Mahakama yaiamuru kampuni ya Masai kulipa zaidi ya Sh13.78 milioni

Arusha. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Tanga imemwamuru Jonas Ihashe, anayeendesha biashara kwa jina la Masai Utalii Company Limited, kulipa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wake kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili, yenye thamani ya zaidi ya Sh13.78 milioni.

Fedha hizo ni malimbikizo ya michango ya wafanyakazi kwa kipindi kuanzia Mei, 2022 hadi Septemba 2024.

Maombi ya madai hayo namba 30136/2024 yaliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Bodi ya Wadhamini wa NSSF dhidi ya Jonas kupitia kampuni hiyo ya utalii.

Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 12, 2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Katarina Mteule, ambaye alisikiliza shauri hilo na nakala ya uamuzi ikawekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Katika maombi hayo, wadai waliiomba Mahakama imwamuru mdaiwa kulipa Sh13.78 milioni, kati yake Sh12.28 milioni ni michango ya wanachama na Sh1.49 milioni ni faini za kuchelewa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, waliiomba Mahakama kutoa amri nyingine yoyote itakayoonekana inafaa pamoja na kuwalipa gharama za shauri.

Wadai walieleza kuwa licha ya wajibu wa kisheria alionao, mdaiwa alishindwa kuwasilisha michango hiyo kwa mujibu wa sheria katika kipindi tajwa.

Baada ya kusikiliza hoja zote, Mahakama ilibaini kuwa mdaiwa alishindwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria, hivyo ikaamuru alipe zaidi ya Sh13.78 milioni pamoja na gharama za kesi.

Huu ni mwendelezo wa hukumu zinazotolewa na Mahakama dhidi ya waajiri wanaokiuka sheria baaada ya Novemba 11, 2025 Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kuimuru Kampuni ya SCI Tanzania Limited kuilipa NSSF Sh2.3 bilioni za michango ya wafanyakazi pamoja na faini za kati ya Machi 2021 hadi Julai 2024.

Maombi hayo pia yalifunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bodi ya Wadhamini wa NSSF dhidi ya kampuni ya SCI Tanzania Limited.

Ilielezwa mahakamani kwamba mdaiwa alishindwa kuwasilisha michango inayofikia Sh1.64 bilioni faini Sh685.2 milioni.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani, Jaji Kirekiano aliamuru kampuni hiyo kulipa jumla ya Sh2.3 bilioni, ikiwa ni malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wake.

NSSF kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, iliwasilisha madai hayo baada ya barua ya kumbusho iliyopelekwa kwa kampuni hiyo Septemba 2, 2024, ikitaka kutekelezwa wajibu wa kisheria juu ya utumiaji wa michango ya wanachama, kushindikana.

Katika maombi hayo, wadai waliiomba Mahakama iiamuru kampuni hiyo kulipa deni malimbikizo na faini hizo.

Pia waleta maombi waliomba riba ya asilimia tano kwa mwezi inayotozwa kwa mwajiri anayechelewesha michango, hadi deni lote litakapolipwa.