Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amelihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza leo Novemba 14, 2025.
Katika hotuba yake hiyo ametumia muda mrefu kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu vijana, ambao wenyewe wamekuwa wakiona kama wameachwa nyuma.
Rais Samia, ambaye ametumia hotuba yake hiyo kutoa mwelekeo mpya wa Serikali yake kwa muhula wa pili, amesema vijana watapewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kuanzisha wizara maalumu itakayojikita kutatua, kupanga na kuwawezesha vijana ikiwemo suala la changamoto ya ajira tofauti na ilivyo sasa.
Mara baada ya hotuba yake, wabunge wamezunguzia kile ambacho Rais Samia amekiahidi wakisema wanaona mwanga kwamba, changamoto za vijana zinakwenda kupata suluhisho.
Akizungumza baada ya hotuba hiyo, Mbunge wa Tunduma, David Silinde amesema hotuba ya Rais Samia imekuja na suluhisho kwa vijana kwani, ndiyo kizazi kinachotakiwa kuangaliwa zaidi.
Amesema mpango wa kuanzisha wizara kamili ya vijana utakuwa na manufaa makubwa kwa kuwa katika kipindi hiki kumeibuka kizazi ambacho hakisikii wala hakiambiliki.
“Rais amekuja na mwelekeo chanya wenye kuivusha Tanzania, nimefurahishwa na kauli ya kuunda wizara ya vijana ambapo, naamini matatizo mengi yatashughulikiwa moja kwa moja bila kupitia maeneo mengine,” amesema Silinde.
Silinde ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo katika muhula wa kwanza wa Samia, amewaomba viongozi watakaoteuliwa kuongoza wizara hiyo kuwa makini katika utekelezaji na usimamizi wa maono ya Rais ili Taifa liweze kusonga mbele.
Naye Dk Stephen Chaya (Mbunge wa Manyoni) amesema hotuba ya Rais Samia imejaa matumaini kwa Watanzania hasa kipindi hiki ambacho wengi wanataka nuru ya maisha.
Dk Chaya amesema tafsiri kubwa na neno lililomfurahisha ni ahadi kwamba, anataka kuacha nyuso za Watanzania zikiwa na tabasamu kipindi atakachokuwa anamaliza muda wake wa utumishi.
Amegusia pia uanzishwaji wa wizara mpya itakayoshughulikia mambo ya vijana kwamba itasaidia kupunguza matatizo makubwa ambayo yalitaka kuanza kuota mizizi.
Profesa Palamagamba Kabudi (Kilosa-CCM) amesema hotuba imejaa matumaini makubwa ambayo yanakwenda kujenga mshikamano na umoja wa Tanzania.
Profesa Kabudi amesema hotuba aliyoitoa Rais inajenga utu lakini inatoa mwelekeo wa kulinda mipaka ya nchi ambayo itasaidia kupeleka heshima kwa nchi na wananchi wake.
Mbunge wa Arumeru (Mashariki-CCM), Joshua Nassari amesema:”Nimefurahishwa na mwelekeo wa Serikali kuona umuhimu wa kuwaangalia vijana kwa jicho maalumu ikiwemo kuunda wizara ya vijana ili kutatua changamoto zao, ambao ni asilimia 60 mpaka 70 ya Watanzania.
“Maombi yangu, wizara ya vijana iongozwe na vijana kuanzia waziri mwenye dhamana mpaka watendaji wake. Hao ndio wanaojua issues (masuala) ya vijana kwa uhalisia wake, ndio wanaojua kilichopo mitaani na ndio watakaofikika kirahisi na vijana wenzao. Isije wizara ya vijana ikaongozwa na wazee.”
Kwa upande wake Mbunge wa Nanyumbu mkoani Mtwara, Yahya Mhata amesema kitendo cha Rais Samia kuwakumbuka waliopoteza maisha kwenye vurugu za Oktoba 29, 2025 na kuwataka wabunge wasimame dakika moja kuwaombea kimemgusa kwamba, ni kiongozi mwenye huruma kwa watu wake.
Amesema pia amefurahishwa na kitendo cha kuwaombea majeruhi wa vurugu hizo, lakini kubwa ni kitendo cha kuwasamehe walioingia kwenye vurugu hizo kwa mkumbo.
Pia, amesema kitendo cha Rais Samia kuzingumzia kuimarisha Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) katika ujenzi wa miundombinu ya barabara vijijini kitasaidia hasa kwenye jimbo lake la Nanyumbu.
Kwa upande wake Mbunge wa Ikungi Mashariki, Thomas Kitima amesema hotuba ya Rais Samia inakwenda kujibu matatizo ya vijana hasa katika suala la ajira.
Amesema hotuba hiyo imesheheni mambo mengi kuhusu utatuzi wa ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.
Kitima amesema katika masuala ya uchukuzi Rais ameeleza namna atakavyofanikisha ikiwemo uboreshaji wa viwanja vya ndege na anatamani kuona Singida nayo inakuwa na uwanja wa ndege.
Mbunge wa Simanjiro, James Milya amesema hotuba ya Rais Samia ni nzuri kwani, imegusia na kulenga kuwakwamua Watanzania wa kawaida katika hali yao duni ya maisha.
Milya amesema Rais Samia amefafanua kwa undani namna ajira milioni nane zitakavyopatikana ndani ya kipindi cha miaka mitano na kuwezesha vijana kupata ajira za uhakika. Lakini akataja suala la amani ya nchi alipowaasa vijana kutokubali kutumika na watu wenye malengo mabaya na Taifa.
“Hotuba imegusia suala la maboresho ya Katiba Mpya na muhimu zaidi kwenye maridhiano na mwafaka wa Taifa letu, lakini amewaomba wanasiasa kuepuka kupotosha malengo mazuri ya 4R kama baadhi walivyofanya hapo mwanzo,” amesema Milya.