Kisukari tishio, Tanzania yataja mikakati

Dar es Salaam. Idadi ya wagonjwa wa kisukari duniani imepanda kwa kasi isiyokuwa ya kawaida, ikifikia zaidi ya watu milioni 800 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara nne ikilinganishwa na miaka ya 1990. 

Ripoti mpya ya jarida maarufu duniani la afya The Lancet, kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO), inaonya kuwa hali hii ni tishio jipya  linalokua haraka, hasa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati kama Tanzania.

Wataalamu wanasema ongezeko la unene, lishe duni, na kupungua kwa mazoezi ya mwili vimekuwa chanzo kikuu cha ongezeko la kisukari duniani.

Kwa upande wa Tanzania, ripoti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2025/2026 inaonyesha kuwa jumla ya wagonjwa wanaougua ugonjwa huo ni 646,474. 

Ongezeko hili linatokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha, lishe duni, na vikwazo vya kiuchumi vinavyoathiri maisha ya Watanzania.

Sababu za kisukari Tanzania

Wataalamu wa afya wanasema sababu kubwa ya Watanzania kupata ugonjwa wa kisukari ni mabadiliko ya mtindo wa maisha, unene uliokithiri, lishe duni, kutofanya mazoezi na changamoto za kiuchumi. 

Mwenyekiti wa Chama cha Kisukari Tanzania, Dk Andrew Musa Swai, anasema  kati ya watu 100, tisa wanaugua kisukari na waathirika wakubwa ni kuanzia miaka 30 na kuendelea. Anasema  idadi hii haijawahi kushuka na inaendelea kuongezeka kila mwaka.

“Kuongezeka kwa idadi ya watu wanaougua kisukari siyo Tanzania pekee; ni duniani kote. Inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya watu duniani wana kisukari, na hii inatokana na unene, lishe duni, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, mawazo, na tamaa,” anasema.

Jinsi ya kukabiliana na kisukari

Dk Swai anasema kuwa njia bora ya kukabiliana na ugonjwa huu ni kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kuzingatia lishe bora, na kupunguza ulaji wa vitu vyenye sukari nyingi, kupunguza unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara. 

Kwa upande mwingine, Meneja Miradi kutoka Tanzania Diabetes Association (TANCDA), Renatus Nyarubamba, anaeleza kwamba takribani seli zote za mwili wa binadamu,  huhitaji sukari ili kuzalisha nishati na kufanya kazi.

Akifafanua kuhusu makundi ya ugonjwa huo, anasema kuna kisukari aina ya kwanza ambacho kinaathiri watu wa umri mdogo hasa watoto.

“Kisukari aina ya pili, ambacho kinatokea kwa watu wazima na ni aina inayohusisha zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wa kisukari duniani. Mambo kama mtindo duni wa maisha na unene ni miongoni mwa sababu kuu,” anasema Dk Nyarubamba.

Anaendelea kusema kwamba kipo kisukari cha mimba, ambacho hutokea wakati wa ujauzito na mara nyingi hupotea baada ya kujifungua, lakini huongeza hatari ya kupata kisukari cha aina ya pili baadaye maishani.

Takwimu kutoka Chama cha Kisukari Tanzania zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto na vijana 7,130 wenye kisukari aina ya kwanza, wamenufaika na huduma zinazotolewa bure katika kliniki 85 zilizojengewa uwezo wa kutoa huduma kwa kundi hili.

Huduma hizi zimeongeza upatikanaji wa insulin, vifaa vya kupima sukari, na elimu kuhusu ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza. Mikakati hii inasaidia kupunguza mzigo wa ugonjwa huu, lakini bado kuna changamoto za kimkakati na kifedha zinazohitaji juhudi za ziada.

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Tamisemi inashirikiana na wadau mbalimbali ili kutekeleza mikakati ya kudhibiti ongezeko la kisukari. Mikakati hiyo inajumuisha kutoa elimu kwa jamii, kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisukari katika ngazi zote za mfumo wa afya, kuboresha uwezo wa watumishi wa afya, na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa vya matibabu.

Serikali pia inahamasisha mazoezi ya mwili, lishe bora, na kupinga uvutaji wa tumbaku na unywaji wa pombe. 

Sambamba na hayo, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kufanya utafiti ili kutambua ukubwa wa changamoto ya kisukari na kubuni mikakati bora zaidi ya kupambana na ugonjwa huu.

Bima ya afya kwa wote ni mkakati muhimu katika kuhakikisha watu wote, wakiwemo wanaoishi na kisukari, wanapata huduma bora za afya.

 Hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Ufuatiliaji wa kisukari duniani

Katika hatua nyingine, WHO imezindua mfumo wa kimataifa wa ufuatiliaji wa kisukari ambao utasaidia mataifa kufuatilia, kutathmini, na kuboresha juhudi za kinga na matibabu.

Nchi zote zinahimizwa kuhakikisha kwamba angalau asilimia 80 ya wagonjwa wanadhibiti kiwango cha sukari ipasavyo ifikapo mwaka 2030.

Kupitia mfumo huu, ujumbe mkuu unabaki kuwa lishe bora, mazoezi ya mwili, uchunguzi wa mapema, na mifumo ya afya inayozingatia kinga kama  silaha pekee za kuzuia janga hili lisigeuke kuwa tatizo kubwa la kimataifa. 

Kwa hapa nchini, Serikali na wadau wanaendelea kubuni mikakati zaidi ili kupambana na kisukari na kuokoa maisha ya Watanzania.