Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu imesimamisha kwa muda usiojulikana usikilizwaji wa kesi ya Kocha Listoni Katabazi dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), akipinga kusimamishwa na TFF kujishughulisha na soka maisha yake yote.
Mahakama hiyo imesimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo baada TFF kukimbilia Mahakama ya Rufani, ilikokata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ambayo iliielekeza Mahakama ya Kisutu kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya Jana Alhamisi Novemba 13,2025 TFF kupitia wakili wake Oseah Chamba kuithibitishia kuwa wameshasilisha notisi ya rufaa hiyo kama ilivyoelekezwa
Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa Oktoba 21, 2025, na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga.
Hata hivyo TFF kupitia wakili wake Makubi Kunju iliieleza Mahakama ya Kisutu kuwa haiko tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo kwa kuwa inakusudia kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuamuru kesi hiyo iendelee kusikilizwa.
Alipoulizwa kuwepo notisi ya rufaa kama uthibitisho, Wakili Kunju alijibu kuwa mpaka siku hiyo hazikuwepo kwa kuwa bado walikuwa ndani ya muda wa kuwasilisha notisi hiyo.
Hivyo Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo mpaka Novemba 13, 2025, huku akiwaelekeza mawakili wa TFF kuwasilisha uthibitisho wa rufaa hiyo, huku akitahadharisha kwamba kama watashindwa kufanya hivyo mahakama itaendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.
Jana Wakili Chamba aliieleza Mahakama kuwa wameshawasilisha mahakamani notisi hiyo na kwamba tayari wameshampatia mlalamikaji, Kocha Katabazi, ingawa alisema kuwa bado walikuwa hawajaipandiaha kwenye mfumo wa Mahakama wa usajili mashauri.
Kocha Katabazi ambaye alikuwepo Mahakamani hapo alikiri kupokea notisi hiyo
Mahakama hiyo baada ya kupokea ushahidi huo, sasa imesimamisha usikilizaji wa kesi hiyo kusubiri uamuzi wa rufaa hiyo, ambayo haijulikani ni lini itasikilizwa na lini itaamuliwa.
“Kwa mujibu wa taratibu, baada ya kuwasilishwa kwa notisi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Juu, mahakama hii inakosa mamlaka ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo. Hivyo shauri hili linasimama mpaka hapo Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wa rufaa hiyo”, amesema Hakimu Kiswaga.
Pia Hakimu Kiswaga ameelekeza wakili wa TFF ahakikishe notisi hiyo inawekwa kwenye mfumo wa Mahakama.
Kocha Katabazi anayejitambulisha kuwa mdau wa soka na kocha wa mchezo huo mwenye leseni ya daraja C, iliyotolewa na TFF, alifungua kesi hiyo dhidi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa TFF na TFF yenyewe mwaka 2024.
Alifungua kesi hiyo baada ya kufungiwa na TFF kujishughulisha na soka ndani na nje ya nchi maisha yake yote, kufuatia barua aliyoliandikia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Juni 15, 2021, akiilalamikia TFF kushindwa kusimamia soka kulingana na Sheria, Kanuni na miongozo yake.
Kutokana na barua hiyo aliitwa katika Kamati ya Maadili ya TFF, lakini hakuhudhuria akijibu kuwa yeye si mwanachama wa TFF kwani si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF.
Hivyo Juni 24, 2021 TFF lilichapisha katika tovuti yake uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi, ndipo akafungua kesi hiyo.
Katika kesi hiyo ya madai namba 14708/2024, Kocha Katabazi alidai kuwa Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kumpa adhabu hiyo kwani Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.
Alidai kuwa kanuni hizo hazijasajiliwa na BMT kulingana na matakwa ya Sheria ya BMT namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake, hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika kwa wanachama wake na mtu mwingine yeyote.
Pia alidai kuwa amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake, na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.
Hivyo aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi huo wa kumfungia maisha uliotolewa kwa maksudi, kimakosa na kwa nia ovu.
Pia aliomba alipwe Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa uamuzi huo wakijua kuwa hawana mamlaka ya kisheria kumchukulia hatua hiyo, riba ya kiwango cha Mahakama kwa tuzo (fedha ambazo ingeamuriwa alipwe) na gharama za kesi.
Vilevile aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Katiba na Kanuni za Maadili za TFF, akidai kuwa si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.
Kocha Katabazi aliwasilisha mahakamani hapo barua ya BMT ya Juni 13, 2022 iliyothibitisha kuwa yeye si mwanachama wa TFF.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Kiswaga, iliifuta kesi hiyo baada ya kukubaliana na pingamizi la TFF.
Hakimu Kiswaga alikubali kuwa Katabazi ni mwanachama wa TFF na kwamba kwa Katiba ya TFF, alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili, na asingeridhika anaweza kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Hivyo alikubaliana na TFF kuwa kwa kuwa Katabazi hakufuata utaratibu huo, mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Katabazi alikata rufaa Mahakama Kuu akiwakilishwa na wakili Peter Majanjara pamoja na sababu nyingine, akidai kuwa pingamizi la wajibu rufani halikuwa na msingi wa kisheria kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa kwenye pingamizi hilo.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Butamo Jaji Phillip Septemba 26, 2025, alikubalina na Rufaa hiyo, hivyo akatengua uamuzi wa Kisutu, ndipo ikaiamuru jalada lirejeshwe Kisutu iendelee kuisikiliza madai ya msingi.