Januari 2026, tunaanza awamu nyingine ya miaka mitano ya uongozi, huku wastaafu tukiendelea kuhaha na pensheni yetu ya shilingi laki moja na elfu hamsini tuliyoanza kupata kuanzia Januari 2025, katika kile tulichoaminishwa na Siri-kali kwamba ni kuboresha maisha ya mstaafu! Laki moja na elfu hamsini!
Wastaafu wanaoweza kuboresha maisha yao kwa shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi wanyooshe mikono yao, tafadhali… Hakuna! Hakuna mstaafu hata mmoja aliyenyoosha mkono. Hii ikiwa ni ujumbe muhimu kwa wahusika kwamba hakuna mstaafu anayeweza kuishi kwa shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi!
Naomba niweke sawa hapa, hakuna muajiriwa, rudia hakuna muajiriwa hata mmoja anayeweza kuishi kwa shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi. Hakuna!
Haieleweki kwa nini Siri-kali inataka kutuaminisha kuwa mstaafu aliyelijenga na kuipigania nchi hii anaweza kuishi kwa muujiza wa shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi, wakati miujiza iliisha tangu enzi za Agano Jipya, na sasa tumebaki na “miujiza” ya kununua maji, mafuta na leso!!
Bunge jipya limeanza kazi, na pamoja na kutopewa mwakilishi kwenye viti maalumu apigie kelele yale yanayowahusu wastaafu, wanatumaini kuwa Bunge hili litajitofautisha na Bunge lililomaliza miaka mitano yake, ambalo halikuzungumza chochote kinachohusu nyongeza ya pensheni kwa wastaafu!
Sana sana Bunge likaishia kupitisha fasta muswada wa pensheni inayoeleweka kwa wenza wa waheshimiwa, huku wenza wa wastaafu wa kima cha chini wakiishia kubamizwa na tozo na kikokotoo kisichowahusu.
Ndiyo, kikokotoo na tozo kibwena, huku tukiaminishwa kwamba tuna vyama kibwena vya wafanyakazi, na Bunge likiishia kuunga mkono hoja na kushangilia kwa kuzaba makofi meza badala ya kuzaba makofi wanaohusika na kupanga pensheni!
Tunatumaini kuwa Bunge hili jipya litajitofautisha na Bunge la miaka mitano iliyopita, la miaka kumi iliyopita, la miaka kumi na tano na miaka ishirini iliyopita, bila hata kukohoa chochote kuhusu pensheni njiwa ya mstaafu….
…ambayo imedumu kwa miaka 20, wastaafu wakipata shilingi laki si pesa, na Bunge liko tu likipiga makofi meza badala ya kupiga makofi mashavu na machafu ya wahusika ili kuwaamsha wamkumbuke mstaafu wa Taifa.
Pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini kwa mwezi ni mzaha mkubwa kwa wastaafu. Shilingi laki tatu kwa mwezi angalau itasaidia-saidia, wakati tukijitahidi kuirejesha “matibabu ya bure kwa wazee wa zaidi ya miaka 60” iliyopotelea kwenye khanga!
Enzi zile shule zilipokuwa shule kweli, tulifundishwa methali kama ile njema isemayo: “Mvumilivu hula mbivu.” Ni matumaini yetu sisi wastaafu kwamba wahusika, Bunge jipya na mhusika mkuu hawatatufanya tuibadili methali hiyo muhimu kuwa: “Mvumilivu huishia kula vilivyooza.”
0754 340606 / 0784 340606