Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inatarajia kukusanya takribani Sh800 milioni kwa mwaka kupitia mradi wa kilimo cha parachichi, hatua inayotarajiwa kuchochea uchumi wa wananchi na kufungua fursa za ajira kwa vijana.
Imebainishwa kuwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ambazo kwa pamoja huchangia zaidi ya asilimia 67 ya pato la halmashauri hiyo, zinaendelea kupewa kipaumbele kwa kuweka mazingira rafiki ili wananchi wanufaike na shughuli wanazozifanya.
Akizungumza leo Ijumaa, Novemba 14, 2025, ofisini kwake, Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa halmashauri hiyo, Gidion Mapunda amesema kupitia mradi wa zao la parachichi ulioanzishwa wilayani humo, wanatarajia kuvuna mapato ya Sh800 milioni.
Amesema shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 200 limefanikiwa kutoa ajira za muda kwa vijana na pia litakuwa kituo cha mafunzo kwa wananchi wa maeneo jirani, akibainisha kuwa soko la zao hilo ni la uhakika.
“Kwa sasa bei ya parachichi ni Sh2,500 kwa kilo. Tunatarajia mradi huu kuwa kichocheo cha uchumi wa halmashauri, kufungua fursa za ajira kwa vijana na kutoa elimu kwa wakulima,” amesema Mapunda.
Akizungumzia hali ya uzalishaji wa chakula, Mapunda amesema Wilaya ya Mbeya ina uwezo wa kuzalisha hadi tani 600,000 za mazao ya chakula na biashara, wakati mahitaji ya wilaya ni tani 157,000 pekee.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea na usanifu wa mabwawa wilayani humo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza tija kwa wakulima.
“Mbali na mradi wa parachichi ambao ni kitega uchumi cha halmashauri, zao linaloongoza kwa kuchangia mapato ni viazi mviringo, ambalo kwa mwaka huingiza zaidi ya Sh1 bilioni. Serikali inaendelea kuhakikisha bei ya mazao inakuwa rafiki kwa mkulima ili kuboresha maisha,” amesema.
Mapunda amesema Halmashauri ya Mbeya inaongoza kwa usajili wa wakulima katika mfumo wa ruzuku bila urasimu, na amewashauri wakulima kupima afya ya udongo kwani watafiti kutoka Tari Uyole wapo tayari kutoa huduma hiyo.
Kwa upande wa sekta ya mifugo, Mapunda amesema wanaendelea na utekelezaji wa mpango wa uchanjaji wa ng’ombe na mbuzi ili kuwaweka kwenye kanzidata kwa lengo la kudhibiti wizi wa mifugo.
“Serikali imetoa ruzuku kwa ajili ya chanjo. Halmashauri inatarajia kuchanja ng’ombe 200,000 kwa Sh500 kila mmoja, na mbuzi 5,000 kwa Sh300,” amefafanua.
Mmoja wa wafugaji wa wilaya hiyo, Asyumwisye Mwangoka amesema uchanjaji umeimarisha usalama wa mifugo yao kwani mifugo ikipotea hutambulika kirahisi popote ilipopelekwa.
“Hata akitokea mtu akaiba na kupeleka nje ya Mbeya, atakamatwa. Mfumo huu umetuwekea usalama na kupunguza gharama kupitia ruzuku. Awali kuchanja ng’ombe mmoja kuligharimu zaidi ya Sh50,000, lakini sasa ni Sh500 tu,” amesema Mwangoka.
Naye Charles Wiliam amesema kipaumbele kinachotolewa na Serikali katika sekta ya kilimo kinaongeza heshima kwa wananchi ambao wanategemea kilimo kwa zaidi ya asilimia kubwa ya kipato chao.
“Tuombe halmashauri izingatie upatikanaji wa masoko, kwani Mbeya Vijijini tunalima mazao mengi ya biashara na chakula. Itasaidia kufungua masoko ndani na nje ya nchi ili kuinua uchumi wetu na wa Taifa,” amesema Wiliam.