Mrundi apewa rungu TRA United

MABOSI wa TRA United zamani Tabora United, wapo hatua za mwisho za kumtangaza kocha mkuu Etienne Ndayiragije, raia wa Burundi ili kukiongoza kikosi hicho msimu huu, huku akiachiwa msala wa kutafuta atakayekuwa msaidizi wake.

Chanzo cha habari kutoka timu hiyo, kililiambia Mwanaspoti, Ndayiragije aliyezifundisha Mbao FC, Azam FC, KMC na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ameamriwa kuamua kama atafanya kazi na kocha msaidizi aliyepo, Mkenya Kassim Otieno aliyeanza nayo msimu huu.

“Uamuzi wa nani atafanya naye kazi hilo litabaki jukumu lake kwa sababu hatutaki kumwingilia, tunachohitaji sisi kama uongozi ni kuona timu inacheza soka safi na la kuvutia na kiukweli hatuna shaka na uwezo wake,” kilisema chanzo hicho.

Kiongozi huyo amesema miongoni mwa mapendekezo yao ni kuhakikisha Ottieno anaendelea kusalia katika kikosi hicho, ila kama Ndayiragije ataamua vinginevyo watasikiliza hoja zake, japo kwa sasa hawataki kuingilia katika utendaji kazi wake.

Kwa msimu huu wa 2025-2026, Ottieno ameiongoza TRA United katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara, ambazo ametoa zote sare, akianza na ya mabao 2-2, dhidi ya Dodoma Jiji, Septemba 20, 2025, kisha suluhu (0-0) na Pamba Jiji, Septemba 28, 2025.

Mechi nyingine ni ya suluhu pia (0-0), dhidi ya maafande wa Mashujaa Oktoba 22, 2025 na timu hiyo ikiwa chini ya Ottieno inashika nafasi ya 15 na pointi tatu, huku kikosi hicho kikifunga mabao mawili na kuruhusu mawili.

Ndayiragije anajiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Kenya Police FC ya Kenya, Oktoba 29, 2025, baada ya kudumu kwa siku 333, tangu ateuliwe kikosini humo, huku akikipa ubingwa kikosi hicho wa Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ msimu wa 2024-2025.

Kocha huyo aliipa Kenya Police ubingwa huo ukiwa ni wa kwanza kwa kikosi hicho katika historia tangu kilipopanda daraja mwaka 2021, hivyo, kuzima utawala wa Gor Mahia iliyochukua mara mbili mfululizo kuanzia msimu wa 2022-2023 na 2023-2024.