Kocha wa Gusa Achia apiga mkwara mzito CAF!

KOCHA wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic ambaye kwa sasa anainoa CR Belouizdad ya Algeria ameichimba mkwara Singida Black Stars ikiwa ni siku chache kabla mechi ya kwanza ya hatua ya makundi kati ya timu hizo katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya wiki ya kalenda ya FIFA, Novemba 22, CR Belouizdad itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa August 20 1955 kuikaribisha Singida Black Stars ambay inanolewa na Miguel Gamondi ambaye naye aliwahi kuinoa Yanga.

Kocha huyo, Mjerumani amesema uzoefu ambao aliupata wakati akigundisha soka nchini anaamini utakuwa msaada wake wakati ambao atakuwa akikabiliana na timu hiyo ambayo kwa mara ya kwanza inashiriki michuano ya kimataifa.

“Najua Singida ni timu mpya kwenye michuano hii, lakini hawatakuja hapa kutembea. Wanakuja kupambana na nami pia nataka hilo. Uzoefu wangu Tanzania najua utasaidia. Najua aina yao ya uchezaji ilivyo, nimeiona ni moja ya timu shindani,” amesema Ramovic na kuongeza;

RAMO 01


“Tunawaheshimu, lakini hatutawaacha wapumue. Hapa ni nyumbani kwetu na tutajua namna ya kuwakaribisha.”

CR Belouizdad ikiwa chini ya Ramovic ipo nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu Algeria ikiwa na pointi 14 baada ya mechi tisa, imefunga mabao 10 na kuruhusu saba, timu hiyo imeshinda mechi mbili kati ya tano zilizopita. Kijumla timu hiyo ya mzee wa gusa achia, imeshinda mechi tatu, sare tano na kuchapwa moja tu.

Singida Black Stars kwa upande wake ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi saba, baada ya mechi tatu, imeshinda mbili dhidi ya Mashujaa (1-0), KMC (1-0) na kutoa sare moja dhidi ya Pamba Jiji kwa bao 1-1.

RAMO 02


Wakati Singida Black Stars ikianzia raundi ya kwanza ya hatua ya awali kwa kushinda nyumbani na ugenini dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1, CR Belouizdad ilianzia raundi ya pili na kuing’oa Hafia ya Guinea kwa jumla ya mabao 3-1 na kutinga hatua ya makundi.

Singida Black Stars ilitinga hatua hiyo baada ya kuichapa Flambeau du Centre ya Burundi katika raundi ya pili kwa jumla ya mabao 4-2.