Mtunisia aichorea ramani Yanga kwa Waarabu

KOCHA wa zamani Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Nasreddine Nabi amekiangalia kikosi cha Yanga kinachojiandaa kuipokea AS FAR Rabat ya Morocco, kisha akakipa tahadhari kihakikishe mechi na Waarabu hao inashinda nyumbani.

Yanga iliyopangwa Kundi B pamoja na klabu tatu za Afrika Kaskazini, Al Ahly ya Misri, AS FAR Rabat na JS Kabylie ya Algeria, itaanzia nyumbani dhidi ya Wamorocco Novemba 22, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kabla ya kuwafuata Waalgeria wiki moja baadaye.

Kwa kutambua ugumu iliyonayo Yanga dhidi ya timu hizo tatu za Waarabu, Nabi ameipa madini timu hiyo ya Jangwani aliyoifikisha katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya sare ya 2-2. Yanga ilianza kwa kipigo cha 2-1 nyumbani kisha kushinda ugenini kwa bao la penalti la beki Djuma Shaban.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi amesema katika mechi ya kwanza ya makundi ni lazima Yanga ipambane sana kuhakikisha inatoka na pointi tatu nyumbani kujiweka katika mazingira mazuri kabla ya kuifuata JS Kabylie na kusubiri mechi mbili za mapema mwakani 2026 dhidi ya Al Ahly.

Nabi amesema, kama Yanga inataka kuanza vizuri lazima ianze kwa ushindi nyumbani, kwani maafande hao wa jeshi kutoka Morocco watakuwa nchini kwa nia ya kujilinda zaidi.

“AS FAR Rabat itakuja kwa tahadhari juu ya Yanga wakiwa ugenini, lakini kama watashindwa kufanya vizuri mechi hiyo watajiweka kwenye presha kubwa. Kwa sababu sheria ya Waarabu ni kumchakaza mgeni kwao, hivyo kama ikishindwa tu kutamba nyumbani, basi Morocco watacheza kwa tabu sana.”

Wakati Nabi akiipa maujanja Yanga, lakini wawakilishi hao wa Tanzania wana kikwazo kingine kwa AS FAR Rabat ambaye ni kocha wa makipa wa zamani wa klabu hiyo ya Jangwani, Alae Meskini anayeinoa timu hiyo ya Morocco aliyojiunga nayo mwanzoni mwa mwaka huu.

Kocha huyo anawafahamu mastaa wengi wa Yanga, kwani alikuwa nao wakati akifanya kazi akiwa na Kocha Miguel Gamondi aliyepo Singida Black Stars kwa sasa, hivyo huenda akauza faili la Wanajangwani na kuwapa ugumu wenyeji kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.