Samia aanza na onyo kwa watendaji

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu amewatangazia hali ya hatari watumishi na watendaji wa Serikali watakaoshindwa kwenda na kasi ya kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi.

Amesema hatosita kuwabadilikia wale wote watakaokwenda kinyume na kasi ya utendaji wa Serikali yake inayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi.

Akizungumza leo wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma ikiwa ni ufunguzi wa Bunge la 13, Samia amesema ahadi zilizotolewa na chama chake wakati wa kuomba kura ni nyingi hivyo zinahitaji watu wenye kasi kuzitekeleza.

“Niliahidi Serikali nitakayoiunda itawajibika na kuendelea na mageuzi ya sera zinazogusa masilahi na ustawi wa maisha ya wananchi moja kwa moja. Hivyo basi ni lazima viongozi wa Serikali kwa ngazi zote kuanzia mawaziri hadi maofisa tarafa wawe karibu na wananchi ili kuweza kufahamu changamoto zao na kuwajibika kwao.

Amesema kwa kuwa ahadi zilizotolewa na chama chake ni  nyingi, matamanio na matarajio ni makubwa na muda wa kuyatimiza ni mchache hivyo ipo haya ya Serikali yake kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ili kufikia  malengo.

“Nayasema haya mapema kwa watendaji waliopo serikalini  na wale nitakaowateua wajitayarishe kisaikolojia na wajipange vyema kufanikisha malengo hayo. Wananchi wanahitaji mabadiliko chanya ili kupata maendeleo hivyo watendaji msipobadilika kuendana na matarajio ya wananchi tutawabadilikia,”amesema Samia.

Kauli hiyo pia ilitolewa jana na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba muda mfupi baada ya kuthibitishwa na Bunge, kuwa Waziri Mkuu mteule, kabla ya kuapishwa kuwa Waziri Mkuu kamili.

Akizungumza wakati wa kushukuru mbunge huyo wa Iramba Magharibi mkoani Singida, mbali na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wabunge wote ikiwamo wa kambi ya walio wachache bungeni, lakini ametoa onyo kwa watumishi wazembe na wala rushwa.

“Watumishi wavivu, wazembe na wala rushwa nakuja na fyekeo na rato lazima kila mmoja awajibike na tutekeleze ahadi alizozitoa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, watumishi na Watanzania wote lazima twende na gia ya kupandia mlima cha msingi ni kuwa chombo kifike salama,” alisema Mwigulu.

Dk Mwigulu alisema katika uongozi wake atahakikisha watumishi wa umma wanatenga muda wa kuwasikiliza wananchi na inapobidi lazima waondoke maofisini waende wakatatue kero za watu.

“Watanzania wa mazingira ya chini watasikilizwa kwa nidhamu katika ofisi za umma, tutahakikisha watumishi wanakwenda kutatua kero za wananchi katika maeneo yao, lakini Dira ya Taifa ya Maendeleo imebeba matumaini makubwa ya Watanzania na kazi ni kubwa, twendeni tukaisimamie,” alisisitiza huku akionya Dk Nchemba.