wanakupiga. Siyo poa kabisa,” anasimulia.

Anasema mara ya mwisho walipofika mafichoni mwao, alikimbia kwa urefu wote wa miguu yake. Akapita kwenye vichaka, akajificha akitazama wenzake wakipigwa.

“Niliona wanavyowachukua, wanavyowapiga halafu wanaondoka nao. Nilikaa kimya, moyo ukidunda,” anasimulia.

Jimmy anasema baadaye alisikia kauli kutoka kwa wale waliokuwa wanakamata vijana: “Wapeleke walipo wenzao.”

Anaeleza waliingiwa hofu, wakakimbilia vichakani hadi walipokutana upya na wenzake waliokuwa wamesalia.

Vijana wasiokuwa na makazi maalum wakiwa kwenye pori lililopo jirani na taa za kuongozea magari barabara ya Sam Nujoma walilojificha kutokana na vurugu zilizotokea wakati wa maandamano Oktoba 29, 2025



Matano anasema alielezwa na watu kwamba anunue chakula cha kutosha, hivyo alinunua sahani mbili za wali akahifadhi.

Anasema chakula hicho alikula Oktoba 30 na 31 licha ya kuwa kiliharibika.

Anaeleza aliishi peke yake, hakujua ni wapi waliko wenzake akieleza kuwa ni mgeni jijini Dar es Salaam na eneo pekee analolifahamu ni Mwenge.

Omari, aliyehamia Dar es Salaam akitokea mkoani Tanga, anasema akiba ya fedha walizopata kutokana na kuosha vioo vya magari na msaada walioomba awali kutoka kwa wapitanjia, iliwawezesha kununua chakula.

“Tunashukuru Mungu tulikuwa tunajiwekea pesa. Lakini pia tulikula maembe na mapapai tuliyochuma kwenye kichaka hiki,” anasema.

Anasema iliponyesha mvua ilikuwa changamoto kwao kwani iliwalazimu kusimama chini ya miti.

Jimmy, aliyetoka mkoani Mbeya na maisha yake kuwa chini ya Daraja la Kijazi, Ubungo, anasema:

“Ukitaka kwenda dukani unapita kwa kunyoosha mtoni, unakwenda mbele huko unakuta maduka yamefunguliwa. Tulinunua unga wa dona kilo tatu na dagaa au mboga za majani,” anasema, akieleza kuna wakati walikaa bila kula siku mbili.

Anaeleza walikuwa wakichanga fedha kulingana na kile ambacho mtu alikuwa nacho, Sh2,000 hadi Sh3,000.

Vijana wasiokuwa na makazi maalumu wakiwa wamelala chini ya daraja la Kijazi, Ubungo, jijini Dar es Salaam ambalo lilitumika kwa wao kujihifadhi kipindi cha vurugu za maandamano zilizotokea Oktoba 29, 2025



Tofauti na wenzake, Mohamed Selemani, aliyefika Dar es Salaam akitokea Mwanza, anasema Oktoba 29 alipata msaada kutoka kwa muokota makopo aliyempeleka kwake, eneo ambako wanakusanya na kupima makopo.

“Waliposema mwisho wa kutembea saa 12:00 jioni, nikakutana na jamaa mmoja muokota makopo. Nikamueleza mimi ni mgeni nawatafuta wenzangu, akaniambia twende nyumbani kwake,” anasema.

Selemani anasema eneo hilo walikuwapo wauza chakula, hivyo mwenyeji wake alimpa chakula na nguo, huku akilala kwenye boksi lakini eneo lililozibwa lililo nje ya nyumba ya mwenyeji wake.

Anasema alikaa eneo hilo kwa siku nne hadi Novemba 2, alipoondoka na kurejea Daraja la Kijazi kuwatafuta wenzake, akaelekezwa wako eneo la uwanjani.

Huko uwanjani, eneo lililoko Ubungo, nyuma ya mitambo ya umeme, Steven Mungi anasimulia miongoni mwao yupo aliyekuwa na Kitambulisho cha Taifa (Nida), ndiye aliyetoka kwenda kutafuta chakula.

Mungi anasema alipokwenda dukani alitumia saa nzima kutokana na umbali, kwani alifuata eneo la Ubungo linalojulikana Kintintale.

Hata hivyo, anasema alipata chakula cha siku moja kutokana na wingi wa watu dukani hapo pamoja na kundi lao.

Wakati mvua iliponyesha, anasema walijificha kwenye mianzi jirani na Mto Gide, pia walitumia majiko ya kukaangia samaki kama mwamvuli.

New Content Item (1)


New Content Item (1)

Mungi anasema aliwapigia simu wazazi wake, akawaeleza alipo na hali halisi ya maisha yake.

Anasema wazazi wake walimtumia fedha za matumizi, wakimuhimiza arudi nyumbani.

“Niliwapigia wazazi wangu kuwaeleza kuwa nakula maembe, walichonieleza ni kwamba wanahitaji nirudi nyumbani, na walituma Sh15,000 kwa ajili ya kula hadi pale hali itakapokuwa imetulia,” anasema.

Kutokana na madhila aliyoyapitia, Matano naye anatamani kurudi nyumbani kwao Dodoma.

Anasema kwa sasa anapambana kutafuta fedha akiweka akiba kwa kidogo anachopata kutokana na kazi ya kuosha vioo vya magari ili apate nauli.

“Wazazi wangu wanajua nipo Dar es Salaam lakini hawajui naishi wapi na maisha ya aina gani. Nilipoongea nao kuhusu hali ya huku waliniambia nirudi,” anasema.

Kichaka kilichopo pembezoni mwa mto Gide nyuma ya mitambo ya kufua umeme Ubungo, kilichotumiwa na vijana wasiokuwa na makazi maalumu kwa ajili ya kujificha kutokana na vurugu zilizosababishwa na maandamano Oktoba 29, 2025



Sawa na maeneo mengine ambako vijana wasio na makazi hulala, saa nne usiku katika Barabara ya Uhuru, eneo la Kariakoo kwenye ukuta wa Shule ya Msingi Uhuru Wasichana, kulikuwa na kundi dogo la watu waliolala.

Rajabu Salum, ambaye hukusanya na kuuza makopo akiwa amelala kwenye boksi, akitumia kipande kingine kufukuza mbu, anasema:

“Tulikuwa tukilala ndani ya mitaa huko, wengine jirani na sokoni. Wakati askari wakipita tulikimbia kwa kupishana nao, wakipita upande mmoja tunazungukia mwingine, na wakati mwingine tuliingia kwenye mitaa ya ndani na vichochoro vya maduka ili tusionekane,” anasema.

“Mvua iliponyesha tulikimbilia kwenye magorofa yanayoendelea kujengwa, kwani kuna kingo zile za juu basi tunasimama hapo na wengine walienda kujificha kwenye vichaka eneo la relini,” anasema.

Anasema walipata msaada wa chakula kutoka kwa wakazi wa Upanga.

“Tulikwenda kuomba chakula, wakati mwingine tulijipenyeza kwenye Soko la Ilala, hasa usiku, kutafuta matunda yaliyotupwa kama maembe na ndizi.”